MWAKYEMBE AVUNJA BARAZA LA MICHEZO

MWAKYEMBE AVUNJA BARAZA LA MICHEZO

561
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA,

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, jana amesitisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT), Dioniz Malinzi, sambamba na wajumbe wote wa baraza hilo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwakyembe alisema agizo la Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, kuwa aifanyie mapitio na kuitathmini upya BMT ili kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini, limekuja wakati mwafaka.

“Baada ya hapo niliitisha kikao na BMT, kulielimisha kuhusu wajibu wake kisheria, changamoto zinazolikabili na hali ya uhuru uliopitiliza katika uongozi na uendeshaji wa michezo karibu yote,” alisema.

Mwakyembe alisema pamoja na BMT kulalamikia uhaba wa fedha kuwa kikwazo kikubwa kinachokwamisha utendaji wake, Wizara iliona hitaji la utashi, dhamira na kujituma kuliko fedha katika kutatua sehemu kubwa ya udhaifu uliotamalaki tasnia ya michezo.

“Mifano michache ni viongozi wa michezo kushika zaidi ya nafasi moja ya uongozi, ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania nje ya nchi bila kuitaarifu BMT; mapromota wa michezo ya ngumi nchini kuendesha shughuli zao bila kusajiliwa, chaguzi za vyama vya michezo kugubikwa na ubabe na rushwa, katiba na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki, ubadhilifu, upendeleo na maamuzi ya kibabe ya wazi kabisa kutofuatiliwa na kufanyiwa kazi,” alisema.

Waziri Mwakyembe, alisema kwa sasa Sekretarieti ya Baraza itaendelea kufanya kazi katika kipindi hiki kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara, wakati taratibu za kumpata Mwenyekiti na wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria.

Awali, Malinzi alikalia kiti hicho cha Mwenyekiti wa BMT baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Wajumbe wa kamati hiyo walikuwa ni Jamal Rwambow, Alex Mgongolwa, Jeniffer Mmasi Shang’a na Zainab Mbiro, Zacharia Hans Poppe, Mohammed Bawaziri, Zainab Vullu, Adam Mayingu, Cresscentius Magori na John Ndumbaro.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU