NUH MZIWANDA: SHILOLE HAWEZI KUVUNJA NDOA YANGU

NUH MZIWANDA: SHILOLE HAWEZI KUVUNJA NDOA YANGU

1052
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA,

IDADI ya wasanii waliotangaza kuanzisha lebo za muziki mwaka jana, ilikuwa ni kubwa na miongoni mwao alikuwamo msanii wa Bongo Fleva, Naftari Mlawa ‘Nuh Mziwanda’.

Staa huyu amewahi kugonga vichwa vya habari za burudani pamoja na chati za muziki nchini, kwa singo zake kali kama Otea Nani, Hadithi, Msondo Ngoma, Anameremeta na Jike Shupa ambazo  zilimpa mafanikio.

Mafanikio aliyoyapata kwenye muziki yalimpa wazo la kuwekeza kwenye tasnia hiyo kwa kuanzisha lebo ya muziki inayofahamika kama ‘Last Born Records’.

Safu ya Jiachie na Staa Wako imefanikiwa kumnasa Nuh na kufanya naye mahojiano kuhusiana na harakati zake za muziki. Karibu.

Swali: Ukiwa kama msanii ambaye huna miaka mingi kwenye muziki, kwanini uliwaza kufungua lebo?

Nuh: Nimefungua lebo kwa sababu wasanii wengi wanahitaji kufanikiwa.

Kama mimi nilipotoka ni mbali na nimenyanyuliwa na kusaidiwa na watu hadi hapa nilipofikia, kwa hiyo nimefungua Last Born Records ili kukuza muziki wangu ili hata nikija kustaafu niwe nimefanya kitu kikubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Swali: Lebo yako inamiliki wasanii wangapi na vipi  kuhusu kazi zao.

Nuh: Ina msanii wa kike anaitwa Aisha, ina prodyuza chipukizi ambaye ni mdogo wangu anaitwa Speso, pia  kuna wasanii wengine wawili ambao siwezi kuwataja kwakua  wapo nje ya Dar es Salaam, walinitumia kazi zao nikawasikiliza nikakaa na uongozi wangu tukaona tunaweza kufanya nao kazi.

Kuna nyimbo nyingi za wasanii tofauti tofauti kama Ali Kiba na Aby Skilliz zimerekodiwa pale, siku si nyingi na mimi nitaachia ngoma mpya.

Swali: Ukiwa kama msanii ambaye umeoa, kuna faida au hasara yoyote kwa staa kuoa au kuolewa.

Nuh: Mimi sioni kama kuna hasara  kama kuna misingi uliyojiwekea, kwakua kazi ni kazi na maisha ya kawaida ni maisha.

Kwa hiyo muziki hauwezi kumzuia mtu kuishi vile Mwenyezi Mungu anavyotaka tuishi. Vijana wengi hawapendi kuoa kwa sababu ukweli ni kwamba, utalazimika kuachana na vitu fulani fulani lakini kwangu sioni shida.

Swali: Vipi kuhusu chakula unapendelea kipi.

Nuh: Mimi napenda sana biriani au ndizi na nyama.

Swali: Unapenda kutumia aina gani ya gari.

Nuh: Mimi sipendi makubwa, gari yoyote nzuri mimi natumia tu, ila kwa kifupi napenda kutembelea Harrier.

Swali: Wiki iliyopita ulifanyiwa upasuaji, waambie mashabiki wako ulikuwa unasumbuliwa na nini hasa na hali yako ikoje kwa sasa.

Nuh: Nilikuwa na tatizo la uvimbe mdogo kwenye koo, niliwahi kuutoa mapema ili usije ukaniletea madhara hapo baadaye, kwa sasa niko poa.

Swali: Kuna ukweli wowote kuhusu madai kwamba mpenzi wako wa zamani, Shilole, kuingilia ndoa yako na je, ni kweli umetengana na mke wako Nawal.

Nuh: Shilole hajawahi kuingilia ndoa yangu na hawezi, anabaki kuwa mshkaji wangu, uhusiano wetu unabaki kwenye muziki kwakua sisi ni wanamuziki lakini zaidi ya hapo hakuna baya lolote linaloendelea kila mmoja ana maisha yake.

Kuhusu kuachana na mke wangu si kweli hizi ni stori za kwenye mtandao, kila mtu ana uhuru wa kuongea.

Kifupi tupo pamoja na mtoto wetu Anyagile, kama anaonekana nyumbani kwao ni kwa sababu ya kwenda kuwatembelea tu ingawa sisi ni vijana misukosuko ya hapa na pale ni kitu cha kawaida.

Swali: Nuh Mziwanda ni mwenyeji wa mkoa gani na safari yake ya muziki ilikuwaje.

Nuh: Mimi natokea Mkoa wa Iringa, baba yangu Mbena na mama yangu ni Mkinga, ila kwa bahati nzuri au mbaya mimi nilizaliwa Hospitali ya Amana hapa Dar es Salaam na ndiyo nyumbani kwa wazazi wangu.

Kwenye muziki nilianza kama prodyuza kabla ya kuanza kuimba baada ya kukutana na menejimenti ya Dar Stamina, ambayo pia ilikuwa inamsimamia Shetta.

Nilifanya nayo kazi kwa miaka miwili  kabla ya kuwa solo artist.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU