YANGA: SIMBA UBINGWA? MNAOTA NYINYI

YANGA: SIMBA UBINGWA? MNAOTA NYINYI

1332
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

SIKU chache baada ya Makamu wa Rais wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu, kusema kuwa bado hajakata tamaa ya ubingwa mpaka pale watakapomaliza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mwadui, Yanga wameshangazwa na kauli hiyo ya wapinzani wao.

Kaburu alisema bado hawajakata tamaa ya ubingwa na lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mwadui.

“Bado ligi haijaisha hivyo bado sijakata tamaa mpaka pale kwenye mechi ya mwisho, najua tunacheza na Mwadui na lolote linaweza kutokea katika mchezo huo,” alisema.

Yanga ambao tayari wana uhakika wa ubingwa baada ya kufikisha pointi 68 huku wakiwazidi kwa pointi tatu Simba ambao ili wawapore mahasimu wao hao taji lao, wanapaswa washinde mabao 13 kwenye mchezo huo wa mwisho.

Simba ambayo awali ilikuwa na matumaini ya ubingwa imejikuta ikiachwa njiani na Yanga baada ya kuzidiwa zaidi kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga, jambo linalowapa matumaini makubwa mahasimu wao wa kutetea taji lao.

Kufuatia kauli hiyo ya Kaburu, kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali, ameibuka na kuwashangaa wapinzani wao hao na kuwashauri wasubiri msimu ujao.

“Yaani mtu afunge mabao 13 ndio aweze kutufikia, halafu unasema bado hujakata tamaa, labda wajipange kwa msimu ujao lakini kwa huu naona hawana chao,” alisema.

Jumamosi hii Yanga wanatarajia kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu huu wakati wakikamilisha ratiba kwa kucheza na Mbao mjini Mwanza, huku Simba wakifunga pazia la ligi na Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU