FEBREGAS ZAO LA WERRASON LILILOMGEUKA

FEBREGAS ZAO LA WERRASON LILILOMGEUKA

1025
0
KUSHIRIKI

NA NOAH YONGOLO

FABRICE Mbuyulu ‘Fabregas’ au ukipenda muite ‘Le Metis Noir’ ni mwendelezo wa vipaji vingi vya wanamuziki vijana waliopikwa na Rais wa Wenge Musica, Noel Ngiama Makanda Werrason ‘Le Roi De La Foret’.

Leo Kona ya Bolingo (KB) inaangazia katikati ya jiji la Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hapa tunakutana na Fabregas, kaa mkao wa kula kwaajili ya kupata simulizi ya kuvutia kuhusiana na historia yake ya muziki, alikoanzia na alipo sasa.

Fabregas alizaliwa Agosti 1987, eneo la Matete, jijini Kinshasa. Ni baba wa familia ambaye alifunga ndoa na mkewe mwaka 2012.

Ndoto za kuwa mwanamuziki zilikolezwa na wazazi wake, waliokuwa na rundo la ‘kaseti’ za wanamuziki tofauti wa DRC, hasa Koffi Olomide.

Akiwa bado mdogo aliendelea kusikiliza nyimbo mbalimbali za wanamuziki wa nchi hiyo na baadhi akijaribu kuziimba.

Mwanamuziki mwingine aliyekuwa akivutiwa naye alikuwa Reddy Amisi. Wakati fulani aliwahi kupigwa na wazazi wake baada ya kwenda kwenye onyesho la muziki moja kwa moja akitokea shule badala ya kurudi kwanza nyumbani.

Kama ilivyo kwa vijana wengi wa rika lake miaka ya 90, alikuwa ni mmoja wa waliolipenda kundi la muziki wa vijana la Wenge Musica BCBG 4×4 na kutamani siku moja kujiunga nao.

Kabla ya ndoto zake kutimia, alianza kujifunza muziki kwa kuimba kwaya kanisani na kwenye bendi ndogo ndogo  za mitaani.

Mwaka 2001 alimshangaza mmoja wa walimu wake shuleni baada ya kuigiza kuimba kwa ustadi sauti ya mwanamuziki Adjani wa Wenge Musica kwenye wimbo 13ans.

Akiwa mitaani aliambatana na kaka yake, Christian ambaye alikuwa akiimba kwenye kikundi cha mtaani kwao ‘Rue De Son’, akiwa na Nono Fudji, Jules Lelo ‘Eboa Lotin’ na wengine wengi.

Mwaka 2002-2003 baadhi ya vijana aliokuwa nao kwenye bendi ya mtaani kwao walipata shavu la kuchukuliwa na bendi kubwa za Kinshasa, hii ilimpa hasira ya kuzidi kujituma na hatimaye kuziba baadhi ya mapengo ya wanamuziki walioondoka, akiwamo Tutu Callugi, ambaye alikuwa hodari wa kughani.

Rafiki yake, Nono Fudji, baada ya kujiunga na Wenge BCBG alimkutanisha na mwanamuziki mwandamizi wa bendi hiyo, Alain Mpela ‘Afande’, ili aone uwezo wake, bahati mbaya aliambiwa akajifue zaidi.

Hakukata tamaa, badala yake aliendelea kujifua kwenye vikundi tofauti vya muziki vya jijini Kinshasa, kama vile Dakamuda, Laviniora Esthetique na vingine vingi.

Mwaka 2005 alipelekwa tena kwa Alain Mpela kwaajili ya kuangaliwa uwezo wake, hata hivyo, walinzi Mpela walimzuia  kwa madai kwamba bosi wao alikuwa bize na mazoezi ya kujiandaa na shoo, hivyo hawakutaka asumbuliwe.

Fabregas alirudi nyumbani kichwa chini akisikitika kwa yaliyotokea, aliendelea na shule huku wazazi wake wakimuahidi kumruhusu aendelee na muziki kama atafaulu vizuri masomo yake.

Mwaka 2006 alipelekwa na rafiki yake wa zamani kwa Fally Ipupa, wakati anaanzisha bendi yake iliyokuwa na wanamuziki wengi chipukizi kama yeye. Hapa alipata nafasi ya kughani zaidi kuliko kuimba, kipindi chote alichokuwa akijaribiwa Ipupa alikuwa safarini barani Ulaya.

Aliporudi kutoka Ulaya, bendi inapoanza kupiga shoo wanamuziki wapya walikuwa wakitangulia kupanda stejini kabla Ipupa hajafika, anapofika tu wote walikuwa wanashushwa stejini kumpisha ‘bosi’ wao.

Lakini kwa Fabregas ilikuwa tofauti, kwani aliendelea kupewa nafasi ya kuimba na kughani. Hakudumu muda mrefu kwa Ipupa, akaamua kurudi kwenye bendi ya awali, Laviniora.

Mwaka 2007 alichukuliwa na rafiki yake Werrason na kupelekwa katika bendi ya Zamba Pla kwaajili ya  kufanyiwa  majaribio, akisimamiwa na mwimbaji Adjani, kwani Werrason alikuwa safarini barani Ulaya.

Hakufaulu vizuri kwenye majaribio yake na hata Werrason aliporudi hakuna kilichobadilika zaidi ya kumwacha arudi nyumbani akajifue zaidi.

Aliondoka akiwa amekata tama, ingawa marafiki walijaribu kumfariji kwa kumwambia asikate tamaa.

Aliporudi tena Zamba Playa kujaribiwa mambo yalikuwa mazuri, kwani alikubaliwa baada ya kuwaridhisha na  uwezo wake.

Kuanzia hapo Werrason alimkabidhi kwa kiongozi wa bendi, Papy Kakol, ambaye alimchukua na kuishi naye nyumbani kwake pamoja na mwanamuziki Deplick Pomba.

Chanzo cha kuitwa Fabregas

Alipewa jina Fabregas na mwanamuziki Heritier Watanabe, kutokana na kupendelea kuvaa jezi yenye jina la aliyekuwa  kiungo wa timu ya Arsenal, Cesc  Fabregas.

Siku chache baada ya kujiunga na bendi ya Wenge Musica, alisafiri pamoja na wenzake kwenda kupiga shoo nchini Ufaransa.

Mwaka mmoja baadaye alishiriki kurekodi albamu ya ‘Malewa Vol.1’, kisha mwaka 2010 aling’ara tena kwenye tamasha la Pan African, lililofanyika kwenye Uwanja wa Soka wa Stade De France, nchini Ufaransa.

Muda mfupi baada ya tamasha hilo alirejea tena nchini humo kufanya onesho maalumu ambalo mwanamuziki marehemu Papa Wemba alipaswa kushiriki.

Hata hivyo, onyesho hilo halikufanyika, baada ya kuzuiwa na Wakongomani wenye msimamo mkali waishio Ulaya, wanaojulikana kama ‘Combattants’.

Mwishowe alianza kufanya mipango ya siri ya kuiacha Wenge Musica na kuanza kuandaa nyimbo zake binafsi ili akifanikiwa akazirekodi Ulaya kama mwanamuziki huru.

Hatimaye alifanikiwa kwenda Ulaya na kuingia mkataba wa ufadhili na kampuni ya Publicom Studio kwaajili ya kusimamiwa kurekodi albamu yake ya kwanza ‘Amour amour’.

Baada ya albamu yake kutoka ilipokelewa vizuri sokoni na hata aliporudi DRC mwaka 2013 alikuwa  karibu sana na Koffi Olomide, kabla ya  kuingia naye mkataba kwenye albamu ya nguli huyo ya ‘Koffi Central’, kisha wakapiga bonge la shoo kwenye ukumbi wa Grand Hotel, jijini Kinshasa.

Kuanzia hapo ikawa ndio mwanzo wa bifu kali kati yake na bosi wake, Werrason, huku akizidi kuachia ngoma kali kama Anapipo, Mascara na nyingine kibao. Mpaka sasa hivi Fabregas anaendelea kupiga kazi akiwa mwanamuziki huru. Tukutane wiki ijayo.

Email;noahyongoro@gmail.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU