BARUA YANGU KWA WAZIRI DK. MWAKYEMBE

BARUA YANGU KWA WAZIRI DK. MWAKYEMBE

724
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR

HIVI karibuni Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alitoa angalizo kali kwa wanachama ambao ni wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa makini na kutowaruhusu viongozi waliowahi kuziongoza Simba na Yanga kugombea kuongoza Shirikisho hilo.

Hiyo ilikuwa ni kauli ya kishujaa ya Waziri Mwakyembe ambaye baada ya kukaa chini na kutafakari kwa kina, amegundua  kuwapo kwa uozo mwingi katika Shirikisho hilo na kuahidi  kuingia mstari wa mbele mwenyewe kuhakikisha makosa yaliyojitokeza huko nyuma hayajirudii tena katika uchaguzi wa mwaka huu.

Waziri huyo ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana kubwa ya kusimamia michezo hapa nchini, naamini uwepo wake katika wizara hiyo kunaweza kuwa ni msaada tosha kwa wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu hapa nchini hasa katika kipindi ambacho TFF inakwenda kufanya uchagazi mkuu wake.

Mengi yamezungumzwa kuhusiana na madudu yaliyofanywa na uongozi wa Malinzi katika kipindi chake cha miaka minne alichokaa madarakani, ikiwamo kushindwa kulitoa soka letu hapa lilipo kulisogeza mbele, timu kupanga matokeo na mengine mengi ya kustaajabisha hadi kufikia Watanzania na wadau wa michezo kuuchukia mpira wa miguu.

Uchaguzi wa TFF utafanyika Agosti mwaka huu huku wadau mbalimbali wakionesha nia ya kuwania nafasi za juu ndani ya shirikisho hilo, ambapo wengi wanatoka kwenye klabu za Simba na Yanga, kwani pamoja na Waziri Mwakyembe kutoa angalizo na kwa wanachama wapiga kura kutoruhusu viongozi waliowahi kuongoza klabu hizo kongwe hapa nchini, lakini tayari kuna baadhi yao wameshaanza kujipanga kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali.

Miongoni mwa watu hao ambao wanatajwa kutaka kugombea ni pamoja na rais wa sasa Jamal Malinzi,  ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Yanga na ambaye chini ya uongozi wake wa sasa mambo yamekwenda kombo sana huku TFF ikilalamikiwa mno kwa kuendeleza ushabiki na kufanya maamuzi yenye kuzinufaisha klabu za Simba na Yanga na hasa Yanga.

Kauli ya Waziri Mwakyembe japo inaonekana kuchelewa lakini ina mantiki kubwa sana, ni kweli soka la Tanzania linahitaji kiongozi ambaye hajawahi kuwa na wadhifa wowote katika klabu hizo kubwa hapa nchini.

Kwa sasa watu wameshapanga safu zao na mikakati imekuwa ikiendelea kufanyika na ndiyo sababu hata leo hii kumekuwa na maamuzi ya kutatanisha kwenye Kamati za TFF juu ya masuala kadhaa.

Fainali ya Kombe la Shirikihso maarufu kama FA, kuchezwa Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri, ni sehemu ya siasa za uchaguzi mkuu wa TFF. Ni kwamba, kuna mambo mengi fainali hiyo kuchezwa katika mji huo na ni mkakati maalumu wa kiuchaguzi.

Rais Malinzi anayetarajiwa kutetea kiti chake anaelezwa kumtaka Mlamu Ng’ambi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma, kuwa Makamu wake katika uchaguzi wa Agosti.

Uamuzi wa fainali hiyo kuchezwa Dodoma ilikuja baada ya sintofahamu iliyotawala vichwani mwa mashabiki wengi wa soka baada ya malinzi kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, kuandika akihitaji kufanyika kwa droo ya kuchagua uwanja wa fainali, kisha akashambuliwa sana wadau wa soka na baadaye kitendawili hicho kikateguliwa na Malinzi mwenyewe alipoutangaza uwanja huo ndio utakaopigwa fainali hizo.

Mheshimiwa Waziri Mwakyembe kuna mipango mingi inaendelea kufanywa lengo likiwa ni kuhakikisha viongozi ambao hawana uchungu na mchezo wa soka, kutaka kurudi madarakani kuendelea kuliongoza shirikisho hilo.

Ukiwa kama Waziri mwenye dhamana ya michezo, umma wa Watanzania wapenda michezo jicho lao lipo kwako, kwani Wizara yako ndiyo yenye dhamana kubwa ya kusimamia michezo hapa nchini, wanakutegemea uwepo wako katika wizara hiyo kuna mambo mengi utayarekebisha ikiwamo kupata viongozi bora kwenye vyama vya michezo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU