ULITAKA SIMBA WAFANYE NINI ZAIDI?

ULITAKA SIMBA WAFANYE NINI ZAIDI?

1071
0
KUSHIRIKI

NA OSCAR OSCAR

KAMA kuna jambo linaloniumiza kichwa ni kuona Simba na Yanga bado wanakwenda kucheza mechi zao za mikoani kwa kutumia usafiri wa barabara. Kama kuna dhambi kubwa kwa klabu hizi, basi nikuona mpaka leo hazina hata viwanja vya kufanyia mazoezi.

Tunapokuwa kwenye mkakati wa kutaka klabu hizi zifanye mabadiliko, maana yake si Yanga apewe Yussuph na Simba apewe Mohamed Dewji ‘Mo’. Mabadiliko ni kuzifanya timu hizi ziweze kujiendesha kwa faida. Mabadiliko ni kuona timu hizi zinajiendesha kibiashara zaidi.

Mfanyabiashara huwa hachagui mteja. Akija SportPesa sawa, akija Azam sawa. Cha msingi ni kuhakikisha timu inatengeneza faida kila mwishoni mwa msimu. Simba na Yanga zilitakiwa kutumia basi zinapotoka hotelini kuelekea uwanjani na si kutoka klabuni kuelekea Mbeya wala Kagera. Simba na Yanga zina uwezo mkubwa wa kushawishi kila kampuni kuingia mkataba nao.

Wiki iliyopita klabu ya Simba iliingia mkataba na Kampuni ya kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali maarufu kama SportPesa. Ni mkataba mnono ambao unawafanya Simba kuvuta kitita cha bilioni 4.9 kwa muda wa miaka mitano. Huu ni mkataba ambao kihesabu simba watapata bilioni moja za Kitanzania kila mwaka. Shilingi za Kitanzania milioni 74.5 kila mwezi.

Unataka habari gani njema zaidi ya hii? Haya ndiyo mabadiliko ya mpira wa Kitanzania yaliyokuwa yanaimbwa kila kukicha. Hii ni aina ya mikataba ambayo inatakiwa kuwa na mwendelezo. Tunapaswa kujifunza kwa watu waliofanikiwa zaidi, Arsenal na Borussia Dortmund wanapaswa kuwa mfano mzuri sana kwa timu zetu zinazotaka kuendelea.

Arsenal wakati wanataka kuingia makubaliano na Arsenal hawakuwachekea. Borussia Dortmund walipowapata Kampuni ya Bima ya Idurna Park hawakufanya makosa pia. Nategemea kuwaona Simba wakiwatumia vilivyo SportPesa.

Mabadiliko ndani ya Simba na Yanga hayamaanishi Yanga iende kwa Yusuph Manji na Simba iende kwa Mohammed Dawji ‘Mo’. Klabu hizi zinapaswa kujiendesha kibiashara. Badala ya Simba kuendelea kuchangishana pesa za kumalizia uwanja wao wa Bunju, wanaweza kukaa tena na Kampuni ya SportPesa na kufanya kama Arsenal. Simba wanapaswa kujiongeza na kumalizana na SportPesa kwenye udhamini wa uwanja.

Uwanja wa Arsenal pale London unaitwa Emirates kwa sababu tu ya mdhamini, pale Ujerumani Uwanja wa Signal Iduna Park ni jina la mdhamini tu. Simba wanapaswa kuwapeleka SportPesa kule ‘Bunju Stadium’ na kuingia nao makubaliano mengine ya haki ya jina la Uwanja. Itapendeza na itakuwa hatua kubwa endapo uwanja ule utapatiwa mdhamini na kuitwa Sportpesa Stadium kwa miaka kadhaa kuliko kuendelea kutembeza bakuli.

 

SportsPesa inapaswa kuwa mwanzo tu wa uwekezaji kwenye klabu zetu kubwa hapa nchini. Natamani pia kuwaona Yanga wakiingia kwenye udhamini huu na kuijenga timu kwenye misingi ya kujitegemea. Mambo ya kuendelea kutegemea mfuko wa mtu kuendesha klabu yamepitwa na wakati. Kwa mujibu wa takwimu kutoka viwanjani, Yanga ndiyo timu yenye mashabiki wengi Tanzania.

Inashangaza kuona Yanga wakitaabika kuiendesha timu ya namna hii. Mtaji mkubwa kwenye mchezo wa soka ni mashabiki na ndio maana Yusuph Manji na Mohammed Dewji wanazitaka Simba na Yanga. Simba na Yanga wanapaswa kuwa na watu kama Sportpesa kama 10 hivi, kila kitu kinachozunguka Simba na Yanga kinaweza kugeuzwa kuwa biashara na timu ikaingiza chochote.

Mapato ya mlangoni yanapaswa kuwa kama ziada tu. Pesa ya klabu ipo kwenye uuzaji wa bidhaa na matangazo. Ulitaka Simba wafanye nini zaidi? SportPesa ni moja ya mikataba ambayo itaipeleka klabu mbele, ni njia ya kuifanya timu ianze kujitegemea kiuendeshaji. Angalau Simba wana chochote cha kuanzia maandalizi ya msimu ujao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU