WAJUMBE TFF WATUCHAGULIE VIONGOZI BORA

WAJUMBE TFF WATUCHAGULIE VIONGOZI BORA

459
0
KUSHIRIKI

AGOSTI 12, mwaka huu, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatarajia kufanya uamuzi mgumu wa kuwachagua viongozi wapya.

Uchaguzi wa shirikisho hilo umepangwa kufanyika mkoani Dodoma, baada ya viongozi waliopo kumaliza muda wa miaka minne ya kuliongoza soka.

Tayari fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho hilo zilianza kutolewa tangu Ijumaa wiki iliyopita, ambapo kesho itakuwa ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha.

Katika mchakato wa kuchukua fomu za kuwania uongozi wa  shirikisho hilo, tayari rais  anayemaliza muda wake, Jamal Malinzi, amejitokeza kutetea nafasi yake huku  bado akikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Lakini uchaguzi wa mwaka huu unaonekana ni tofauti na ule uliofanyika mwaka 2013, kutokana na watu wengi kujitokeza kuwania nafasi ya urais, makamu wa urais na wajumbe wa kamati ya utendaji.

Tunaona kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na changamoto kubwa kutokana na idara ya watu waliojitokeza katika nafasi  hizo na wajumbe wa mkutano watakuwa na kazi kuhakikisha wanachagua viongozi bora ambao watalisukuma soka mbele.

Tunaamini kwamba Watanzania walio wengi wana hamu ya kuona soka letu linasonga mbele tofauti na ilivyo sasa, hivyo kujitokeza kwao wengi ni baada ya kuona changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha miaka minne ya uongozi unaomaliza muda wake.

 

Tunajua kwamba TFF  ni chombo cha juu cha soka hapa nchini kinachosimamia sheria na kanuni mbalimbali zinazoendesha mpira, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa  wadau wengi  kuonekana na  kupindishwa utaratibu mzima na mwongozo wake.

Tumeshuhudia malalamiko mengi katika uongozi unaomaliza muda wake, huku baadhi ya wadau wa soka wakionekana kukosa imani na kile kinachoendelea kwenye shirikisho hilo.

Katika uchaguzi huu, tunataka kuona wajumbe wakiwachekecha watu waliojitokeza kuchukua fomu na kuchagua viongozi ambao watawaona wanafaa kuongoza soka.

Sisi BINGWA macho yetu yapo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo, kwa kuwa wao ndio  wenye kura ya kutuchagulia viongozi watakaoweka masilahi ya mpira mbele.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU