MIAKA 5 KIFO CHA MAFISANGO, SIMBA WANATOKA KAPA

MIAKA 5 KIFO CHA MAFISANGO, SIMBA WANATOKA KAPA

713
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

NI miaka mitano sasa Simba haijanyakua ubingwa wa Ligi Kuu au kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa kutokana na kushindwa kufanya vema kwenye misimu yote hiyo.

Lakini wakati Simba ikitimiza miaka mitano bila ya kombe lolote, pia jana ilikuwa ni kumbukumbu ya kifo cha  kiungo wao, Patrick Mutesa Mafisango, aliyefariki dunia Mei 17, mwaka 2012.

Mafisango alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Veta Chang’ombe, alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki, ambapo gari lake lilipoteza mwelekeo, kuacha njia na kutumbukia mtaroni na kugharimu maisha ya mchezaji huyo.

Kifo chake kiliacha taharuki hasa kwa wapenzi wa soka, kwani alikuwa ni mchezaji wa aina yake Simba, hakuwahi kuwa nahodha wa timu kama kwenye timu yake ya APR ya Rwanda, lakini alikuwa ni zaidi ya nahodha kwani aliweza kuhamasisha wenzake kucheza bila kuchoka na kutokata tamaa hata pale Simba inaposhambuliwa na timu pinzani au hata kufungwa.

Alifariki katika wakati ambao klabu yake ilikuwa inatarajia mengi kutoka kwake. Huyu alikuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Simba na hakuna kingine kilichokuwa kinamfanya awe tegemeo zaidi ya jitihada zake uwanjani.

Mafisango ni mmoja wa wachezaji waliovaa medali ya ubingwa akiwa Simba ambapo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa klabu hiyo ambayo mpaka sasa wengine wanajivunia medali za Mtani Jembe na Mapinduzi tu.

 

Siku hizi Simba ndege wanaziona tu zikipita juu, mashindano ya kimataifa yamekuwa makubwa sana kwao, tiketi aliyoiacha Mafisango ndiyo ilikuwa ya mwisho na mpaka sasa wameshindwa kupata tiketi nyingine.

 

Wekundu wa Msimbazi siku hizi haiwezi tena kuifunga Yanga mabao 5-0, nyakati zimebadilika sana sasa Simba inafungwa na Yanga mara mbili kwa msimu mmoja.

 

 

Licha ya kucheza sana, lakini Simba wameshindwa kunyakuwa ubingwa tena msimu huu kutokana na kuchanga karata zao vibaya.

Leo hii wanaiangalia Yanga ikitetea ubingwa wake kwa mara ya tatu huku wao wakiendelea kuusotea kwa mwaka wa tano sasa toka walipochukua kwa mara ya mwisho mwaka 2012.

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakisononeka kwa muda mrefu na hasa majina wanayopewa na watani zao Yanga yamekuwa mwiba mchungu ndani ya mioyo yao na wanatamani Mungu aitendee muujiza.

Karata pekee iliyobaki kwa Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa ni Kombe la FA, ambapo kama watafanikiwa kuifunga Mbao basi watakuwa wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.

Mechi hiyo imekuwa ndio roho pekee kwa sasa na kila shabiki anatamani kuona timu hiyo ikiibuka na ushindi ili kuondoa kelele za wapinzani wao wa jadi Yanga.

Lakini kiuhalisia ukiangalia kinachoiumiza Simba kwa sasa ni kukosekana mtu wa mwisho (finisher) anayesima mbele kumalizia kazi za mawinga na viungo, badala yake mabao karibu yote yamekuwa yakifungwa na viungo na mawinga ilihali kuna ‘mtu’ maalumu wa kazi hiyo.

Si siri ubutu wa washambuliaji ndio unaoitesa Simba, ndio maana hata kila siku wanaendelea kumkumbuka marehemu Mafisango kutokana na umuhimu wake aliokuwa nao ndani ya Simba.

Kila shabiki wa Simba anatamani kuona mafanikio ya timu hiyo lakini wakati umekuwa tofauti, leo Mafisango amekuwa ndio mchezaji anayekumbukwa zaidi ndani ya timu hiyo.

Wakati watu wakimkumbuka Mafisango na kumwombea mbele ya Mwenyezi Mungu akitimiza miaka mitano huko aliko, Simba pia inaomba miujiza na kumuomba Mungu angalau wapate mafanikio ya kutwaa ubingwa na kurejesha heshima ya klabu hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU