MRITHI WA MSUVA YANGA HUYU HAPA

MRITHI WA MSUVA YANGA HUYU HAPA

8410
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY,

BAADA ya mipango ya winga wa Yanga, Simon Msuva ya kwenda kucheza soka la kulipwa kuiva, uongozi wa timu hiyo umeamua kumpandisha Said Mussa kutoka kikosi chao cha pili ili kuziba pengo lake.

Msuva amepata dili katika klabu ya DHJ ya Morocco na tayari uongozi umekiri kuwa na taarifa hizo, huku ukiweka wazi kuwa muda wowote anaweza kuondoka nchini.

Said amepata nafasi ya kupanda kikosi cha kwanza baada ya kuonesha uwezo katika mashindano ya SportPesa yaliyofanyika mwezi uliopita, jijini Dar es Salaam, ambapo Yanga iliondolewa kwa mikwaju ya penalti na AFC Leopard ya Kenya katika hatua ya nusu fainali.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga zinasema, Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, ambaye alikuwa akifuatilia mashindano hayo kupitia runinga, mara baada ya kurejea Tanzania aliutaka uongozi kumpa nafasi kijana huyo kuchukua nafasi ya Msuva.

“Katika kikao cha Lwandamina na Kamati ya Utendaji pamoja na mambo mengine, aliutaka uongozi kuwapandisha wachezaji wawili, mwingine akiwa ni kiungo namba sita Maka Edward,” alisema mtoa habari wetu.

BINGWA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa, kuzungumzia hilo ambapo alikiri kuwapandisha vijana hao baada ya mapendekezo ya Lwandamina.

“Wapo vijana wawili tumewapandisha ambao ni Said pamoja na Maka ambao walikuwa katika kikosi chetu kile kilichokuwa kikishiriki mashindano ya SportPesa,” alisema.

Wakati huohuo, zoezi la upimwaji wa afya wa wachezaji wa Yanga, limeendelea jana katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salam chini ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA), Nassoro Matuzya, pamoja na Edward Bavu.

Katika zoezi hilo, wachezaji waliojitokeza ni Ibrahim Ajib, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Geoffrey Mwashiuya, Emannuel Martin, Said na Maka ambao wanaungana na Haji Mwinyi, Juma Abdul, Yusuph Mhilu, Amissi Tambwe, Juma Said Makapu, Andrew Vincent, Juma Mahadhi na Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ ambao walishapimwa.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, daktari wa Yanga, Edward Bavu, alisema kuwa Lwandamina ameagiza kila mchezaji kupimwa afya kabla ya kuingia katika kikosi chake.

“Lwandamina ametaka kila mchezaji wa Yanga kabla hajaanza mazoezi naye awe amepimwa afya, hivyo kwa wale ambao hawajajitokeza, tunafikisha taarifa kwa uongozi ambao watajua nini cha kuamua, kwa upande wetu tumetimiza majukumu yetu,” alisema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU