POINTI TATU ZAIPELEKA SIMBA FIFA

POINTI TATU ZAIPELEKA SIMBA FIFA

6493
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

HUENDA sakata la Simba kupokonywa pointi tatu likawakimbiza Wekundu hao wa Msimbazi hadi Uswizi, yalipo makazi ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), kudai haki yao baada ya mwenyekiti wao wa zamani, Ismail Aden Rage, kuwashauri kufanya hivyo.

Rage, ambaye pia alikuwa katibu mkuu wa TFF, wakati huo ikijulikana kama FAT, amesema maamuzi yaliyofanywa dhidi ya Simba yanaonyesha dhahiri uonevu na kwamba wakienda Fifa na Shirikisho la Afrika (CAF), watapata msaada.

Alisema kuwa, sababu walizotoa TFF kwenye sakata hilo hazikuwa na mashiko yoyote, hivyo Simba wanaweza kuomba kutafsiriwa sheria FIFA na CAF na wakakubaliwa.

“TFF wamekubali kama Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano na atakosa mchezo unaofuata, hii sheria ni mpya, maana tunazozijua sisi, hasa ile ya kanuni namba 42 (11) inasema mchezaji mwenye kadi tatu za njano haruhusiwi kucheza mchezo unaofuata, lakini kama Simba walikuwa hawajalipa ada au rufaa yao imechelewa, kwanini wasingeitupilia mbali kama kanuni zinavyoelekeza?

“Hii kanuni ya kusema Fakhi atakosa mchezo unaofuata ni mpya na haipo kokote kule, tunajua TFF ina uwezo wa kufanya marekebisho kwenye vifungu vyake vya katiba, ila si mwishoni mwa ligi, mimi nawashauri waende FIFA kutafuta haki yao,” alisema.

Rage alikwenda mbali zaidi kwa  kuishangaa TFF wanaposema rufaa ya Simba ilikuwa nje ya wakati, kwani kwenye kanuni za Ligi kuna maamuzi mengine hayahitaji kukatiwa rufaa.

“Kanuni za Ligi Kuu kipengele namba 74 kinachozungumzia taratibu za mchezo kifungu namba 14 kinaeleza maamuzi ambayo hayakatiwi rufaa ni pamoja na mchezaji akiwa na kadi tatu za njano ni moja kwa moja timu inapokwa pointi, halafu mbona Azam walipokwa pointi baada ya kumchezesha Agrrey Morris mbona Mbeya City hawakukata rufaa.

“Hata kanuni za FIFA kipengele namba 150 kinaelekeza mchezaji atakayecheza akiwa na kadi tatu za njano basi timu itaadhibiwa na ushindi itanyang’anywa, hivyo tunawashangaa TFF kwa kupindisha kanuni wakati zipo wazi,” alisema.

Wakati Rage akiwashauri Simba kufanya hivyo, uongozi wa wekundu hao wa Msimbazi kupitia kwa Rais Evans Aveva, umeweka bayana kuwa leo ndiyo watazungumzia kila kitu, ikiwamo kufungiwa kwa Msemaji wao, Haji Manara mwaka mmoja na faini ya Sh milioni tisa.

Wekundu hao wa Msimbazi wamepokwa pointi tatu na Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji baada ya kubainika madudu kwenye rufaa yao ya awali,  iliyojadiliwa na Kamati ya Saa 72.

Kamati hiyo ya saa 72 awali iliwapa Simba pointi tatu, baada ya kuwaadhibu Kagera kwa mujibu wa kanuni ya 3 (37) ambayo ilitoa pointi tatu na mabao mawili kwa Simba, ambao kwenye mchezo wa awali walifungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Simba wanailalamikia Kagera Sugar kumchezesha Mohamed Fakhi wakati akiwa na kadi tatu za njano kinyume na taratibu, lakini shauri lao hilo limepigwa chini na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU