AJIB AMTIA WAZIMU NDEMLA

AJIB AMTIA WAZIMU NDEMLA

7268
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

UKISIKIA kutiwa wazimu ndio huku kutokana na alichokifanya Ibrahim Ajib dhidi ya swahiba wake Said Ndemla, ambapo amemfuata nyumbani kwake akiwa na gari aina ya Toyota Brevis inayosemekana alipewa na Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Taarifa za uhakika zinadai kuwa Ajib aliamua kwenda kumtembelea rafiki yake huyo juzi jioni akiwa na gari hiyo kitu ambacho kilimpagawisha Ndemla na kuanza kuhoji wapi alipolitoa.

Hata hivyo, Ajib hakuweza kuweka wazi zaidi ya kucheka tu na kumwambia rafiki yake huyo kwamba, hilo gari linauzwa na wakamalizana kishkaji namna hiyo na kuendelea na stori zao nyingine.

“Jamaa aliamua kumwibukia rafiki yake huyo (Ndemla) akiwa na gari lake jipya na hata mwenzake alipomuuliza kwamba alilipata wapi, alicheka na kumwambia linauzwa,” kilisema chanzo chetu.

BINGWA lilifanya jitihada za kumtafuta Ndemla ili kuzungumzia tukio hilo, lakini hakupatikana kwenye namba zake zote za simu.

Kitendo cha Ajib kumtembelea Ndemla akiwa na gari yake hiyo mpya, kinaweza kumfanya kiungo huyo asiye na mbwembwe uwanjani ‘kupata bonge la somo’ na kuanza kufikiria ni vipi anaweza kupita njia za rafiki yake huyo ambaye habari zake za kutua Yanga zimeonekana kuwatikisa wapenzi wengi wa soka hapa nchini.

Mbali na Ndemla, mchezaji mwingine ambaye ni wazi atakuwa akikosa usingizi anapofikiria jinsi Ajib alivyotua Yanga, ni kiungo Jonas Mkude ambaye mara kwa mara amekuwa akihusishwa na klabu hiyo ya Jangwani. Inasemekana ‘ndoa’ ya Mkude na Simba inafikia tamati.

Ukiachana na suala hilo, Ajib ambaye anadaiwa kusaini mkataba wa miaka miwili Yanga, ameamua kuvunja ukimya na kueleza yaliyomfanya aondoke Simba.

Ajib aliyezungumza na BINGWA jana jijini Dar es Salaam, alisema anafahamu ni jinsi gani mashabiki wa Simba wanavyojisikia kuhusu kuondoka kwake, lakini alichoshwa na maisha ya viongozi kutomthamini kikosini.

Nyota huyo anayedaiwa kupewa dau la Sh milioni 50 na gari aina ya Toyota Brevis na Yanga, alisema amevumilia mengi ndani ya Simba na ameshukuru kumaliza mkataba wake na sasa kuondoka kama mchezaji huru.

“Najua wazi kuondoka kwangu Simba kutawaumiza mashabiki ambao wengi hawafahamu maisha niliyokuwa nikiishi ndani ya klabu, lakini naomba waniombee huko ninakokwenda.

“Miaka miwili kabla ya kumaliza mkataba wangu Simba nilikuwa naishi maisha mabaya na maumivu niliyokuwa nayapata nilikuwa nayajua mimi na familia yangu nyumbani, lakini nashukuru nimemaliza mkataba wenyewe na sasa naondoka,” alisema.

Ajib aliyewaliza baadhi ya mashabiki wa Simba waliosikia taarifa zake za kuhamia Yanga, amesema hata kutokuwa na mahusiano mazuri na baadhi ya viongozi ndiyo iliyochangia kuondoka kwake klabuni humo.

Alisema ili ufanye kazi vizuri unatakiwa kuwa na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzako, benchi la ufundi, wanachama, mashabiki, viongozi na kufafanua yeye hakuwa akifanya kazi katika mazingira hayo.

“Sikuwa na maelewano mazuri na baadhi ya viongozi (Jina kapuni) ambao wengi walishaniona kama mchezaji ninayeringa, sasa hapa unaweza kuliona tatizo lilipoanzia, lakini nashukuru wachezaji wenzangu, makocha, wanachama na mashabiki ambao muda mwingi tulikuwa nao kwenye kipindi kizuri muda wote ndani ya Simba.

“Mpira ni mchezo wa kutumia sana nguvu, lakini kuna baadhi ya viongozi hawalijui hili wao wanaona mchezaji ni kama mashine ambayo haiwezi kuchoka na kupumzika hapo ukisema umechoka na unahitaji kupumzika unaonekana unaringa, hali hii iliniuma sana,” alisema.

Mchezaji huyo alifafanua kuwa msimu ujao hakutaka tu kucheza Simba na kusema timu anayokwenda imempa ofa ya chini tofauti na ofa ya Simba.

“Timu ninayokwenda haikunipa ofa nzuri kama ofa ninayoiacha Simba, lakini niliamua mwenyewe kuacha ofa ya Simba iliyokuwa nzuri na kwenda kuichukua ofa ndogo, ili niwe na amani ndani ya moyo wangu,” alieleza.

Katika hatua nyingine Yanga wameapa kwamba wataendelea kuibomoa Simba kwani jeuri ya fedha wanayo huku pia wakidai hata Azam FC, hawatabaki salama.

“Hili wimbi la usajili halijawahi kumuacha mtu salama, tumeanza kwa Ajib, tutaangalia kama kuna mwingine atatufaa tutamchukua, pia kule Azam tumeona kuna vifaa kadhaa vinatufaa hivyo tutafanya usajili mwingine wa kushtukiza,” alisema kigogo mmoja wa Yanga.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU