TAMBWE KUREJEA YANGA NA NDIKUMANA

TAMBWE KUREJEA YANGA NA NDIKUMANA

4246
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, baada ya kuona ugumu wa kupata kiungo mkabaji wa Mbao FC, Yussouf Ndikumana, wameamua kutafuta njia nyingine ambayo ni kumtumia mshambuliaji wao, Amis Tambwe.

Saini ya Ndikumana inasakwa na klabu mbalimbali ikiwamo Simba, Yanga na Kagera Sugar, baada ya kung’ara msimu uliopita na kuinusuru timu yake ya Mbao FC isishuke daraja na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

Licha ya mazungumzo ya awali kuwapa moyo vigogo wa Yanga, lakini ugumu ulizuka baada ya meneja wa kiungo huyo kutokukubali mazungumzo na timu hiyo yenye maskani yake Jangwani.

Habari za ndani kutoka Burundi ambazo pia zilithibitishwa na Ndikumana mwenyewe, zilisema kuwa Tambwe amekuwa akimshawishi kiungo huyo kutua Jangwani kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo.

“Tulimtafuta Ndikumana kwa ajili ya mazungumzo ya kucheza Simba msimu ujao, ila kilichoshindikana ni meneja wake kuweka ngumu hivyo tumeona bora tumtumie Tambwe ambaye yupo karibu naye zaidi,” kilisema chanzo hicho.

Ndikumana alikiri kusumbuliwa na Tambwe na kusema kwamba jibu ambalo anampa kila siku ni kuzungumza na uongozi wake kwa kuwa yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo.

“Tambwe kila siku ananitafuta kwa simu na nimemwambia azungumze na viongozi ambao wao ndio wanaweza kuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu sehemu ambayo nitakwenda msimu ujao,” alisema.

Yanga wameamua kumtafuta Ndikumana ili kuweka sawa kikosi chao hasa katika safu ya kiungo mkabaji ambao imekuwa ikiwasumbua katika miaka ya hivi karibuni tangu aondoke Frank Domayo na Athuman Idd ‘Chuji’.

Pamoja na mchezaji huyo wa Mbao, pia Yanga wametega mtego wao kwa kiungo mkabaji wa Vital O, Pistis Barenge.

Tayari Yanga wanadaiwa kufanya naye mazungumzo na kama watamkosa Ndikumana, basi wataamua kumalizana na kiungo huyu wa Burundi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU