YANGA MAFURIKO MWANZA

YANGA MAFURIKO MWANZA

1855
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR

WAKATI Yanga wakitarajia kuondoka leo na ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa ajili ya mchezo wao wa mwisho wa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC, mashabiki wa klabu hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza kumiminika Mwanza kushuhudia tukio la timu yao kukabidhiwa mwari wao.

Yanga ambao wana pointi 68, mahasimu wao Simba wanashika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tatu, watahitaji kushinda mabao 13 dhidi ya Mwadui katika mchezo wao wa mwisho utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili waizuie miamba hiyo ya Jangwani isiweze kutetea taji lao.

Lakini matokeo hayo yatakuwa na faida kwa Simba ikiwa Yanga watafungwa na Mbao FC kwenye mchezo wao huo utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, jambo ambalo litakuwa gumu na ndio maana mashabiki wa klabu hiyo wameanza kutua mjini humo kwa ajili ya kushuhudia tukio la kukabidhiwa taji hilo.

Mashabiki wameanza kumiminika katika hoteli na nyumba za wageni za mikoa ya Geita, Simiyu, Bariadi, Dodoma, Morogoro na Tanga, huku Dar es Salaam wakianza kujiandaa kwa kukodisha magari aina ya Coaster kwa ajili ya safari hiyo kwenda kujumuika kwenye sherehe hizo za ubingwa.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, akizungumza na BINGWA, amesema maandalizi yote kwa ajili ya safari yamekamilika ambapo wanakwenda mkoani humo kwa kazi moja ya kuwashusha daraja Mbao FC.

“Kila kitu kipo vizuri na kama unavyojua Yanga ina mashabiki wengi sana jijini Mwanza kuliko hata Dar es Salaam, tayari kuna mashabiki kutoka katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita, Bariadi na Bukoba wameanza kuingia kumiminika kwa ajili ya kushuhudia timu yao ikivikwa taji la ubingwa msimu huu,” alisema Mkwasa.

Alisema kikosi cha timu hiyo kitaondoka na wachezaji wake wote kwenda Mwanza kwani wamedhamiria kuwafunga Mbao FC ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kushangilia ubingwa wao, ambao walijiwekea uhakika wa kuutwaa baada ya kuifunga Toto Africans bao 1-0 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mkwasa aliongeza kuwa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao huo wa Jumamosi, timu itarejea jijini Dar es Salama, Jumapili kuendelea na mipango mingine ya mialiko mbalimbali kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki.

“Baada ya ligi kumalizika tutakuwa na mechi kadhaa za kirafiki, ambapo tutakwenda Mbeya, Iringa, Tanga, Moshi na Arusha, ambapo mashabiki wa Yanga katika mikoa hiyo watapata fursa ya kuiona timu yao ikicheza baada ya kutetea ubingwa. Hivyo tukirudi Dar es Salaam tunaweza kwenda Arusha,” alisema Mkwasa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU