KAMA TRA HAWAKUSHTUKA KWA NEYMAR NA MESSI, BASI WAAMKE KWA RONALDO

KAMA TRA HAWAKUSHTUKA KWA NEYMAR NA MESSI, BASI WAAMKE KWA RONALDO

676
0
KUSHIRIKI

NA JONATHAN TITO

MAMLAKA ya Mapato nchini Hispania imeendelea kuwabana wachezaji wote wanaokipiga La Liga, ambao wanakwepa kodi na kuwalipisha kile wanachodaiwa na sasa nyota ambaye yuko kwenye kesi ya ukwepaji kodi ni mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Ronaldo ambaye anadaiwa kukwepa kodi kati ya mwaka 2011 na 2014, anadaiwa kiasi cha pauni milioni 12.9 (shilingi bilioni 36). Lakini Ronaldo si mchezaji wa kwanza anayecheza Hispania kukumbwa na kashfa hizo za kukwepa kulipa kodi. Mpinzani wake Ronaldo, Lionel Messi, naye aliingia kwenye kesi ya kukwepa kodi ya kiasi cha euro milioni 4.16 (shilingi bilioni 10) na kufungwa kifungo cha nje cha miezi 21 na kupigwa faini ya dola milioni 2.2 (shilingi milioni 4.8).

Baba wa nyota huyo wa Barcelona, Messi, Jorge Messi, alipigwa faini ya euro milioni 1.5 (shilingi bilioni 3.2), kutokana na kuhusika kwenye ukwepaji huo kodi wa mwanawe uliofanyika kati ya mwaka 2007 hadi 2009.

Wachezaji wengine waliokumbwa na mkasa huo wa kukwepa kulipa kodi ni kama mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Davor Suker, alitakiwa kulipa euro 258,592 kwa kosa hilo alilofanya mwaka 1998.

Wachezaji wengine wa Barcelona waliopigwa faini kwa kukwepa kulipa kodi ni Romario, ambaye alilipa euro 800,000, huku Javier Mascherano akilipa euro 815,000, Luis Figo akiwa kwenye klabu hiyo ya Catalan. Mahakama Kuu nchini Hispania ilipiga faini ya euro milioni 2.4 kwa kukweka kulipa kodi mwaka 1997 hadi 1999.

Samuel Eto’o alikuwa mchezaji mwingine wa Barcelona pamoja na Neymar kupigwa faini kwa kosa hilo, ambapo Eto’o alikwepa kulipa kodi kutoka kwenye mkataba wake wa Puma kati ya mwaka 2006 hadi 2009.

Neymar alikwepa kodi ya uhamisho wakati anasajiliwa Barca akitokea Santos na kutakiwa kulipa euro milioni 45.

Lakini shughuli hiyo ya Mamlaka ya Mapato nchini Hispania, haikuanzia utaratibu huo wa kuchunguza wachezaji pekee, bali walianzia kwenye klabu na kugundua jinsi wanavyopoteza kiasi kikubwa cha kodi kwenye soka na tangu walipotambua hilo wamelifanyia kazi bila kuchelewa.

Baada ya kugundua hilo, mpango wao wa kwanza ulianzia kwenye klabu hizo za Hispania na kwa muda mfupi walifanikiwa kupata kodi yao wakishirikiana na Rais wa Barala za Soka la Hispania, Miguel Cardenal na kiongozi wa La Liga, Javier Tebas.

Ndani ya miaka michache, kiasi cha euro milioni 560 (shilingi bilioni 1.3) kati ya deni la kodi la euro milioni 750 (shilingi bilioni 1.8) kilikusanywa.

Kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimebaki kiliwekewa mipango ya kulipwa kwa awamu kwa zile klabu ambazo zilikuwa zikidaiwa kodi hiyo, huku wakiwekewa hadi mwaka 2020 wawe wamekwishalipa kiasi hicho.

Lakini bado wamekuwa na kazi nzito katika kuangalia njia nyingine linapokuja suala hilo la kukwepa kodi. Karne iliyopita kabla ya soka kuwa la kulipwa wachezaji walikuwa wakilipwa kwa mtindo wa mahitaji yao, tofauti na sasa hulipwa kulingana na makubaliano ya fedha wanazotaka.

Baada ya mamlaka hiyo ya mapato kushughulika na klabu, janga jipya ambalo wanapambana nalo sasa ni ukwepaji wa kodi kwa haki za matangazo na mikataba mingine kwa wachezaji.

Kwa mujibu wa sheria zao za mapato, wachezaji wanapaswa kulipa asilimia 15 kwa kipato wanachoingiza kwenye mikataba yao ya matangazo (image rights), lakini wachezaji hao wamekuwa wakikwepa na wao kuamua kulivalia njuga.

Je, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajifunza nini kutokana na kile kinachotokea nchini Hispania, hasa kwenye nchi hii ambayo wachezaji wanaficha mishahara yao huku wwengine wakionekana kwenye matangazo kadhaa.

Je, wachezaji hao wanalipa kodi za wachezaji wao na klabu nazo zinalipa kodi kwa kile wanachokiingiza kwenye mikataba yao kama ilivyokuwa kwa Simba, Yanga na Singida United ambao juzi walidhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.

Ukiachana na timu hizo, kuna mkataba wa Azam na benki ya NMB na makampuni mengine yaliyodhamini klabu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwasasa ukiuliza kiasi walichokiiingiza kwa mikataba ya usajili wa wachezaji lazima utaambiwa kwamba huko ni kutoa siri za mteja, lakini wenzetu walioendelea na matajiri wanataja kile wanachokipata kwa wachezaji na wanataja kile wanachowadai ila sisi maskini wenye shida ya fedha tunasema ni siri.

Nakumbuka mlinda mlango wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, aliwahi kuwamo kwenye tangazo la kinywaji cha pepsi na kampuni ya simu ya Zantel wakati huo akiwa Simba, Jonas Mkude na Shomari Kapombe walikuwa kwenye matangazo ya magodoro, je, walilipa kodi kutokana na kiasi cha fedha walichoingiza kwenye matangazo hayo? Hakuna anayejua hilo.

Lakini TRA hawajachelewa, kama walishindwa kuwakamata wachezaji wanaokwepa kodi wanaweza wakaanzisha uchunguzi kama wanavyofanya Hispania au wakaamua kuachana nao na kuanza upya.

Kesi ya Rais wa Simba, Evans Aveva ya kudaiwa kutumia akaunti binafsi kupitishia fedha za usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wao Emanuel Okwi ili kukwepa kulipa kodi, bado pia basi la Taifa Stars liliwahi kukamatwa, huo unaweza ukawa mwanzo mzuri.

Ila sasa ndio wakati wa TRA kujifunza kama walishindwa kushtuka baada ya kesi ile ya Neymar na Messi, basi huu ndio wakati wanaopaswa kuamka na kuanza kuwapiga faini wanaokwepa kodi, kuliko kuendelea kusubiri hadi yatokee yale ya mchanga wa dhahabu ‘makinikia’.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU