UKIMFANYA MWENZAKO AJIHISI HIVI, UNAMFANYA AKUUMIZE BAADAYE

UKIMFANYA MWENZAKO AJIHISI HIVI, UNAMFANYA AKUUMIZE BAADAYE

737
0
KUSHIRIKI

UNA amani katika mahusiano yako? Unajivunia kuwa na mwandani wako? Bila shaka kama una amani, ina maana huna wasiwasi na matendo ya mwenzako juu yako.

Mwenzako ana amani kuwa na wewe kama wewe ulivyo kwake? Unamfanya ajione wa thamani kwa namna unavyompa tumaini na amani ya nafsi?

Katika hali yoyote ile, usimfanye mpenzi wako akawa na wasiwasi ikiwa yeye anakupa amani na furaha. Wasiwasi ni zao la kutojiamini katika mahusiano.

Unajua nini wanafanya wengi wakiwa na wasiwasi katika mahusiano ya kimapenzi? Twende pamoja ujue ukweli uliojificha juu ya wasiwasi wa wengi.

Wasiwasi mbali na kuwa na athari za kibaolojia kama vidonda vya tumbo na maradhi mengine ila pia ni chimbuko kubwa la wahusika kukosa amani.

Mtu mwenye wasiwasi juu ya mwenzake, huwa hana raha katika mahusiano. Akiona mwenzake anashika simu na kuchati, uhisi anasalitiwa. Mwenzake akiwa na safari, anajua katika safari hiyo kuna jambo lingine litatendeka. Katika hali hiyo atakuwa vipi na amani na furaha? Haiwezekani.

Watu wengi walio katika uhusiano wenye kuwapa wasiwasi, hata kama wanaishi katika majumba ya kifahari, wanaendesha magari ya thamani na hadhi ila hujiona hawana kitu.

Huona kama dunia ina wadhihaki kwa kila wanachofanya na kutamani. Katika uhusiano wako mwenzako ana amani na wewe? Mwenzako ana amini kuwa wewe ni mtu muafaka kwako na humuendei kinyume?

Kama mwenzako ana wasi wasi na wewe, fanya hima umfanye awe na amani na furaha. Mfanye atokwe na wasiwasi wake na aanze kukuona wewe ni kiumbe wa thamani na baraka. Bila kufanya hivyo, kuna hatari ya wewe kusalitiwa.

Nani anaweza kuhisi kisha kuamini mwenzake ana msaliti na yeye akatulia na kuona kawaida? Hakuna. Wengi wakihisi hali hiyo huchanganyikiwa, hujiona hawana thamani na umuhimu.

Baadhi hutumia busara kutafuta suluhu na wenzao ama kuomba msaada wa kitaalamu kupata ufahamu zaidi ama mbinu za kuwazuia wenzao waache tabia hiyo. Wengi hutafuta furaha bandia kwa kulipa kisasi.

Huamini kwa kusaliti basi na wao watapata tulizo na kusahau madhila ya wenzao. Kwao kusaliti ni njia muafaka ya kulinda utu wao na kuonesha namna wasivyo wanyonge. Umejipanga namna gani mwenzako asikusaliti?

Mbali na wema na kila zuri unalotakiwa kufanya. Mbali na thamani na hadhi unayotakiwa kuonesha anayo kwako, hakikisha mwenzako hana fikra za kuamini una msaliti katika kichwa chake. Bila kufanya hivyo unatengeneza bomu ambalo litakuja kulipua mahusiano yako na isiwezekane tena kurudi kama ilivyo kuwa mwanzo.

Katika mahusiano kitu kizuri zaidi ni kutengeneza fikra za mwenzako ziamini katika wema na ubora wako. Anatakiwa kuamini kuwa wewe ni bora sana, ni muhimu sana kwake, na una mjali sana kiasi cha kushindwa kumsaliti. Mwenzako ana amini hilo?

Wakati mwingine matendo mengi mazuri ama maneno mengi yasiomfanya mwenzako akuamini hayana maana sana. kuanzia sasa, jipange umfanye mwenzako akuamini, akuone katika namna zote bora katika akili yake.

Mwenzako akiamini wewe ni bora na una mjali kwa kiwango stahili, hawezi kuhisi una msaliti. Kama anaamini huwezi kumsaliti, hawezi kuwa na wasiwasi na wewe. Katika namna  hii, ndipo mahusiano ya amani furaha na raha yanapojengeka.

Mahusiano mengi yanazidi kuingia kizani kwa sababu ya fikra hasi za baadhi ya waliopo katika uhusiano. Kama mtu anakutazama katika jicho la uasi na kusaliti, hata siku moja hawezi kujivunia kuwa na wewe. Mtu akiacha kujivunia kuwa na wewe, abadani asilani hawezi kuhisi dhambi kubwa kukusaliti.

Mwenzako akiona thamani unayompa na heshima unayomtunzia, hawezi kukurupuka kukusaliti ikiwa anakupenda kwa dhati. Matendo maovu mengi ya binadamu, husukumwa na fikra hasi katika nafsi zao.

Uovu mwingi, hata uitwao ugaidi katika mataifa mengi hufanywa na wahusika wakisukumwa na fikra na hisia hasi juu ya watu fulani. Ili mwenzako awe na fikra safi juu yako ni lazima umfanye akuone wa thamani na bora sana kwako.

Ni lazima umfanye akuone wewe ndiyo sababu ya furaha yake, amani yake, utu wake na thamani yake. Je, unamfanya mwenzako aamini hivyo na ajione hivyo?

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU