KUKATALIWA KWA BAO LA MAHREZ ULIKUWA UONEVU?

KUKATALIWA KWA BAO LA MAHREZ ULIKUWA UONEVU?

514
0
KUSHIRIKI

MANCHESTER, England

DAKIKA ya 77, Man City 1-1 Leicester City. Mwamuzi Bobby Madley anaamuru lipigwe pigo la penalti baada ya Gael Clichy kumwangusha staa wa Leicester, Riyad Mahrez, katika eneo la hatari.

Mahrez anautenga mpira, anasogeza hatua, anaupiga, ghafla…anateleza huku mpira alioupiga ukitinga nyavuni. Madley anakataa bao na anawapa City pigo la adhabu kuelekea Leicester.

Ilikuwa ni nafasi pekee kwa Leicester kupata bao la kuongoza lakini Madley aliikata furaha ya sekunde chache iliyotaka kuongozwa na Mahrez kwa kulikataa bao hilo na kuamuru mpira wa adhabu upigwe kuelekea lango la timu pinzani.

Nini kilichotokea?

Marudio yalionesha kuwa mguu wa kulia wa Mahrez uliugusa mpira ambao ulipigwa na mguu wa kushoto wa Mualgeria huyo wakati akiteleza, hivyo kufanya mwelekeo wake kubadilika na kumwacha kipa wa City, Willy Caballero, akiwa hana la kufanya.

Kwa mujibu wa sheria ya Fifa, mpiga penalti haruhusiwi kuugusa tena mpira ambao ameshaupiga hadi mchezaji mwingine atakapougusa.

Na wakati sheria ilipoundwa ili kuzuia wachezaji kuupa msaada zaidi mpira unaoelekezwa nyavuni, ni kweli Mahrez aliugusa mpira mara mbili hivyo kukiuka sheria hiyo.

Ila uonevu uliodaiwa kutendeka kwa mashabiki wa Leicester ulisaidiwa na rekodi ya mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita baina ya Real Madrid na Atletico, mechi ambayo straika Antoine Griezmann alifunga bao kama hilo lakini likakubaliwa!

Bao hilo la penalti liliwafanya Atletico kuongoza 2-0, lakini marudio yalionesha kuwa ilibidi bao hilo likataliwe na mwamuzi na Madrid walistahili mpira wa adhabu.

Hata hivyo, matokeo hayo hayakuwazuia Los Blancos kufuzu kucheza fainali ya michuano hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU