RICK ROSS WIZI WA JINA LA MUUZA ‘UNGA’ ULIMPONZA, ALIDAIWA BIL 20

RICK ROSS WIZI WA JINA LA MUUZA ‘UNGA’ ULIMPONZA, ALIDAIWA BIL 20

1016
0
KUSHIRIKI

LOS ANGELES, Marekani

UKIACHANA na yale wanayopewa na wazazi wao, wasanii wamekuwa wakiwekeza akili nyingi kufikiria majina yanayoweza kuwatambulisha kwa mashabiki wao.

Cha kufurahisha zaidi ‘a.k.a’ hizo ndizo ambazo huchukua nafasi kubwa na hata kusahaulisha jina halisi.

Ukifuatilia jinsi wasanii mbalimbali wa muziki walivyopata majina yao ya jukwaani, inaweza kuwa burudani tosha kwako.

Hata hivyo, ukiachana na wale wa aina nyingine ya muziki, asili ya majina ya kistaa ya wale wa hip hop imekuwa ikifurahisha na kuvutia zaidi.

Mfano; unajua jina la Eminem lilitokana na kifupi cha lile la alilopewa na wazazi wake ambalo ni Marshall Matthers?

Alianza kujiita ‘M&M’ lakini katika swaga za utamkaji wa jina hilo ndipo ilipotokea Eminem.

50 Cent aliiba jina hilo kutoka kwa rapa wa zamani aliyekuwa akiitwa Kelven ‘50 Cent’ Darnell Martin ambaye alikuwa akitamba kwenye soko la muziki wa hip hop katika miaka ya 1980.

Mkali The Game alipewa jina hilo na bibi yake kutokana na kipaji chake katika michezo mbalimbali.

Kwa upande wake, 2Pac alijipachika jina hilo kutokana na mapenzi yake kwa aliyekuwa mwanamapinduzi wa Peru, Tupac Amaru II.

Rick Ross ni miongoni mwa mastaa walioachana na majina yao ya halisi na kujipa majina ya kujitafutia umaarufu.

Kwa wanaomfahamu, jina lake halisi ni William Leonard Roberts II, lakini alipoanza kufanya muziki aliamua kujiita Rick Ross.

Hata hivyo, supataa huyo alijikuta katika majanga makubwa wakati alipochukua jina hilo.

Inaelezwa kuwa jina hilo aliliiba kutoka kwa aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya ‘unga’ katika miaka 1980. Mshikaji alikuwa akifahamika kama Freeway Rick Ross.

Freeway alianza kuuza dawa za kulevya akiwa shule ambapo ni mwalimu wake ndiye aliyekuwa akimpa mzigo na baadaye ‘mishe’ hizo ziliweza kumuingizia si chini ya Dola za Marekani milioni 3 kwa siku.

Ili kuficha kipato kikubwa kilichokuwa kikitokana na biashara zake hizo za magendo, aliweza kufungua hoteli mjini Los Angeles.

Baada ya kusakwa kwa muda mrefu na vyombo vya dola, Freeway alikamatwa mwaka 1996 na alitumikia kifungo cha gerezani kwa miaka 13 kati ya 20 aliyohukumiwa. Alitupwa gerezani baada ya kunaswa akiwa amenunua zaidi ya kilo 100 za dawa za kulevya aina ya cocaine.

Alipotoka gerezani mwaka 2010, aliona jarida moja lililokuwa na orodha ya wasanii wa hip hop na mmoja wao alikuwa Rick Ross.

Jamaa alikerwa na kitendo hicho na ndipo alipofungua mashtaka akimtaka Rick Ross ‘feki’ kumlipa kiasi cha Dola milioni 10 (zaidi ya Sh bilioni 22 za Tanzania) kwa kulitumia jina hilo kujipatia umaarufu.

Mbali na jina, Freeway aliongeza kwamba Rick Ross amemuiga kila kitu ikiwamo kujifanya ‘muhuni’ ambayo ndiyo maisha yake halisi.

“Mtu kusema hakuwahi kunisikia mimi ni uongo. Ni kweli hakuwahi kusikia jina la Rick Ross?” alihoji Freeway.

“Mimi ndiye niliyeanzisha jina la Rick Ross na lazima nilirudishe kwangu.

“Huyo (Rick Ross) hana uhuni wowote, anaiga maisha yangu ya geto,” aliongeza.

Pia aliishutumu lebo ya muziki ya Universal Music na mwanamuziki Jay Z kwa kuhusika katika mpango wa kumkuza rapa huyo kupitia jina lake la Rick Ross.

“Ni uhuni kuchukua jina la mtu na utambulisho wake na kuvifanya vyako,” alisema mshikaji huyo ambaye pia ni mwandishi wa vitabu.

Katika hatua nyingine, ushahidi wa mahakamani ulibaini kuwa Freeway alikuwa akijua wazi kuwa Rick Ross alikuwa akilitumia jina hilo tangu mwaka 2006, lakini alikaa kimya hadi mwaka 2010 ndipo alipoibua madai hayo, hivyo madai yake yalipitwa na wakati.

Uamuzi  huo wa mahakama haukumuingia akilini Freeway ambapo alisema: “Kama mtu anakuibia na inachukua miaka 10 kumkamata na ikabainika kuwa ni mali yako, kwanini usirudishiwe haki yako?”

Kwa upande wake, Rick Ross alimjia juu mshikaji huyo akisema anatafuta ‘kiki’ kwani jina hilo alipewa akiwa shule na wala hakuliiba kutoka kwake.

Licha ya kukiri kuwa alikuwa akivutiwa na maisha ya ‘kisela’ ya Freeway, Rick Ross alisema jina hilo liliibuka wakati alipokuwa akicheza soka shuleni, jambo ambalo lilipingwa vikali na Freeway.

Kesi ya wawili hao kuhusu jina iliendeshwa kwa miaka mitatu kabla ya Freeway kuambulia patupu katika madai yake ya Dola milioni 10 kutoka kwa Rick Ross.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU