VIFAA VYAZIDI KUTUA SIMBA

VIFAA VYAZIDI KUTUA SIMBA

3606
0
KUSHIRIKI

SAADA SALIM NA ZAINAB IDDY

KLABU ya Simba imeendelea kufanya kweli kwenye dirisha la usajili, baada ya kumsainisha beki wa Mtibwa Sugar, Ally Shomari, kwa mkataba wa miaka miwili, huku ikikaribia kumalizana na wachezaji wengine wawili wa kigeni ambao tayari wanadaiwa kuwapo nchini.

Wachezaji hao wa kigeni ni kinara wa mabao wa Ligi Kuu Zambia, Bwalya Walter na nyota wa Uganda, Shaban Nassuuna, wakiwa wameletwa kusaidiana mchezaji mwingine anayesubiriwa kwa hamu Msimbazi, Emanuel Okwi.

Bwalya, ambaye amekuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu Zambia mara mbili, msimu huu akifungia timu yake ya Nkana Rangers mabao 24, anadaiwa kuwa tayari ameshatua jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha ndani cha habari kimeliambia BINGWA jana, kuwa nyota huyo, Bwalya, ambaye alitoswa timu ya Taifa ya Zambia na kocha Wedson Nyirenda kwasababu ya uraia wake kuwa na utata kutokana na kuzaliwa na mama mwenye asili ya Jamhuri ya Kongo na baba yake kuwa ni Mzambia, amekubali kumwaga wino na wakati wowote atakamilisha usajili wake.

Mkongwe wa klabu ya Simba, Amri Said, aliwapongeza viongozi kwa usajili walioufanya, lakini anaamini kwamba wakimpata Bwalya na Okwi, timu itakuwa tishio kwenye safu ya ushambuliaji.

“Huyu Bwalya ni mchezaji mzuri sana na Simba inatakiwa kumpata nyota huyo ili kuimarisha zaidi safu ya ushambuliaji, ukizingatia msimu uliopita walikosa ubingwa kwasababu ya mabao machache,” alisema beki huyo wa kati wa zamani.

Kwa Shaban, ameshaanza mazungumzo na Simba na wakati wowote watakamilisha usajili wake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Shaban yupo hapa nchini, amefanya vizuri sana Uganda, ambapo amefunga mabao 30. Mabao 16 katika Kombe la Ligi, saba akifunga Ligi Kuu Uganda, mengine saba katika Kombe la Mikoa ya Uganda,” kilisema chanzo chetu.

Naye Shomari, ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi na kiungo wa kati na pembeni, amesaini mkataba huo wa miaka miwili baada ya kuichezea Mtibwa kwa miaka mitatu.

Akizungumza mara baada ya kumalizana na Simba, Shomari alilimbia BINGWA kuwa amejiunga na Simba baada ya kukubaliana mambo muhimu ya kimkataba, lakini kubwa anahitaji kupata changamoto.

“Nimekuja Simba kutafuta changamoto nyingine. Ingawa nacheza nafasi nyingi, lakini najua nitakuwa na kazi ya kujiweka fiti ili kupata namba kutokana na Simba kuwa na wachezaji wengi wazuri,” alisema.

Naye Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu‘, amesema usajili wa mchezaji huyo ni mwendelezo wa kutaka kuboresha kikosi chao ili kiweze kuwa bora na cha ushindani kwenye mashindano ya ndani na nje.

“Mipango yetu ni kufanya usajili makini kwaajili ya mashindano ya ndani na yale ya nje tunayoshiriki, hivyo huu ni mwendelezo, hivyo mashabiki na wanachama wa Simba wasubiri, bado upo usajili wa kishindo unaokuja zaidi ya tuliofanya hadi sasa,” alisema Kaburu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU