YANGA MAFIA

YANGA MAFIA

5031
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

SASA matajiri wa Yanga wameanza kuonyesha ubabe wao kwenye suala zima la usajili baada ya kudaiwa kumalizana na mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, wamemgeuzia nguvu kiungo wao Haruna Niyonzima na kumpiga ‘stop’ asimalizane na mahasimu wao hao.

Tangu kuvuja kwa taarifa za kudaiwa kurejea kwa matajiri wa klabu hiyo ya Jangwani, Seif Magari na Abdallah Bin Kleb akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, tayari wameanza kuwaumiza vichwa wapinzani wao wote wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwamo Simba na Azam FC.

Baada ya matajiri hao wa Yanga kusikia Simba wanamsumbua Niyonzima na tayari wamekwishamtengea Sh. milioni 110, wamekuja juu na kumtaka mchezaji huyo kurejea nchini haraka ili kuja kuelewana nao suala la kuongeza mkataba mpya baada ya ule wa sasa kubakiza miezi michache.

BINGWA limejulishwa kwamba mchezaji huyo atawasili leo kutoka nyumbani kwao Rwanda alikokuwa mapumzikoni, ili kuja nchini kumalizana na matajiri hao baada ya jana kushindwa kufika.

“Niyonzima bado yupo Rwanda, ila kesho (leo) atawasili nchini kwa ajili ya kuja kuelewana juu ya suala la kuongeza mkataba mpya,” kilisema chanzo hicho.

Pia chanzo hicho, kilisema: “Nimezungumza na Niyonzima amesema kweli Simba wanamtaka na wamemsumbua sana, tena walitaka kwenda Rwanda akawakatalia, ila kesho (leo) anakuja nchini baada ya kuitwa na akina Bin Kleb.”

Pamoja na Niyonzima na Ajib kuwa kwenye mipango ya Yanga, mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana walikaribia kumsainisha beki wa kushoto wa Azam FC, Gadiel Michael ila kuna mambo madogo wanayaweka sawa na mpango huo utakamilika leo.

“Gadiel amerejea kutoka Tanga na leo (jana) ilikuwa amalizane na viongozi wa Yanga, lakini kuna mambo yaliingiliana, ila kesho (leo) kila kitu kitakwenda sawa,” kiliongeza chanzo hicho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU