HAPA NDIPO CONTE ALIPOWAUMIZA WENZAKE EPL

HAPA NDIPO CONTE ALIPOWAUMIZA WENZAKE EPL

515
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

WAKATI Antonio Conte akitua Chelsea, kuna baadhi ya mashabiki ambao walikuwa na wasiwasi kama Muitaliano huyo ataweza kuvaa viatu vya watangulizi wake, akiwamo Jose Mourinho na kisha vikamuenea.

Wasiwasi huo kwa mashabiki uliibuka baada ya kuwapo tetesi zikimhusisha Conte kuwa amekubali kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa muda,  Guus Hiddink kwenye klabu hiyo ya  Stamford Bridge kutokana  na kuwa kuna ambao walikuwa wakihoji kama ataweza kulimudu soka la Uingereza,  licha ya kuwa alikuwa ameshajijengea jina akiwa na klabu ya Juventus.

Hata hivyo, mashabiki hao walikuwa wakimfahamu juu juu na sasa amewadhihirishia kuwa yeye ndiye Conte, mfalme wa mataji kutokana na usiku wa kuamkia leo alikuwa akijiandaa kuipa ubingwa timu hiyo, huku akiwa bado ana mechi nyingine mbili mkononi na huku akisubiri mwingine wa Kombe la FA.

Baada ya kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kocha huyo kwa takribani msimu mzima, BINGWA imejaribu kuangalia mambo kadhaa ambayo pengine ndiyo yaliyomfanya Muitaliano huyo kuwazidi maarifa makocha wengine 19 aliokuwa akikimbizana nao katika mbio za kuwania taji hilo.

Yafuatayo ni mambo kadha wa kadha ambayo BINGWA imejaribu kuyabaini kama pengine ndiyo yaliyomfanya kuwapiku wapinzani wake hao.

  1. Uzoefu wa kutwaa mataji

Katika kipengele hiki, Conte anaonekana kuwa mzoefu kutokana na kwamba amewahi kufanya hivyo mara nyingi akiwa kama mchezaji na kocha.

Ifuatayo ni orodha ya mataji ambayo kocha huyo amewahi kuyatwaa akiwa mchezaji na kocha.

Akiwa mchezaji :

Serie A – 1994/95, 1996/97, 1997/98, 2001/02, 2002/03

Ligi ya Mabingwa  – 1995/96

Kombe la Uefa – 1992/93

Coppa Italia – 1994/95

Uefa Super Cup – 1996

Intercontinental Cup – 1996

Uefa Intertoto Cup – 1999

Supercoppa Italiana – 1995, 1997, 2002, 2003

Akiwa kama kocha:

Serie A – 2011/12, 2012/13, 2013/14

Supercoppa Italiana – 2012, 2013

Nje ya Juve, vilevile Muitaliano huyo aliwahi kutwaa mataji ya Ligi za   Serie B akiwa na timu ya Bari msimu wa  2008/09 na huku akishika nafasi ya pili akiwa na kikosi cha  timu ya Taifa ya Italia katika fainali za Kombe la Dunia 1994 na za fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2000.

  1. Ni mkali wa kuvunja rekodi

Kama ilivyotokea msimu huu, Conte ameweza kuendelea  kujivunia uwezo wake wa kuvunja rekodi kama alivyokuwa Juventus  alipoiwezesha kumaliza msimu wa  2011/12 bila kupoteza mchezo hata mmoja, ukiwa ni wa kwanza kuinoa klabu hiyo ya mjini Turin na hivyo kuwa  Muitaliano wa kwanza asiyeshindwa tangu ilivyofanya hivyo AC Milan msimu wa 1991/92.

Baada ya kutwaa taji hilo, Conte aliongeza mataji mengine mawili ya ligi na katika taji lake la tatu akafanya maajabu wakati  Juve iliposhinda mechi nyingi 33 na kujikusanyia pointi 102 na huku ikiwa imeshinda mechi zake zote  19 ilizocheza  ikiwa nyumbani.

Mafanikio hayo vilevile ndiyo yalimfanya kuwa kocha wa kwanza  katika michuano ya Serie A  kunyakua tuzo ya kocha bora wa mwaka misimu mitatu mfululizo.

3.Kubadili mfumo kwa haraka

Wakati akilisoma soka la Uingereza, Conte amekuwa akionekana kutumia mifumo tofauti kulingana na timu pinzani alizokuwa akikutana nazo na huku akilisoma zaidi soka hilo la England.

Mfano ni wakati alipoanza kibarua kwenye klabu hiyo ya Stamford Bridge, kocha huyo alianza kutumia mfumo wa 4-1-4-1, zikiwamo mechi ambazo alikutana na kichapo kutoka kwa Arsenal na dhidi ya Liverpool, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Desemba 2009 kwa kocha huyo kupoteza mechi mbili mfululizo tangu akiinoa Atlanta.

Hata hivyo, baadaye Conte akachekecha kichwa na kubaini mbinu za Arsenal waliokuwa wakijaribu mbinu zake mpya na hivyo akaamua kubadili wachezaji na kutumia mfumo wa 3-4-3 katika muda uliokuwa umebaki wakati wa mechi dhidi ya Arsenal, ingawa nao haukuonekana kuwazuia Gunners kuendelea kuwatesa.

Ikiwa ni miezi miwili baada ya kucheza michezo 11 akitumia mfumo huo, Conte alibadilisha tena na kuamua kutumia mfumo aliokuwa akiutumia akiwa na Juventus wa 3-5-2, lakini nao ukaonekana kutofua dafu na hivyo Muitaliano huyo akaamua  tena mfumo wake wa 3-4-3 ambao aliutumia katika michezo dhidi ya    Hull City na  Everton na ukaonekana kuwa mbadala na hivyo akaamua kuuboresha zaidi wakati wa mapumziko ya kupisha mechi za timu za taifa kwa kuongeza muda wa nyongeza wa mazoezi ili kuwanoa zaidi wachezaji wake.

Mfumo huo ndio hadi sasa unatumiwa na kocha huyo na ndio tunaushuhudia  ukitumiwa na Juventus pamoja na timu ya Taifa ya Italia,

Conte alifikia uamuzi huo baada ya kuanza vyema mechi zake za kwanza, lakini baadaye akakishuhudia kikosi chake kikisimamishwa na hivyo kukifanya kiambulie pointi 13 katika michezo saba na huku kikiwa nyuma kwa pointi tano dhidi ya timu zilizokuwa zikiongoza ligi.

Mfumo huu unaonekana kuwanufaisha mastaa wake wengi, hususan Kanté, akisaidiwa na Matic ambapo hadi sasa nyota huyo wa zamani Leicester City ameshatoa pasi 70 zilizowafikia walengwa, ambayo ni rekodi katika michuano ya Ligi Kuu, huku akitibua pasi za wapinzani mara 4, akapokonya mipira mara 13, chenga zilizozaa matunda mara 3 na huku akifunga mara mbili katika nafasi alizozitengeneza mwenyewe.

  1. Ujanja wa kujifunza lugha

Kitu cha kwanza kilichokuwa kikiwatia wasiwasi mashabiki wa  Chelsea ni kwa kocha huyo kama ataimudu klabu yao kutokana na kutofahamu vyema lugha ya Kiingereza.

Wasiwasi huo kwa mashabiki wa  Blues ulitokana na kwamba aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, Felipe Scolari, alishindwa kufikisha mawazo yake kwa wachezaji katika kipindi alichoinoa klabu hiyo kutokana na kutomudu vyema lugha hiyo.

Hata hivyo, Conte aliweza kulibaini hilo na kwa haraka kabla ya hajaanza kibarua hiyo Stamford Bridge aliweza kujifunza Kiingereza na hivyo kuwa rahisi kwake kuelewana na wachezaji na huku akiwafikishia maelekezo yake bila shida.

  1. Kumbe ni kama Mourinho

Kwa namna nyingine, Conte amekuwa akifananishwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jose Mourinho.

Kufananishwa huku kunatokana na kwamba mbinu za Muitaliano huyo mwenye umri wa miaka 46 amekuwa akitumia mfumo wa kujihami, maarufu kama ‘kupaki basi’.

Hata hivyo, licha ya kuwa hakufanya vizuri katika zama za mwisho za  Mourinho mwishoni mwa zama zake kwenye klabu hiyo ya Stamford Bridge, lakini Conte unaonekana kumkubali kama ilivyokuwa kipindi cha miaka mingi wakati Mreno huyo akiutumia.

Kwa kutumia mfumo huo, ilishuhudiwa kuna kipindi aliweza kucheza michezo 11 na kushinda yote, huku ukimsaidia kupata mabao 25 na huku pia wakiruhusu mawili.

Miongoni mwa timu ambazo zilionja machungu ya mfumo huo ni Leicester, Man Utd, Spurs, Everton, Southampton  na  Man City, ambazo ni kati ya mahasimu wakubwa wa timu hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU