MAKINDA AJAX KUIONDOA MAN UNITED LIGI YA MABINGWA?

MAKINDA AJAX KUIONDOA MAN UNITED LIGI YA MABINGWA?

691
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

MANCHESTER United wametinga fainali ya Ligi ya Europa ambapo watavaana na Ajax, mchezo utakaochezwa Mei 24 kwenye Uwanja wa Friends Arena, uliopo mjini Stockholm, Sweden.

Man United wameipata nafasi hiyo baada ya juzi kutoa sare ya bao 1-1, ikiwa ni baada ya mchezo wa kwanza walioshinda bao 1-0.

Katika mchezo huo wa marudiano uliochezwa Old Trafford, Marouane Fellaini alikuwa wa kwanza kuifungia Man United, kabla ya Facundo Roncaglia kuisawazishia Celta Vigo.

Kwa upande wao, Ajax walifika hatua hiyo baada ya kuwatoa Lyon kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-4.

Hakika Kocha Jose Mourinho anategemea zaidi kuifunga Ajax ili kunyakua taji la michuano hiyo, ambalo litampa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya moja kwa moja.

Kikosi cha Ajax, kinachoundwa na wachezaji wengi chipukizi, kinasifika kwa soka lao la kasi, lakini watakutana na Mourinho, ambaye ni mara chache kumuona akifanya makosa katika hatua kubwa kama hiyo.

Tangu alipoiacha Porto baada ya kuipa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mourinho ameshinda mechi 11 kati ya 13 alizoingia fainali.

Lakini pia, katika mechi hizo mbili alizofungwa, haikuwa katika dakika 90, bali alipambana hadi dakika za nyongeza na hata kufikia mikwaju ya penalti.

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 54, amekuwa akipingwa kwa aina ya uchezaji wa kikosi chake, lakini linapokuja suala la fainali, anabaki kuwa bora.

Katika mchezo dhidi ya Celta Vigo, mashabiki wa Man United hawakufurahiswa na kiwango, lakini kitendo cha timu yao kutinga fainali kinabaki kuwa kumbukumbu nzuri kwao.

Celta walionekana kuwatawala zaidi Man United pale Old Trafford, kwani walimiliki mpira kwa asilimia 67 na walipiga mashuti 16, huku Man United wakiwa na 11.

Kunyakua ubingwa wa Ligi ya Europa ndio kipaumbele cha Mourinho. Kutokana na mwenendo mbaya walionao Ligi Kuu England, ubingwa wa mashindano hayo utawapa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kupoteza mtanange wa fainali dhidi ya Ajax, litakuwa ni pigo kubwa kwa Mourinho na Man United kwa ujumla.

Kuthibitisha kuwa Mourinho ameelekeza nguvu na akili yake kwenye ubingwa wa Ligi ya Europa, wikiendi iliyopita, kocha huyo alilazimika kuwapumzisha mastaa wake nane wa kikosi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal.

Katika mtanange huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Emirates, kikosi chake kiliambulia kichapo cha mabao 2-0.

Kichapo hicho kiliwapunguza kasi vijana hao wa Old Trafford kwenye mbio za kuifukuzia top four, hivyo kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Ajax itakuwa ni hatari zaidi kwao.

Ujio wa Mourinho uliibua matumaini mapya kwa mashabiki wa Man United, ambao tayari walishakata tamaa kutokana na mwenendo mbaya wa timu yao hiyo mara baada ya kustaafu kwa babu Sir Alex Ferguson.

Mara baada ya Ferguson kuondoka, chini ya kocha wa kimataifa wa Scotland, David Moyes, Man United ilijikuta ikimaliza ligi ikiwa nafasi ya saba.

Baadaye ilimaliza ikiwa nafasi ya nne, kabla ya msimu mwingine kujikuta nafasi ya tano na kuangukia michuano ya Ligi ya Europa, ambako hata hivyo hawakufanya vizuri.

Kwa takwimu hizo, Man United haikuwahi kuwa kwenye ubora wa juu tangu kutundika daluga kwa mkufunzi huyo, Ferguson.

Mourinho, aliyechukua nafasi ya Mholanzi Louis van Gaal, alionekana kuwa ndiye atakayekuwa shujaa na alipewa nafasi kubwa ya kubadili upepo mbaya ulioikumba timu hiyo.

Wengi waliamini kuwa ingekuwa kazi rahisi kwa kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Inter Milan na Real Madrid, kumaliza ligi akiwa ‘top four’.

Ikiwa ni miezi 10 pekee imepita tangu Mourinho akabidhiwe mikoba, tayari inaonekana wazi kuwa Mreno huyo ana wakati mgumu kuhakikisha Man United inamaliza ikiwa nafasi nne za juu.

Kwa sasa kikosi chake kinashika nafasi ya sita, kikiwa kimeachwa pointi nne na mahasimu wao, Manchester City, waliopo nafasi ya nne.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU