NAMNA HII NDIVYO ANAPASWA KUWA MWANDANI WAKO

NAMNA HII NDIVYO ANAPASWA KUWA MWANDANI WAKO

781
0
KUSHIRIKI

NA RAMADHANI MASENGA,

BAADHI wapo katika uhusiano, ila ni kama wako utumwani. Mambo wanayofanyiwa na maneno wanayoambiwa hayastahili kwa watu walio katika uhusiano, au wenye urafiki wenye kuashiria safari hiyo. We upo katika uhusiano wa namna gani? Kuna sifa za mpenzi wa dhati. Je, wako anazo?

Kama upo na mtu anayekufanya ujute na ujihisi kama  hauna mtu ilhali unaye, unadhani unastahili kusema kuwa uko katika uhusiano kamili wa mapenzi?

Kuna urafiki wa kingono na uhusiano wa kimapenzi. Ni lazima hapo utofauti ujulikane. Urafiki wa kingono ni ule wahusika wapo pamoja kwa sababu ya vitu fulani, ila katika nafsi zao hakuna faraja na mashiko stahiki.

Katika urafiki wa aina hii ni rahisi mmoja kumuumiza mwenzake kimakusudi kwa sababu huwa hana maana kubwa katika moyo wake.

Ona, upo naye katika uhusiano, ila ana vimada wengi. Utasema unapendana naye huyu? Kila ukijaribu kusema anakuona mjinga na kila unapotaka kumsahihisha anakwambia maisha ya kubwanwabanwa hawezi. Ni kwa namna gani huyu utasema ni mtu sahihi katika maisha yako?

Wapo wanaostahili kuitwa watu bora katika maisha yako. Yule anayekuja kwako kwa dhamira ya nafsi yake na mwitikio halisi wa moyo wake. Huyu kwako atajenga uhusiano kamili wa mapenzi wenye kushikiliwa kikamilifu na upendo halisi. Hata siku moja hatataka kukuumiza wala kukukera. Atakujali na kukuthamini. Kwa kila jambo unalotakiwa kufanyiwa atakufanyia namna unayotakiwa na kwa staili utakayopenda.

Hata iweje, kwako atajitahidi kuwa mwema na mtakatifu kadri inavyowezekana. Ni raha sana kuwa na mtu wa aina hii. Mtu halisi na wa hadhi ya maisha yako.

Kama mtu anakujali na kukuthamini kwa nia halisi, ni kwanini usijivunie kuwa naye katika maisha yako? Ni safi kuwa katika mahusiano, ila ni safi zaidi kuwa na mtu sahihi katika mahusiano yako.

Nimeona wengi. Walioamua kuingia katika mapenzi kwa furaha na amani. Na katika hao pia nimeona wengi wenye kulia na kuona mapenzi kama janga katika maisha yao. Wewe upo upande gani?

Mwangalie vizuri uliye naye, je, anapaswa kuwa nawe katika maisha yako? Anakujali, anakuthamini na kukupa furaha kila inapohitajika?

Mchague mtu bora katika maisha yako. Japo haiwezekani kuwa na mtu asiyekukosea, ila kuwa na mtu mwenye kuonesha kujali na kukuthamini katika maisha yako. Kuna watu wengi. Wengine wana mvuto sana kuliko wengine. Wapo wenye uwezo mkubwa sana kifedha kuliko wengine. Na baadhi wana madaraka makubwa sana kuliko wengine. Kwa sifa hizo, hufai kuchagua mtu wa maisha yako. Angalia ni nani anagusika katika hisia zako. Gari na kila kitu chake weka kando. Chunguza nafsi yako katika upande wa upendo, kisha tazama kama naye kwake anavutika kiupendo au kitamaa nyingine.

Kuna wakati mwingine huwa nachoka. Unakuta binti anasema natafuta mume mwenye gari, elimu ya kutosha pamoja na fedha nyingi. Ni kweli! Na kila mmoja anapenda kuwa na mke au mume mwenye vitu hivi. Ila jiulize, yako wapi mapenzi yake kwako? Yako wapi mapenzi yako kwake? Kwa hiyo kila mwenye gari na mali nyingi anafaa kuwa mpenzi wako? Katika namna hiyo, ni kwa namna gani utaona mapenzi yana thamani na maana katika maisha yako?

Mapenzi si vile unavyofikiri, bali ni vile unavyojihisi katika nafsi yako. Katika akili ya kawaida kila mtu atasema gari na nyumba nzuri ni sifa za kuwa na mtu katika maisha yako, ila katika hisia halisi ni nafsi inayochagua mtu katika maisha yako. Na kama ukishindwa kuishirikisha katika maamuzi yako, jua umepotea.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU