VITA YA GUARDIOLA, KLOPP NA WENGER… VINAWEZA KUAMULIWA NA MECHI YA MTOANO

VITA YA GUARDIOLA, KLOPP NA WENGER… VINAWEZA KUAMULIWA NA MECHI YA MTOANO

471
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

KOCHA wa Chelsea, Antonio Conte na wa Tottenham, Mauricio Pochettino, tayari wameshajua nafasi zao kabla za mechi wa mwisho wa msimu huu zitakazochezwa Jumamosi hii.

Lakini kazi ngumu watakayokuwa nayo makocha watatu, Pep Guardiola wa Manchester City, Jurgen Klopp wa Liverpool na Arsene Wenger (Arsenal), kugombea nafasi mbili zilizobaki na kuwapo ‘top four’.

Pointi tatu pekee ndizo zimewatenganisha anayeshika nafasi ya tatu, nne na ya tano ambao ni Arsenal na kama watalingana kwa mabao ya kufunga na kufungwa basi itabidi timu mbili kati ya hizo zicheze mechi moja kwa ajili ya kupata timu moja itakayoshika nafasi ya nne.

Manchester City wamepiga hatua kubwa ya kujiweka vizuri katika harakati za kusaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, baada ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya West Brom juzi Jumanne. Ikiwa kikosi hicho cha Guardiola kitashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Watford, basi watapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Liverpool wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 73, wakijua kabisa kwamba watacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kama wakiifunga timu ambayo imekwishashuka daraja, Middlesbrough kwenye Uwanja wa Anfield, Jumapili hii.

Pointi moja nyuma ya Liverpool ni Arsenal wanaoshika nafasi ya tano, watategemea matokeo mabaya ya wengine pamoja na kuifunga Sunderland mabao 2-0 kwenye mchezo wa juzi Jumanne na kupata matumaini ya kuwamo katika timu zitakazocheza michuano hiyo ya Ulaya msimu ujao.

Jumapili, City watasafiri kuifuata Watford, Liverpool wataikaribisha Middlesbrough na Arsenal watacheza nyumbani dhidi ya Everton.

Hivyo kwa hali hiyo ya kukaribiana kwa pointi na mabao, kuna uwezekano mkubwa kwa moja ya timu itakayoingia ‘top four’ itaamuliwa kwa kucheza mechi ya mtoano kwenye uwanja wa ugenini kwa timu zote mbili. Ingawa kwa timu nyingine huamua kwa kuangalia kwa matokeo ya timu hizo mbili zilipokutana ilikuwaje.

Kanuni C ya msimu huu (2016/17) wa Ligi Kuu England: “Mwisho wa msimu timu ambayo inataka kuchukua ubingwa au kushuka daraja au kufuzu michuano yoyote ikiwa wanalingana kwa pointi, tofauti ya mabao na mabao waliyofunga, basi klabu hizo zitacheza mchezo mmoja wa mtoano kwenye uwanja wa ugenini kwa wote ambao utapangwa na bodi.”

Hali hii inaweza kuwakumba City na Liverpool, ambapo itabidi wacheze kumpata mshindi wa tatu na wa nne ambao watapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumwacha Wenger kwenye mataa.

Ikiwa City atatoka sare ya mabao mengi kama 3-3 kwenye Uwanja wa Vicarage Road dhidi ya Watford, nao Reds wakaichapa Middlesbrough mabao 3-0.

Matokeo ya aina hii yatafanya timu hizo zilingane kwa pointi 76 na mabao 78 ya kufunga na tofauti ya mabao kuwa 36, hiyo itawafanya kucheza wenyewe kwa wenyewe kumsaka nani atakuwa nafasi ya tatu, huku Arsenal wakichinjiwa baharini katika nafasi ya tano, bila kuangalia matokeo yoyote atakayoyapata dhidi ya Everton.

Lakini kama Liverpool watafungwa mabao 2-0 na Middlesbrough kwenye mechi hiyo ya mwisho na Gunners kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Everton, matokeo hayo yatawafanya Arsenal na Liverpool kulingana kwa pointi 73 wakiwa na mabao 75 ya kufunga na tofauti ya mabao kuwa 31.

Basi ikitokeo hivyo, Manchester City watapeta katika nafasi yao ya tatu hata wakifungwa na Watford, akiwaacha Liverpool na Arsenal kucheza mechi ya mtoano kuamua nani anashika nafasi ya nne na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Man City na Arsenal wanaweza kukutana katika mechi ya mtoano, ikiwa Watford watawafunga 4-0, kisha Gunners waichape Everton bao 1-0, timu hizo zitamaliza msimu zikiwa na pointi 75 wakiwa na tofauti ya mabao 32 na kufunga mabao 75.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU