WENYE UCHUNGU NA SOKA LETU NI WAKATI WENU SASA

WENYE UCHUNGU NA SOKA LETU NI WAKATI WENU SASA

438
0
KUSHIRIKI

NA WINFRIDA MTOI

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unatarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu,  mjini Dodoma,  baada ya uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Jamal Malinzi kumaliza muda wake wa  miaka minne.

Tayari fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho hilo zilianza kutolewa tangu Ijumaa wiki iliyopita, ambapo kesho itakuwa ni siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha.

Nafasi kuu tatu zinazogombaniwa kwenye  uchaguzi huo ni rais, makamu wa rais na wajumbe wa kamati ya TFF na wagombea waliochukua fomu ya kuwania urais ni pamoja na Malinzi na aliyekuwa makamu wake Wallace Karia.

Wengine ni makamu wa rais wa zamani wa shirikisho hilo, Ramadhani Nyamlani,  Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, Iman Madega na wengineo.

Idadi ya wagombea ilizidi kuongezeka jana katika nafasi mbalimbali zilizotajwa kwenye uchaguzi huo.

Kutokana na watu kuvutika kwa wingi kuchukua fomu, inaashiria kwamba, Watanzania waliowengi wana hamu ya kuona soka letu linasonga mbele tofauti na ilivyo sasa, hivyo kujitokeza kwao ni kutaka kuongeza mawazo mapya katika shirikisho hilo linaloongoza soka hapa nchini.

Tunajua kwamba TFF ndiyo sehemu kuu ya kutoa mwongozo na kutunga kanuni mbalimbali za kuendesha soka hapa nchini ambazo kwa muda mrefu zimekuwa  zikilalamikiwa na wadau wengi kwa kuonekana kupindishwa.

Tumeshuhudia malalamiko mengi katika uongozi unaomaliza muda wake huku baadhi ya wadau wa soka kukosa imani na kile kinachoendelea kwenye shirikisho hilo, licha ya kwamba yapo yaliyofanikiwa kwa upande fulani chini ya uongozi huo.

Miongoni mwa vitu vilivyokuwa vinalalamikiwa zaidi ni uendeshwaji wa ligi mbalimbali, ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara na kuboronga kwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambapo kwa miaka mingi haijawapa furaha Watanzania.

Kitendo hicho kimewafanya wadau na wachambuzi wa soka kutoa lawama kwa uongozi uliopo madarakani kwa kushindwa  kuweka mikakati imara ya  kulifanya soka la Tanzania kupiga hatua.

Ninaamini Tanzania ni moja ya nchi iliyobarikiwa vipaji vingi vya soka, kinachokosekana ni mwongozo na mikakati thabiti katika kufanikisha maendeleo ya mchezo huo ambapo kwa sasa maneno yamekuwa mengi kuliko utekelezaji.

Ili kuondoa hali hii tunahitaji viongozi makini na wale wenye uchungu wa kweli kwa soka la Tanzania na watapatikana endapo kila mmoja atajiamini na kujitokeza kuchukua fomu ya nafasi anayoona inaweza kumfaa.

Wapo watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza mipango  na mikakati na soka letu likapiga  hatua zaidi tofauti na hapa tulipofikia, ila tatizo  linakuja pale wanaposhindwa kujitokeza kwa kipindi hiki na kusubiri mambo yaharibike na kuanza kupiga kelele pembeni.

Inafahamika kuwa wapo Watanzania wengi wanaotumika  kuandika mipango na mikakati ya soka katika nchi nyingine  na inafanikiwa, lakini kwa hapa nchini  wanashindwa kufanya hivyo kutokana na kutopewa  kipaumbele cha kutoa mawazo yao au kutotambulika kama wana uwezo wa kufanya mambo hayo.

Hakuna  jambo lolote linaloweza kufanikiwa bila uwepo wa wataalamu wa kitu husika, hivyo basi wale wataalamu wetu wa soka wanaotumika  sehemu nyingine au kutoa maoni yenu pembeni jinsi  gani mchezo huo unatakiwa kuendeshwa, ni wakati wenu kujitokeza kuwania uongozi ndani ya shirikisho hilo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU