DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

709
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

“NI kweli mume wangu itakuwa hivyo, lakini kilio changu ni kwamba, unaondoka kipindi ambacho nakuhitaji kuliko kipindi kingine chochote. Hata sijalala kwenye kifua chako mara nyingi, hata hujaugusa mwili wangu vile upendavyo,” alijibu Julia, akiendelea kulia sana.

Usiku huo ulikuwa mbaya kwa wanandoa hao, amani ilitoweka kabisa, kila mmoja hakupenda kuachana na mwenzake, kwani walikuwa wanaachana kipindi ambacho utamu wa maisha yao ya ndoa ndio ulikuwa unaanza.

SASA ENDELEA

Kai alimpenda Julia kupita kiasi, Julia naye aliona maisha bila Kai hayawezekani.

“Mume wangu usiniache, ukiniacha nitakufa,” aliongea Julia akiwa bado amejilaza kwenye kifua kizuri cha Kai.

“Julia mke wangu, hivi ni shetani gani aliyekudanganya kuwa mimi ninaweza kukuacha? Nilimuomba Mungu usiku na mchana, nilishawahi kufunga kula, nikakesha mlimani nikimsihi Mungu anipe wewe uwe mke wangu. Nilimuahidi nitakulinda dhidi ya hatari yoyote ile. Hivyo nikivunja ahadi hizo, nimevunja agano takatifu. Nakupenda sana Julia usiogope mke wangu.”

“Maneno yako yamenipa uhai mwingine. Nitakusubiri wakati wowote na kwa vyovyote vile lazima nije kukutembelea London.”

“Nitafurahi na kuchanganyikiwa siku utakayokanyaga London,” aliongea Kai kwa tabasamu.

“ Nitakuja mume wangu mwaaaa,” alijibu Julia na kumbusu mumewe.

“Hivi mume wangu unataka tuzae watoto wangapi?” aliuliza Julia.

Kai alicheka na kumshika mkewe shavu. Akamtazama kwa sekunde chache kama ameambiwa achague zawadi ya thamani.

“Nataka tuzae watoto watatu tu,” alijibu Kai kwa tabasamu.

“Mmh! Mume wangu watatu wanatutosha?” aliuliza Julia.

“Wanatutosha kabisa we ulitaka wangapi?”

“Watano au sita.”

“Haaaa watano? Hata haiwezekani sitaki mke wangu uchakae watoto watatu tu wanatutosha.”

“Nakutania mume wangu hata mimi napenda watatu tu au wawili kabisa.”

“Vizuri ila napenda sana mapacha,” Kai aliongea.

“Ha haa haaa! Unapenda mapacha?”

“Ndio nawapenda sana.”

“Unapenda mapacha wa kike wa kiume?”

“Wote nawapenda.”

“Utajisikiaje siku nikikwambia nina mapacha wako tumboni.”

“Nadhani furaha yangu itapasuka, nitakupa zawadi kubwa zaidi ya ile utakayoniambia wewe ni mjamzito wa mtoto mmoja.”

“Basi usijali mume wangu, mapacha wanakuja.”

“Japo najua ni juhudi fulani naweza kuitumia ili unizalie mapacha, lakini ni vema na wewe ukaikubali,” aliongea Kai.

“Kwa nini tusiitumie, wakati sayansi inatuweka wazi?”

“Basi tutaifanyia kazi  ukija London.”

“Sawa mume wangu mzuri,” alijibu Julia huku akijilaza vizuri kwenye kifua cha mumewe Kai.

Usiku huo ulikuwa ni usiku wa mwisho kwa Kai na Julia kulala kwenye kitanda kimoja. Walizungumza mambo mengi kuhusu maisha yao ya ndoa. Ingawa mwanzo wa mazungumzo yao ulikuwa umetawaliwa na majonzi, lakini walijifariji kwa kuzungumzia familia yao ijayo, ambayo ni watoto watakao wazaa. Majonzi yalipungua kutokana na Kai kumfariji vizuri mkewe.

Walijifariji zaidi kwa kuingia kwenye mapigano ya mahaba. Usiku huo walifanya kazi kubwa kwa nusu nzima ya usiku mmoja. Kai alifanya juhudi kubwa iliyomfikisha mkewe sehemu ambayo hakuwahi kufika. Baada ya kazi hiyo ya ndoa, usingizi mzito uliwachukua. Julia alikilalia kifua cha mumewe kama gogo la ukombozi ndani ya bahari.

Asubuhi Kai alikuwa akijiandaa kwa safari yake ya London. Julia alimwandalia mumewe kifungua kinywa kizuri kilichomuingiza kwenye majaribu ya kuichukia safari yake ya London. Alipenda kubaki nyumbani na mkewe. Huzuni iliendelea kuwatawala wanandoa hawa. Hawakupenda kabisa kuachana.

Baada ya saa moja, Julia alimsindikiza mumewe uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere. Wakiwa njiani, kule kuchekeshana kulipungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu kila mmoja alichukia kitendo cha wao kutengena. Japo walikuwa wakitengana kwa muda kutona na masomo, lakini majonzi makali bado yalizidi kuwaonea.

Muda mfupi tu walikuwa wamekwisha fika uwanja wa ndege. Walikumbatiana kwa muda mrefu pasipo kuachanisha miili yao, hata abiria wengine waliwashangaa. Kai alimfuta Julia machozi, alimuaga kwa busu kali lililomfariji mke wake vilivyo.

“Baki salama mke wangu na wewe nakutakia safari njema ya Afrika Kusini. Mengine mengi tutaongea kwenye simu,” aliongea Kai akiwa amemshika mkewe kwenye mashavu yake mawili.

“Nawe safiri salama mume wangu Mungu akulinde. Ukifika tu, jambo la kwanza naomba unipigie simu sawa?” alijibu Julia kwa tabasamu hafifu.

“Sawa usijali.”

“Kwa kheri Julia, ukipata muda naomba uje London tafadhali sana.”

“Sawa Kai mume wangu.”

Waliagana kwa shingo upande. Kai aliuachia mkono wa mkewe pasipo kupenda na Julia aliuacha mkono wa mumewe akiwa ameunyosha vile vile. Kai aligeuka mara kwa mara kumtazama mkewe Julia pindi alipokuwa akizipiga hatua kwenda kwenye eneo la ukaguzi wa abiria. Uzuri wa mkewe ulimpa majonzi zaidi.  Alimtazama kwa mara ya mwisho, pindi alipokuwa akizamia kwenda kwenye chumba cha abiria. Alimuona Julia akitokwa machozi huku akitabasamu.

Julia alirudi kwenye maegesho ya magari. Aliingia kwenye gari lake, akaulalia usukani na kulia sana. Alimlilia mumewe kama vile Kai alikuwa amepatwa na umauti. Aliimuomba Mungu mara nyingi kuwa amlinde mumewe usiku na machana. Alibaki pale akiisubiria kuiona ndege ya Qatar Airways, ambayo ndio aliyokuwa ameipanda mumewe, ikiiacha ardhi  ya Tanzania na kuruka angani.

Baada ya ndege kuruka na kupotelea mbali, Julia alinyonga ufunguo, akaliwasha gari lake na kuondoka uwanja wa ndege, huku akibubujikwa na machozi mengi.

Kai naye akiwa ndani ya ndege, machozi hayakukauka mara moja usoni mwake. Japo alijifuta kwa kitambaa mara kwa mara, lakini uzuri na mapenzi ya kweli kwa mkewe, yalizidi kumliza vilivyo. Moyo wake ulitambua vema upweke na huzuni kubwa atakayo kwenda kukutana nao.

Ndani ya ndege Kai alishindwa kula chochote. Maana picha ya mke wake kipenzi haikuondoka mbele yake. Alianza kuhisi kuwa nguvu yake ya kisayansi inaweza kupungua kwa mara nyingine, kutokana na upweke anaokumbana nao kipindi hicho. Alijipa nguvu, akamshukuru Mungu na kumuomba ampe moyo wa uvumilivu katika kipindi hicho kigumu.

Siku ya jumanne ndege ya Qatar airways ilitua kwenye uwanja wa malikia Elizabeth. Kai alishuka na kuelekea moja kwa moja kwenye nyumba yake iliyokuwa mtaa wa Kingstone jijini London. Alipofika tu, jambo la kwanza alimpigia simu Julia. Simu ilipokelewa haraka.

“Mume wanguuu,” aliongea Julia kwa sauti nzuri iliyomfanya Kai atabasamu.

“Ndio mke wangu. Nimefika salama.”

“Waao Mungu ni mwema sasa nina amani, vipi baridi ni kali kiasi gani?”

“Hakuna baridi sana  kwani hiki ni kipindi cha majira ya joto.”

“Mume wangu naomba uwe na amani. Soma kwa bidii. Naomba usiniwaze sana kiasi cha kushindwa kusoma. Amini mimi nipo na ni wa kwako peke yako sawa mpenzi?”

“Sawa mke wangu. Sauti yako imenipa nguvu. Naomba na wewe usome kwa bidii wewe ni daktari wa nchi usilisahu hilo, watoto wa Muhimbili wanakusubiria” alijibu Kai na kumfanya mkewe acheke.

“Haa haa haa sawa mume wangu.”

Baada ya maongezi hayo na mengine mengi, walikata simu zao. Kai alijipumzisha kitandani, akiwa na amani kutoka moyoni, maana alikuwa ameisikia sauti ya Julia.

Muda mfupi baadaye, aliamka na kwenda sebuleni. Alikaa kwa uchovu na kuwasha runinga. Taarifa ya habari ya kituo cha Sky, ilikuwa ikitangazwa muda huo. Taarifa hiyo iliripoti kutoka Afrika, ikisema kuwa ugonjwa wa Ebola ulikuwa unazidi kusambaa kwa kasi. Tayari ulikwisha kutoka nje ya nchi za Ghana na Ethiopia, nchi ambazo ndiko ulikoanzia. Mtangazaji wa kituo hicho alisema kuwa, tayari ugonjwa wa Ebola ulikuwa umekwishaingia katika nchi ya Kenya na Uganda huku nchi nyingine nyingi za Kiafrika zikiwa tayari zimekwishapatwa na ugonjwa huo hatari.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa kwenye mazungumzo makuu yaliyokuwa yakifanyika nchini Canada, likijadili kuhusu njia na mipango mbalimbali ya kuweza kukabiliana na ugonjwa huo. Tayari zaidi ya madaktari 60 na wauguzi 100 walikuwa wamesambaa nchi mbalimbali za Afrika.

Nini kitafuatia? Usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU