MJESHI AMALIZANA NA AZAM

MJESHI AMALIZANA NA AZAM

2262
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

KLABU ya Azam imefanikiwa kumalizana na beki wa Tanzania Prisons, Salum Kimenya, baada ya kumpa mkataba wa miaka miwili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kimenya ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza, ameamua kuachana na ajira hiyo na kwenda kujiunga na Azam ambayo msimu uliopita imeshindwa kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu ya Azam zinasema kuwa wamelazimika kuitafuta saini ya mchezaji huyo ili kuziba pengo la beki wao Shomari Kapombe aliyetua Simba kwa msimu ujao.

Mtoa habari huyo amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni kutambulishwa baada ya wao kufuata taratibu zote za usajali ili aweze kukitumikia kikosi chao.

“Kimenya ni mwajiriwa wa Serikali  katika  Idara ya Jeshi la Magereza, sisi  Azam tumemalizana na Kimenya na msimu ujao atavaa jezi za timu yetu,” alisema mtoa habari  wetu.

BINGWA lilimtafuta mchezaji huyo ili kujua ukweli wa suala hilo, alisema kwa sasa ni mchezaji halali wa Prisons na timu yoyote inayomhitaji ni lazima iwasiliane na mwajiri wake.

“Mimi ni mchezaji sehemu yoyote nacheza, lakini kwa sasa nipo chini ya Prisons hivyo siwezi kuzungumza lolote kwani anayenihitaji lazima awasiliane na waajiri wangu,” alisema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU