DUNIA YA MKE WANGU UTANGULIZI (06)

DUNIA YA MKE WANGU UTANGULIZI (06)

344
0
KUSHIRIKI

NA EMAN FISIMA, 0654 076 265

Kuanzia mwanzo wa mipaka ya Ethiopia, hadi nchi za jirani, maiti zilikuwa zimetapakaa juu ya ardhi. Huku harufu mbaya ikiendelea kuharibu hali ya hewa ya maeneo hayo, kwa sababu mwili wa binadamu ukishaoza ni chukizo kubwa kwa pua inayopenda kuhisi harufu nzuri.

Hali hiyo ilizidi kumuogopesha KAI na kumfanya ajione kama yuko kuzimu. Alipiga hatua za haraka, akiutafuta mwili wa JULIA mke wake kipenzi, japo alikuwa akihitaji utulivu mkubwa katika kufanya hivyo. Hurufu kali iliyosambaa kutokea katikati ya nchi nyingine hadi ile aliyopo, ilimfanya kuzikagua maiti kwa tabu na kwa haraka sana.

Hakika ugonjwa wa Ebola ulikuwa unakwenda kummaliza kabisa binadamu anayeishi Afrika na yule anayeishi pembeni ya bara hilo. Hakuna binadamu aliyekuwa hai eneo alilokuwepo Kai. Kwani ugonjwa huo ulishaanza kuambukiza kwa njia ya hewa.

Kai alikuwa akilia muda wote, ingawa alikuwa amejichoma sindano ya kujikinga na ugonjwa huo hatari uliopata kutokea karne 21. Alilia kwa sababu, juhudi ya kumtafuta mke wake aliyokuwa ameifanya kwa kila hali, ilikuwa  inakwenda kuvunja matumaini ya kumuona. Shauku yake ilikuwa ni kutaka kumuona mke wake akiwa hai au akiwa amekufa.

ILIPOISHIA 

Mungu huwa haishiwi maswali ya kumuuliza mwanadamu, alimuuliza Kai kupitia nafsi yake iliyokuwa inazungumza ndani ya moyo wake.

Kai alijikuta akijiuliza swali, endapo Mungu atampa Julia awe mke wake, yeye atampa  Mungu nini. Swali hilo alijiona kama amejiuliza yeye lakini ukweli ni kwamba, Mungu muumbaji ndiye aliyekuwa ameuulizia kupitia nafsi yake.

SASA ENDELEA

“Mungu nakuahidi endapo Julia atakuwa mke wangu, nitakutumikia siku zote za maisha yangu.”

Usiku mnene uliingia Kai akiwa pale pale mlimani. Aliamua kulala hadi asubuhi, asubuhi ilipofika, aliendelea kukaa mlimani mchana na hadi usiku  mwingine. Akiwa anauwaza uzuri wa msichana Julia, Mungu alimuuliza swali jingine.

Nafsi ya Kai ilijiuliza ikiwa je Julia si mwanamke mwema je, itakuwaje. Je, Mungu atampa mke asiye mwema? Swali hilo lilikuwa gumu kwa upande fulani. Aliliogopa  kulijibu ingawa majibu alikuwa nayo. Upande mwingine wa nafsi yake ulijiambia kuwa ni kweli, Mungu hawezi kumpa mke asiye mwema, hata kama atakuwa amemuomba  kwa kilio cha machozi na damu. Kwa sababu uzuri wa msichana Julia, Mungu pekee ndiye anayeujua.

Kai alimjibu Mungu jibu la juu juu kuwa anaamini Julia ni mwanamke mwema na mwenye tabia nzuri. Lakini Mungu alimuuliza tena kama je si mwanamke mwema ampe hivyo hivyo. Swali hilo lilikuwa gumu aliiambia nafsi yake kuwa atalijibu baadaye.

Usiku ulipoingia, Kai alibeba begi lake na kushuka mlimani. Mwili wake ulikuwa umechoka na njaa ilikuwa inakaribia kumuua, maana ni siku ya pili alikuwa hajatia chakula chochote tumboni. Alirudi chuoni akaoga na kula chakula, alijipumzisha kitandani. Macho yake yalitazama darini kwa muda kidogo, alimuwaza Julia kabla usingizi mzito, usingizi aliokuwa ameuzuia kwa siku mbili zilizopita kumchukua.

Baada ya miezi mitatu, siku moja Kai akiwa peke yake kwenye chumba chake cha siri cha maabara, alipokea simu kutoka nyumbani Tanzania. Mama yake ndiye aliyekuwa amempigia, ambapo alimtaka mwanaye kurudi mara moja nchini akimtaarifu kuwa kulikuwa na harusi ya dada yake.

“Mama kwani harusi ya dada tayari?” aliuliza Kai.

“Ndio mwanangu, fanya upesi urudi, kwani Jumamosi ijayo ndio harusi yake.”

“Mmh mama mbona mapema?”

“Ndio hivyo mwanangu shemeji yako hataki kuchelewa kuoa.”

“Basi sawa, kama ni hivyo si mbaya keshokutwa nitaianza safari ya kuja huko.”

“Sawa mwanangu nakutakia safari njema.”

Kai alikuwa na furaha baada ya kusikia dada yake anaolewa wiki ijayo. Alijiandaa kwa safari ya kuelekea Tanzania. Lakini alikwenda kwanza kuomba ruhusa kwa makamu mkuu wa chuo. Aliruhusiwa kuondoka, lakini aliambiwa kuwa Desemba 13 atatakiwa kwenda maabara ya Hatic iliyopo nchini Marekani.

Maabara hiyo ilikuwa inawahitaji wanafunzi wenye vipaji kwa ajili ya kujifunza na kusaidia kutafuta dawa ya ugonjwa wa UKIMWI na magonjwa mengine hatari, ukiwemo ugonjwa wa Ebola ulioanza kusikika barani Afrika, hasa katika nchi za Ethiopia na Ghana.

Kesho kutwa ilipofika, Kai alipanda ndege ya Fly Emirates na kuelekea Tanzania. Mawazo juu ya ndoa ya dada yake hayakuwepo sana kwenye akili yake. Muda mwingi alikuwa akimuwaza Julia, msichana aliyekuwa akimpa mateso makali mithili ya shoti ya umeme kuhusu mapenzi.

Alijiuliza hivi itakuwaje siku atakapofunga ndoa na Julia, atakuwa na furaha jinsi gani. Na pia alijuliza itakuwaje siku atakapoona Julia ameolewa na mwanamume mwingine, alijihoji maumivu hayo atayahisi jinsi gani. Alitokwa na machozi mengi, akiomba hilo lisipate kutokea, maana likitokea litaharibu kabisa mfumo mzima wa maisha yake.

Siku ya Jumatano, saa 9:30, Kai aliwasili Dar ss Salaam nchini Tanzania na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwao Kigamboni.

Wazazi wake pamoja na dada yake bado hawakupendezwa na hali aliyokuwa nayo Kai. Bado waliuona udhahifu wa mwili na unyonge aliokuwa nao. Lakini Kai aliwakuta wenye nyuso za furaha, tena furaha kubwa zaidi. Alijua furaha hiyo ni kwa sababu dada yake Melina alikuwa anakwenda kuolewa. Usiku Kai alikaa na dada yake. Licha ya undugu waliokuwa nao Kai na Melina walikuwa ni ndugu wanaopenda kupita kawaida. Kila mmoja alipenda kumtania mwenzake na kumshauri mambo mengi, walikuwa ni zaidi ya kaka na dada.

“Siamini kama ndio unatuacha na kwenda kwa mumeo,” aliongea Kai kwa tabasamu.

“Amini tu maana wakati umefika,” alijibu Melina.

“Lakini hata hivyo naona kama ndoa yenu imewahi vile?”

“Mmh Kai siku hizi ukichelewa tu utakuta mume si wako.”

“Kwani mtu wa kwanza kufanikisha ndoa ni mwanamke au mwanamume.”

“Mwanamume ndio mtu wa kwanza, kwa kuwa yeye ndiye anayeoa, lakini mwanamke hufanikisha jambo hilo haraka ikiwa atamshawishi mwanamume kwa kila jambo akimpenda na kumthamini.”

“Sawa, naona umefanikiwa kumteka Franco,”

“Tena nimemshika kikweli, ananipenda ajabu.”

“Hongera, naona wivu.”

“Haaaa! Haa haa haa! Unaona wivu mi kuolewa au unanipenda dada ako.”

“Sina maana hiyo dada.”

“Kumbe?”

“Naona wivu kwa sababu hata mimi natamani kumuoa Julia,” alijibu Kai kwa huzuni kidogo.

Melina alimshika Kai begani na kumwambia:

“Usiache kumuomba Mungu, siku si nyingi nauona muujiza wake juu yako.”

Kai alishangazwa na maneno hayo ya dada yake. Alimtazama kwa furaha ndogo na kisha akamjibu.

“Sizioni dalili zozote za Julia kuwa mke wangu, naona moyo wangu ushaanza kukata tamaa, nimemweleza Julia vile nilivyoweza lakini hajaonyesha hata chembe ya kukubali. Yuko mbali kabisa na mateso yangu wala hajali. Bila shaka naona kabisa kuna mtu mwingine anampenda.”

“Usiseme hivyo Kai, mimi Melina ninakuhakikishia kuwa Julia anakupenda na utakwenda kumuoa.”

“Mmh! Melina unanifariji tu wala hakuna kitu kama hicho.”

“Niamini mimi Kai.”

Melina alizungumza kwa ujasiri, ujasiri huo ulikuwa wa kweli kwa kuwa Kai aliuona machoni. Alishangazwa na kujiamini  huko kwa dada yake. Ihali kuwa yeye mwenye kumpenda Julia, hakuwa nao tena. Hakuelewa kabisa ni kwanini dada yake alikuwa na nguvu kiasi kile.

Melina alimwacha Kai na maswali, akainuka na kwenda kulala. Akiwa amebaki pale bustanini, Kai aliinua macho yake na kulitazama anga lililokuwa na nyota chache, nyota alizokuwa ana uwezo wa kuzihesabu. Aliitazama nyota moja iliyokuwa na mwanga mwekundu iliyokuwa yenye kung’aa kuliko zingine. Nyota ile ilikuwa imejitenga pembeni.

Nini kitafutia usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU