MADEGA AMVAA MALINZI TFF

MADEGA AMVAA MALINZI TFF

677
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

MWENYEKITI wa zamani wa klabu ya Yanga, Iman Madega, ameamua kumvaa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, baada ya kuwa mtu wa kwanza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Madega ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, kwenye upande wa soka anasifika na kauli zake mbalimbali za kishujaa alizokuwa akizitumia wakati akiongoza Yanga kabla ya kuondoka na kumpa kijiti, Yusuph Manji.

Madega amechukua fomu hiyo jana asubuhi katika ofisi za shirikisho hilo zilizopo Karume, jijini Dar es Salaam, hiyo ni dalili njema kwa wanamichezo ambapo awali ilionekana kama Malinzi hatakuwa na mpinzani katika nafasi yake.

Wakati Madega akichukua fomu, Rais Jamal Malinzi amechukua fomu ya kutetea nafasi yake ya kuendelea kuongoza nafasi hiyo kwa miaka minne ijayo.

Mbali na Madega na Malinzi, naye Michael Wambura ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa (FAT) sasa (TFF) ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara (FAM), amechukua fomu kuwania nafasi ya makamu wa rais.

Nafasi hiyo ya umakamu imeonekana kuwa moto wa kutolea mbali baada ya Makamu wa Rais Simba ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF Kanda ya Pwani, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, amechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Dodoma (DOREFA), Mulamu Ng’ambi, ambaye pia ni mwanachama wa Simba naye amechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Upande wa wajumbe wa kamati ya utendaji waliochukua fomu ni Shafii Dauda, Salum Chama, Athumani Kambi, Saleh Alawi, Kalilo Samson, Vedatus Lefano, Kenneth Pesambili, Mbasha Matutu, Samuel Daniel, Dastan Mkundi, Gorlden Sanga, Elias Mwanjala na Efram Mwajinge.

Zoezi hilo la uchukuaji fomu lililoanza jana litaendelea hadi Juni 20, mwaka huu ambapo baada ya hapo kutakuwa na mchujo wa awali kwa wagombea utakaofanyika Juni 21 hadi 23.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu ambapo utafanyika kwa mara ya kwanza mkoani Dodoma.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU