JIULIZE NI KWANINI AMEAMUA KUISHI KIJASUSI NA WEWE?

JIULIZE NI KWANINI AMEAMUA KUISHI KIJASUSI NA WEWE?

379
0
KUSHIRIKI

UNASHIKA simu yake unakutana na ‘password’, unaamua kuachana nayo. Ila unamwona anafungua intaneti na kuingia Facebook, ukitaka kujua ana chati nini na na nani na huko nako pia anaficha.

Kila ukijaribu kufikiria ni kitu gani huwa anafanya bila kukuficha na huwa huru zaidi mkiwa pamoja, huoni. Kila jambo analofanya anakuficha tu. Kwenye simu kuna namba ya siri, hata akipigiwa simu mbele yako huwa kuna hali ambayo si’ ya kawaida.

Huwa ni aidha asipokee, aongee naye kidogo kisha amuamuru ampigie baadaye au aende mbali na wewe ndipo akaongee na simu husika. Katika hali kama hii ni lazima utakuwa kuna kitu kinakusumbua katika nafsi yako.  Mapenzi hujengwa na hali f’lani ya wivu.

Kama ukiwa na chembe ya hali hii ni dhahiri vitu kama hivi havitakuwa na tafsiri timamu katika akili yako. Utamuangalia mwenzako katika jicho la kiulizo na hatimaye kutoa tafsiri hasi juu yake. Ila kabla hujatoa tafsiri tofauti juu yake, kuna siku umekaa na kuzungumza naye kuhusiana na hali hiyo?

Katika hali ya kawaida unapoona kitu kama hiki kikitokea tafsiri inayokuja moja kwa moja katika akili yako kuwa ni lazima atakuwa na mtu ana chati naye ambaye si kwa wema.

Na kweli katika hali ya kimapenzi si mbaya sana kuwaza hivi. Ila ni vyema ikatambulika  kuna baadhi hufanya hivi si kwa sababu hiyo, hapana.

Kuna dada mmoja nilikuwa nikiongea naye katika basi wakati nikienda Moshi. Yeye alisema huwa hapendi hata kidogo mpenzi wake ajue kile anachofanya katika mitandao au katika simu yake. Kwa mujibu wa maelezo yake, ni kuwa mpenzi wake huwa ana wivu sana na huwa hapendi utani wa kijinga hata kama huwa ana chati na marafiki zake wa kike.

Katika kuepusha ugomvi baina yao huwa anaona bora mpenzi wake asione kile anachochati na hao marafiki zake. Kwa kuwa katika maongezi yake huwa kuna mambo ya kijinga na hata wakati mwingine hutaniana katika utani unaoweza kutafsirika tofauti. Huepusha kutokea matatizo kwa mpenzi wake kwa kuficha huwa anachati nini.

Kwa wengine maneno hayo yanaweza kuonekana kama utetezi na kumtafsiri kuwa huwa anafanya mambo mengine ya ajabu.

Ndiyo, anaweza kuwa kuna mahali anakosea ila isiwe kuwa anafanya usaliti. Haipendezi wala haifai kufichana mambo na mwandani wako. Ila vipi kuhusu utani na watani zake? Nakubaliana moja kwa moja kuwa utani una mipaka, ila kwanini kabla hujatoa hukumu usikae naye na kuzungumza naye kuhusiana na vitu unavyopenda na usivyopenda? Kumtafsiri vibaya wakati hujamwambia namna unavyoumizwa na usiri wa mambo yake wakati mwingine ni kama kumwonea tu.

Kuna wengine mazingira waliyokulia yamewatengeza kuwa katika hali ya namna hiyo. Kila kitu anaficha. Akipoke simu anataka mwingine asisikie, akipokea sms anataka akaisomee katika mazingira ya pekee yake.

Wakati mwingine katika ufichaji huo kunaweza kuwa hakuna kitu cha maana wala cha kutisha kinachomsukuma kufanya hivyo zaidi ya mazoea tu.

Kwani wangapi wakiongea huwa kama wanagombana? Kwani kila muda huwa na hasira ndipo huwa wanaongea hivyo? Hapana. Ni mazoea na mazingira waliyokulia ndiyo yamewatengeza kuwa katika hali kama hiyo. Kaa naye zungumza naye kila kitu usichopenda.

Kama huo usiri wake unakupa tafsiri tofauti kwanini uumie wakati una uwezo wa kuongea na muhusika moja kwa moja?

Baada ya kuongea naye na kuona bado kama humuelewi hapo unaweza kuomba ushuri wa kitaalamu ili kujua nini ufanye uweze kujua zaidi kipi kiko nyuma ya usiri wake. Narudia tena, kama hujaongea na mwenzako juu ya tabia f’lani anayofanya alafu ukataka kumuhukumu huko ni kumuonea.

 

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU