SERENGETI BOYS, NIA NA SABABU YA KUPATA USHINDI IPO

SERENGETI BOYS, NIA NA SABABU YA KUPATA USHINDI IPO

455
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

MACHO na masikio ya kila Mtanzania mpenda soka siku ya leo yapo nchini Gabon kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana, ambapo timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys itakapotupa karata yake ya kwanza dhidi ya Mali.

Mchezo huo wa kwanza wa kufungua dimba na bingwa mtetezi Mali, utafanyika kwenye Uwanja wa Franceville, jijini Libreville na kufuatiwa na mchezo wa Angola dhidi ya Niger.

Mtanange huo utaanza kuchezwa majira ya saa 9:00 Gabon ambapo ni sawa na saa 12:00 za Tanzania.

Mchezo wa pili utakuwa dhidi ya Niger, Mei 18 saa 9:00 za Gabon sawa na saa 12:00 za Tanzania huku mchezo wa mwisho kwenye makundi utachezwa Mei 21 dhidi ya Angola.

Timu zitakazofuzu nusu fainali zitakuwa zimefuzu kuwakilisha Afrika katika fainali za Fifa U-17 zitakazofanyika nchini India kuanzia mwezi Oktoba.

Serengeti ni timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ilifuzu baada ya kutolewa kwa Congo Brazaville iliyomchezesha mchezaji aliyezidi umri na kushindwa kumpeleka mchezaji huyo kwenye vipimo vya MRI ili kuthibitisha umri wake.

Kikosi hicho ambacho kipo kundi B wakiwa na Mali, Niger na Angola ambapo timu itakayoshinda michezo yake miwili itakuwa imepenya hatua ya nusu fainali na kupata nafasi ya moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini India.

Ikumbuke Serengeti imefanya maandalizi ya kutosha kuelekea michuano hiyo ambapo wamecheza michezo ya kirafiki saba, wameshinda michezo mitano ikitoka sare na kufungwa mmoja jambo liloifanya kuwa na dalili nzuri za kubeba taji hilo.

Maandalizi waliyofanya wana kila sababu ya kutotoa Watanzania kimasomaso, hasa kuanzia kambi hadi michezo hiyo saba ya kirafiki ambayo imeonyesha kujiamini uwanjani na utayari wa kukabiliana na timu yoyote ile.

Kisaikolojia Serengeti Boys inaaminika ipo vizuri ila rai kubwa ni kutojiamini sana na kukumbuka kuwa wamebeba dhamana ya Watanzania wengi nyuma yao hivyo wapingane kwa jasho na damu.

Kikubwa ni wasijione wameiva kiasi cha kujisahau na baadaye kuwadharau wapinzani na kuleta kejeli kwamba kama tuliwafunga Misri kwanini tushindwe kwa Mali, hii kauli kamwe si rafiki na wapambane kwa ajili ya Taifa.

Tusisahau soka ni mchezo unahojitaji nidhamu wakati wote, ukileta mzaha kidogo unaambulia patupu hivyo basi mafanikio yasiwavimbishe vichwa bali wajiandae kikamilifu kwa ajili ya kupeperusha vema bendera ya Taifa.

Jiandaeni ili kuvuka kizingiti hiki cha kwanza, Watanzania tunawasapoti na tunawatakia kila la kheri ili muweze kufanya vema kwenye mashindano haya.

Tukumbuke hatuko peke yetu kwenye michuano hii, kuna kundi A lenye timu mwenyeji Gabon, Geinea, Cameroon na Ghana, hivyo kuna haja ya kupambana hadi tone la mwisho.

Wapinzani wetu Mali wao wapo kwenye mashindano baada ya kuruhusiwa kushiriki baada ya adhabu yao waliyopewa kwa kosa la Serikali yao kuingilia mchezo huo wa soka kufutwa Aprili 28, hivyo tuna kila sababu ya kuwafunga.

Watanzania wote tupo nyuma yenu na tunaimani kubwa huu ni wakati wetu au zamu ya taifa letu kujidai kama wafanyavyo majirani zetu kama Kenya na Uganda, ambao wao jambo la kufuzu limekuwa kawaida.

Ikumbukwe hii ni mara ya kwanza kupata nafasi hii baada ya miaka ya nyuma kuondolewa kufuatia kumchezesha Nurdin Bakari ambaye alikuwa amezidi umri hivyo tusichezee nafasi hii.

Kila Mtanzania anatamani kuona timu hii inafika mbali ndio maana wadau mbalimbali walijitokeza kuwachangia, hivyo thibitisheni kama mmeweza kwa kufanya vema.

Kubwa tunalowaombea ni ushindi, hivyo tunawatakia kila la kheri katika michezo yote ili tuweze kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia hapo baadaye nchini India.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU