KWA MEDALI HIZO RT WAKIKAZA ZAMA ZA NYAMBUI, BAYI ZITARUDI

KWA MEDALI HIZO RT WAKIKAZA ZAMA ZA NYAMBUI, BAYI ZITARUDI

394
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

MASHINDANO ya vijana chini ya umri wa miaka 18 Afrika Mashariki na Kati (EAAR) maarufu Kanda Tano, yamefika tamati Jumapili iliyopita.

Mashindano hayo yalifanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Watanzania tuling’ara vilivyo na kutoana jasho na Wakenya.

Mwaka huu mashindano hayo yameshirikisha nchi saba za ukanda huo, ambazo ni Sudan, Sudan Kusini, Zanzibar, Kenya, Eritrea na Tanzania Bara, ambao tulikuwa wenyeji.

Katika mashindano ya mwaka huu, Kenya imeongoza kwenye matokeo ya jumla, baada ya kuzoa medali nane za dhahabu, nne za fedha na shaba tatu.

Kwa upande wa Tanzania Bara, tulipata medali saba za dhahabu, fedha saba na nane za shaba, huku Zanzibar wakishika nafasi ya tatu kwa kuvuna dhahabu nne, fedha tano na shaba nne.

Somalia ilishika mkia katika mashindano hayo, ambao hawakupata medali hata moja, wakati Tanzania tukishika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanawake, baada ya kushika namba moja, tukifuatiwa na Kenya, huku Zanzibar wakishika nafasi ya tatu kwa wanaume.

Kutokana na kufanya vizuri, Tanzania tumepata nafasi 13 za wanariadha kwenda kushiriki mashindano ya mbio za dunia yatakayofanyika Julai, mwaka huu, mjini Nairobi, Kenya, katika vipengele vinne.

Haya ni mafanikio makubwa kuwahi kuyapata Tanzania, kwani timu yetu ilikuwa na wachezaji 23 na kupata idadi hiyo ya nyota 13, ambao watakwenda kushiriki mashindano hayo ya dunia.

Hamasa iliyotolewa kwa wanaridhaa hao, ilikuwa chachu kubwa ya vijana wetu kujituma, wakiamini nyuma yao kuna watu wanawaunga mkono.

Pamoja na hamasa, njia zilizotumika kuchagua timu nazo zilikuwa sahihi, ambapo baada ya kuchaguliwa, vijana hao walikaa kambini Kibaha kwa wiki moja na ndiyo maana tulionekana kuwa na kikosi bora.

Safari hii kila aina ya mbio tulikuwa na mkimbiaji, jambo ambalo lilisaidia kupata medali nyingi kwenye mashindano hayo na Rose Seif akifanikiwa kuvunja rekodi kwa kuondoka na medali mbili za dhahabu.

Pamoja na Rose, wanariadha wengine Watanzania waling’ara kwenye mbio za vijiti za mita 400 na zile za 1600 kwa wavulana, lakini pia zile za mita 1500 na 3000.

Vijana wetu walionekana kupania kukomesha uteja kwa Wakenya, ambao walikuwa wakiitesa Tanzania kwa miaka mitano na kupunguza pengo la medali kutoka nne hadi moja.

Uwepo wa Wilhelm Gidabuday, ambaye sasa ndiye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), umeonekana kuleta mabadiliko makubwa katika shirikisho hilo.

Mwanaridha huyo wa zamani, Gidabuday alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipinga uendeshwaji wa RT, kabla ya kuingia madarakani na kuonekana kuleta mabadiliko kwa muda mfupi.

Jambo linalofanya wadau kuanza kuamini yale aliyokuwa akiyalalamikia kipindi akiwa nje ya uongozi yalikuwa ya kweli, kwani tayari RT imeonekana kuanza kufufuka baada ya kupoteza mwelekeo na riadha kushindwa kupiga hatua.

Huu ni mwanzo mzuri kwa RT, bila shaka mwenendo huu ukiendelea zama za akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui zinaweza kurudi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU