KANUNI UEFA ZITAKAVYOZIBEBA ‘TOP FOUR’ ENGLAND

KANUNI UEFA ZITAKAVYOZIBEBA ‘TOP FOUR’ ENGLAND

1526
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

TIMU za Chelsea na Tottenham tayari zimeshajihakikishia kushiriki katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Chelsea wamekata tiketi hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo na huku Tottenham wakiwa nafasi ya pili, baada ya hadi sasa kuwa wameshajikusanyia pointi nyingi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Kutokana na hali hiyo, kinyang’anyiro hicho kimebaki kwa timu nne za Manchester City, Liverpool, Man Utd na Arsenal, ambazo bado zinapigana vikumbo na huku ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Hata hivyo, licha ya vigogo hao kuwa katika vita hiyo, kuna swali jingine kwa sasa ambalo ni la kujiuliza ni timu ngapi za Ligi Kuu England zitafuzu kushiriki michuano hiyo endapo Man Utd watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa?

Katika Makala haya, BINGWA imejaribu kuangalia kanuni za Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ili kuona zitakuwa ni timu ngapi zitafuzu michuano hiyo endapo mashetani hao wekundu watafanikiwa kubeba ndoo hiyo.

Kanuni za Uefa zinaeleza kwamba, mshindi wa michuano ya Ligi ya Europa anakuwa amefuzu moja kwa moja kushiriki katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia hatua ya kufuzu.

Mfano ni kama mwaka 2012, wakati Chelsea iliponyakua taji hilo dhidi ya Bayern Munich, ambapo iliilazimu Tottenham kunyang’anywa nafasi, licha ya kumaliza michuano ya Ligi Kuu ikiwa ya nne.

Utaratibu huo bado unakumbukwa jinsi ulivyowaumiza mashabiki wa  Tottenham na sasa bado kuna  wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa timu zinazoshika nafasi nne za juu, wakihisi kwamba endapo Man Utd itafanikiwa kutwaa taji hilo la Ligi ya Mabingwa, huenda ikawagharimu kwa kujikuta wakipoteza nafasi zao.

Hata hivyo, safari ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2012, kutokana na kwamba, ushindi wa Man United hautaweza kuziathiri timu nyingine za Ligi Kuu zitakazofuzu kushiriki katika michuao hiyo ya Ligi ya Mabingwa.

Hii ni kutokana na kwamba kanuni za sasa za Uefa ambazo zilianzishwa mwishoni mwa mwaka 2012 zinaeleza wazi kwamba walau timu tano zinazoshiriki katika ligi moja zinaweza kufuzu michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.

Hivyo basi, kutokana na kanuni hiyo, hata endapo Man United watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa, timu nyingine ambazo zitashika nafasi nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu hazitapokonywa nafasi zao za kushiriki ligi hiyo kubwa kwa klabu.

Usalama wa timu hizo kutopokonywa nafasi zao ni kutokana na kwamba endapo Manchester United watashinda taji hilo la Ligi ya Europa watakwenda moja kwa moja hatua ya makundi.

Na hii pia ni kwa sababu timu    za Real Madrid na Juventus ambazo zimefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo mwaka huu tayari zimeshakata tiketi ya mwakani, kutokana na nafasi zinazozishika kwenye msimamo wa ligi zao za nyumbani.

Kutokana na utaratibu huo, ni kwamba bingwa wa michuano hiyo anakuwa huru na hivyo kati ya Man Utd na Ajax atakayeibuka mbabe katika mchezo huo utakaopigwa  Stockholm moja kwa moja atakuwa amejihakikishia tiketi ya kucheza mechi za awali za michuano hiyo.

Manchester United watakutana na Ajax katika mechi hiyo ya fainali, baada ya kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uholanzi, Eredivisie kutinga hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-4 waliyoyapata dhidi ya Lyon.

Jose Mourinho anaamini ushindi wa mtanange huo wa  Stockholm yatakuwa ni mafanikio mazuri kwake wakati akimaliza msimu wake wa kwanza akiinoa klabu hiyo ya Old Trafford.

“Baada ya mechi 14 sasa tupo fainali na endapo tutafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya  Europa nitakuwa na furaha kubwa  na yatakuwa ni maajabu,” alisema Mourinho katikati mwa wiki iliyopita.

“Ina maana kuna nafasi ya kutwaa ubingwa, nafasi ya kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na itakuwa ni nafasi nzuri ya kumaliza msimu huu vyema kwa sababu mechi hiyo ya fainali ndiyo itakuwa ya mwisho,” aliongeza tena Mourinho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU