MBAPPE? ISCO? NANI KUIRITHI JEZI NAMBA 10 REAL MADRID?

MBAPPE? ISCO? NANI KUIRITHI JEZI NAMBA 10 REAL MADRID?

948
0
KUSHIRIKI

MADRID, Hispania

BILA shaka, kiungo mshambuliaji wa Real Madrid, James Rodriguez, ameamua kuwa huu ndio msimu wake wa mwisho kuitumikia miamba hiyo ya Hispania, baada ya staa huyo anayevaa jezi namba 10 kuonekana akiwaaga mashabiki katika dimba la Santiago Bernabeu Jumapili iliyopita, walipokuwa wakiivaa Sevilla.

Nahodha huyo wa timu ya Colombia, mwenye thamani ya euro milioni 75, ni wazi atakayesajiliwa kuirithi jezi yake hiyo atakuwa mtu muhimu katika kikosi cha kocha Zinedine Zidane.

Rodriguez alitua Madrid baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2014, na kuirithi nafasi ilyoachwa wazi na fundi wa Kijerumani, Mezut Ozil, ambaye alitua Arsenal.

Jumla ya mashabiki 45,000 walijitokeza Bernabeu kumkaribisha, wengi wao wakiwa ni Wakolombia na tangu hapo mauzo ya jezi yake yakawa ni mazuri. Wanunuzi wakubwa wakiwa ni mashabiki kutoka Amerika Kusini.

Sasa anaondoka, nani kuirithi jezi yake namba 10?

Luka Modric anatajwa kuwa mmoja wao, hasa kwa sababu alishawahi kuitinga akiwa na timu ya taifa ya Croatia, huku Marco Asensio pia akitajwa, alipokuwa timu ya taifa ya Hispania chini ya miaka 19 mwaka jana, aliivaa namba hiyo.

Kiungo mnyumbulifu mwenye uwezo wa kuufanya mchezo wa soka kuwa mwepesi, Isco, pia anahusishwa na kuirithi jezi namba 10, kwani hata alipokuwa akiitumikia Hispania chini ya miaka 21 alikuwa akivaa pia.

Hata hivyo, namba hiyo huenda ikatunzwa kwa ajili ya mchezaji mkubwa atakayesajiliwa hivi karibuni, Kylian Mbappe wa Monaco ana asilimia kubwa ya kutua Madrid.

Tangu LaLiga ianzishe mtindo wa namba kwenye vikosi, jezi namba 10 ina historia ya kuvaliwa na mastaa wakubwa nane pale Madrid: Michael Laudrup, Clarence Seedorf, Luis Figo, Robinho, Wesley Sneijder, Lassana Diarra, Mesut Ozil na Rodriguez mwenyewe, lakini kabla ya hapo, wachezaji kama Ferenc Puskas, Gunter Netzer, Gheorge Hagi na Robert Prosincki waliwahi kutumia namba hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU