VIGOGO KICHEKO MECHI ZA UFUNGUZI EPL 2017-18

VIGOGO KICHEKO MECHI ZA UFUNGUZI EPL 2017-18

743
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

KUWEKWA wazi kwa ratiba kumeanza kuamsha mizuka ya Ligi Kuu England (EPL) na ni wazi uhondo wake hauko mbali. Ligi hiyo inayotajwa kuwa na mashabiki wengi duniani itaanza rasmi Agosti 12.

Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa kwa hamu ni kuona endapo Chelsea ya Antonio Conte itaweza kulitetea taji lake la msimu uliopita.

Pia, presha kubwa itakuwa kwa Pep Guardiola ambaye alikishuhudia kikosi chake cha Manchester City kikiondoka mikono mitupu.

Kwa Guardiola, ilikuwa ni ajabu kwani ni kwa mara ya kwanza kukutwa na majanga hayo tangu alipoanza kufundisha soka.

Mbali na hilo, habari nyingine itakuwa kwa kocha Arsene Wenger ambaye mashabiki wake wanasubiri kuona atakachokifanya kwa msimu ujao baada ya kusaini mkataba mpya wa  miaka miwili.

Bila shaka Mfaransa huyo atataka kuwathibitishia wakosoaji wake kuwa alistahili kuendelea kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu licha ya kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 20.

Utamu mwingine utakuwa kwa kocha Jose Mourinho ambaye ana rekodi ya kipekee katika kila msimu wake wa pili katika ligi zote alizofundisha.

Kwa mujibu wa rekodi za mkufunzi huyo wa kimataifa wa Ureno, hajawahi kukosa taji la Ligi Kuu katika msimu wake wa pili akiwa na Porto, Chelsea, Inter Milan na Real Madrid.

Hata hivyo, baada ya kutoka kwa ratiba ya msimu ujao, ni wazi timu vigogo zitakuwa zinaifurahia kutokana na rekodi zake katika mechi za ufunguzi.

Arsenal v Leicester

Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa Leicester City hawajashinda katika mechi 21 walizokutana na wakali hao wa Emirates katika michezo ya Ligi Kuu England iliyochezwa katika miaka ya hivi karibuni. Leicester wamefungwa mara 14 na kuambulia sare saba.

Lakini pia, Arsenal wameshinda mechi zote 10 ambazo wamekuwa nyumbani dhidi ya Leicester. Katika mechi za ufunguzi wa ligi, Arsenal wamefungwa na Liverpool na West Ham tu tangu mwaka 1960.

Brighton v Manchester City

Agosti 12 itakuwa ni siku nzuri pia kwa mashabiki wa Man City na Pep Guardiola. Katika mechi sita zilizopita za ufunguzi wa ligi, Man City wameshinda zote. Katika idadi hiyo, Sergio Aguero amefunga jumla ya mabao matano.

Brighton ambao ni wageni wa Ligi Kuu England msimu ujao, wana rekodi ya kushinda mechi moja pekee kati ya tano za ufunguzi.

Chelsea v Burnley

Chelsea ndio timu pekee ambayo imezoa pointi nyingi katika mechi za ufunguzi (54).

Chelsea wamepoteza mechi moja pekee kati ya 25 za ufunguzi wa Ligi Kuu England huku wapinzani wao Burnley wakiwa wamepoteza mechi zote tatu za hatua hiyo na kufunga bao moja pekee.

Man United v West Ham

Jose Mourinho ameshinda mechi saba kati ya nane za ufunguzi wa ligi.

West Ham ndio timu inayoongoza kwa kupoteza mechi nyingi za ufunguzi katika historia ya Ligi Kuu England.

Man United haijafungwa katika mechi tisa ilizocheza dhidi ya West Ham pale Old Trafford.

Mechi ya mwisho kwa Man United kufungwa na West Ham nyumbani ilikuwa ni ile ya mwaka 2007.

Watford v Liverpool

Liver wameshinda mechi zao nne zilizopita za ufunguzi wa Ligi Kuu England. Liver wameifunga Watford katika mechi tatu zilizopita na kupata mabao 19.

Watford hawajawahi kushinda mechi za ufunguzi wa ligi kwani imepoteza mara mbili na kutoa sare mbili.

Newcastle v Totteham

Kwa mujibu wa rekodi, tofauti na vigogo wengine wanaobebwa na rekodi zao za mechi za ufunguzi, Tottenham watakuwa kwenye wakati mgumu.

Kocha wa sasa wa Newcastle, Rafael Benitez, hajafungwa katika mechi zake nane zilizopita za nyumbani dhidi ya Tottenham.

Huku ikimtegemea Hary Kane, Totteham haijawahi kufungiwa bao na mshambuliaji huyo katika mechi za Agosti.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU