BAADA YA DIAMOND, NANI KUMSINDIKIZA DIAMOND KWA FUTURE?

BAADA YA DIAMOND, NANI KUMSINDIKIZA DIAMOND KWA FUTURE?

668
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU,

RAPA mahiri aliyeiteka dunia kwa sasa, Mmarekani Nayvadius DeMun Wilburn, maarufu kwa jina la Future, anatarajiwa kufanya onyesho kabambe ndani ya ardhi ya Tanzania Julai 22, mwaka huu.

Mkali huyo, ambaye pia ni mwimbaji na mtunzi wa muziki, katika shoo yake hiyo atasindikizwa na mtaalamu wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’, lakini pia wasanii wengine kibao wa hapa nchini.

Ukiachana na Diamond, wasanii wengine wa hapa nchini wanaotarajiwa kupanda jukwaa moja na Future pamoja na Diamond, watajulikana muda si mrefu, kwa mujibu wa waratibu wa tamasha la kampeni ya ‘Castle Lite Unlocks’, litakatalofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Mmoja wa mashabiki wa muziki hapa nchini, Shaaban Omari, alizungumza na gazeti hili na kusema kuwa angetamani mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba, naye kujumuishwa katika tamasha hilo, ili kuonyeshana kazi na Diamond.

“Tamasha lolote la muziki atakaloshiriki Diamond, haliwezi kunoga bila kuwapo Ali Kiba, hivyo tunawaomba waratibu kuhakikisha wanamjumuisha na Kiba siku hiyo,” anasema.

Kwa mujibu wa Meneja Masoko wa TBL Idara ya Kuunganisha Wateja Afrika Mashariki, George Kavishe, tamasha hilo litawahusisha wasanii wengine wa hapa nyumbani ili kunogesha tukio hilo kubwa na la aina yake ya burudani.

Anasema kuwa, tamadha hilo limelenga kuhamasisha wateja wake wa bia chapa Castle Lite kuifurahia zaidi na pia kuwaleta pamoja kupitia tukio hilo kubwa la burudani.

“Uzinduzi huu utafikia kilele chake tarehe 22 Julai mwaka huu ambapo kutakuwa na tamasha kubwa Dar es Salaam litakalowapa nafasi wateja wetu kushuhudia wanamuziki wakubwa wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuwapa wateja burudani itakayokuwa kwenye kumbukumbu zao kwa muda mrefu,” alisema Kavishe.

Kavishe anaongeza kuwa, kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ya kampeni, zawadi kedekede zitatolewa, zikiwamo muda wa maongezi wa simu za mkononi wa zaidi ya milioni 30 na pia tiketi zaidi ya elfu moja kwa washindi wa droo ambazo zitakuwa zinashindanishwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Afrika Mashariki, Thomas Kamphius, anasema Tamasha hilo litakuwa ni hitimisho la kampeni ya miezi mitatu iliyozinduliwa wiki iliyopita kwenye Club ya Next Door, iliyopo Masaki, Dar es Salaam ya ‘Castle Lite Extra Cold Unlocks.

“Kampeni ya ‘Castle Lite Unlocks’ imekuwa kwenye harakati za maandalizi kwa miaka michache sasa, ambapo Castle Lite imebadili mfumo wa kawaida uliozoeleka kwa kuwaletea wasanii wa ngazi ya juu kimataifa ili kuburudisha ukanda wa pwani ya Afrika kwa maonesho yaliyo na uzoefu wa ‘Extra Cold katika kilele cha tamasha ‘Castle Lite Unlocks’, anasema Kamphius.

Anaongeza: “Tunaelewa kwamba wateja wetu si kila mara wanapata fursa ya kuona baadhi ya matukio haya makubwa, hivyo tunataka kuwaletea fursa hii na kuendelea  kuwaletea uhalisia wa kukumbukwa na mara moja katika uzoefu wa tukio.”

Hali ya baadaye ya muziki inaonekana ni shwari, ya kisasa  na inayohusiana na ipo njiani  kujenga  baadhi ya chapa binafsi zilizo imara, ambao unafungamana na huko nyuma na michakato ambayo ndio tunahusikana nayo kwa ujumla,” Kamphius anaongeza.

Kamphius anaongeza kuwa, kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ya kampeni, zawadi kedekede zitatolewa, zikiwamo muda wa maongezi wa simu za mkononi wa zaidi ya milioni 30 na pia tiketi zaidi ya elfu moja kwa washindi wa droo ambazo zitakuwa zinashindanishwa.

Kwa wale wasiomfahamu Future, huyu si mwanamuziki maarufu sana katika medani ya muziki ikilinganishwa na wakali kama 50 Cent, Drake, Snoop Dogg, Jay Z na wengineo wa kiwango chao, lakini ndani ya muda mfupi tu, Mmarekani huyo amefanya mambo makubwa yaliyowashangaza wengi, zaidi wakiwa ni wapenzi wa muziki.

Rapa Future, ambaye pia ni mwimbaji, mtunzi na mtayarishaji wa muziki, kwa sasa anatamba na ngoma kali zinazokwenda kwa majina ya Low Life aliyoitoa mwaka jana 2016 na Draco pamoja na Mask Off ambazo tayari ameziachia mwaka huu.

Cha kufurahisha zaidi kwa wapenzi wa mwanamuziki huyo ni kwamba, kwa sasa anatamba katika chati za Billboard za Marekani na kuwa msanii wa kwanza kuvunja rekodi ya albamu yake mwenyewe katika nafasi ya kwanza ya chati hizo.

Future aliachia albamu aliyoipa jina la Future iliyotoka Februari 17, mwaka huu ambapo wiki moja baadaye, alitoa nyingine inayokwenda kwa jina la HNDRXX (ikitamkwa Hendrix) ambayo kwa sasa inaongoza katika chati za Billboard.

Future ni mwanamuziki wa kwanza katika historia ya chati hizo kwa kutoa albamu mbili ndani ya muda mfupi na kukamata namba moja katika chati za Billboard.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba, amefanya hivyo huku akiwafunika wanamuziki nguli Marekani na Ulaya kwa ujumla ambao wamejikuta wakipatwa na butwaa kutokana na kile kilichofanywa na Future ndani ya wiki moja.

Hadi sasa, Future amejikuta akiingiza fedha nyingi zaidi kutokana na mauzo ya kazi zake hizo, iwe ni moja kwa moja au kupitia njia ya mtandao.

Mkali huyo aliyeanza kujikita kwenye muziki mwaka 2010, ameshatoa albamu sita za studio, ‘mixtapes’ 12, singo 61 na video za muziki 33 tangu muda huo mfupi.

Kutokana na ubora wake pamoja na kazi zake, Future amefanikiwa kujizolea mashabiki lukuki duniani kote ambapo katika wiki yake ya kwanza, nyimbo zilizopo katika albamu ya Future, zilisikilizwa mara milioni 109.

Future alizaliwa Novemba 20, mwaka 1983 katika kitongoji cha Kirkwood, kilichopo Atlanta, huko Georgia, nchini Marekani ambapo kwa sasa ana umri wa miaka 33.

Kwa sasa mkali huyo ambaye anaonekana kuelekea kuiteka dunia kutokana na ubora wa kazi zake, ana watoto watatu ambao ni: Londyn Wilburn, Prince Wilburn na Future Zahir Wilburn.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU