SIRI UTAJIRI WA LIL WAYNE

SIRI UTAJIRI WA LIL WAYNE

1202
0
KUSHIRIKI

LOS ANGELES, Marekani

KWA sasa, mbali na kuimba na kutunga mashairi ya muziki wa hip hop, ni bilionea na Mtendaji Mkuu wa Kampuni anayoimiliki ya Cash Money Entertainment.

Lakini kufikia mafanikio hayo aliyonayo, haikuwa kazi rahisi, kwani amepitia maisha magumu kabla ya kupata utajiri wake wa sasa unaotajwa na jarida la Forbes la Marekani kuwa unafikia dola milioni 150.

Hapa namzungumzia msanii wa hip hop, Dwayne Carter, baba wa watoto wanne ambaye wengi wanamfahamu kwa jina la Lil Wayne.

Anafahamika kwa mafanikio yake makubwa katika soko la muziki ulimwenguni, ikiwamo kuwa miongoni mwa wasanii waliowahi kuwania na kuchukua tuzo kubwa za BET, Billboard, BIM na Grammy.

Miongoni mwa ngoma zake zilizomweka kwenye ramani ya muziki wa hip hop, ni ‘No Frauds’, ‘Mirror’, ‘Lollipop’, ‘Forever’, Sucker for Pain’ na ‘A Milli’.

Wayne si mmoja kati ya mastaa waliotokea katika familia tajiri. Nitakueleza alivyoupata utajiri wake.

Akiwa na umri wa miaka miwili, Wayne aliyezaliwa Septemba 27, 1982, alikimbiwa na baba yake, Dwayne na hiyo ilitokana na ugumu wa maisha.

Hata alipoulizwa kwanini aliamua kutumia Wayne na si jina kamili la baba yake, alisema aliamua kuiondoa herufi ’D’ kwa kuwa mzee huyo si sehemu ya maisha yake.

­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­­Kwa mazingira hayo, Wayne alilazimika kujituma na hatimaye alirekodi ngoma yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 8, ingawa haukuwa mwanzo wa safari yake ya umaarufu na mafanikio katika muziki.

Je, kwa kuwa alitokea katika familia ya masikini, nini kilichomwezesha Wayne kufanikiwa na kufikia utajiri wa Dola milioni 150 alionao?

Kwanza, Wayne alifanya kile alichokipenda bila kujali jamii ingemzungumziaje. Ikumbukwe kuwa Wayne alikacha shule kwa ajili ya muziki. Alikatisha masomo yake katika Shule ya McMain Magnet na kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 14.

Mwaka mmoja baadaye, alijiunga na Hot Boys akiwa ndiye rapa mdogo zaidi katika kundi hilo. Akiwa na umri wa miaka 18, ndipo alipoanza kutoboa katika soko la muziki kutokana na albamu yake ya ‘The Block is Hot’.

Mafanikio hayo ndiyo yaliyomfanya kuwa karibu na mastaa Drake, Nick Minnaj ambaye anatajwa kuwahi kutoka naye kimapenzi, Dj Khaled na Eminem.

Pili, Wayne hakuwa mwoga wa kutumia njia ngumu katika kuyafikia mafanikio. Aliwahi kukiri katika hilo akisema; “Mimi ni mlevi, ni mlevi wa mafanikio. Ninachoshukuru hakuna tiba ya ulevi wa mafanikio,” aliwahi kusema staa huyo wa hip hop.

Ni ngumu kufanikiwa katika maisha bila kuwa na elimu, lakini Wayne alijitoa sadaka katika hilo na hakurudi nyuma. Aliacha shule akijua wazi elimu ni msingi. Lakini je, nani anayeweza kutabiri kuwa angekuwa na mafanikio aliyonayo ikiwa angeendelea na elimu?

“Ukiamua kuachana na matatizo ya nyuma, unaweza kuijenga kesho yako,” aliwahi kusema mwanamuziki huyo.

Kuthibitisha kuwa kuacha kwake shule hakukuharibu mipango yake ya kimaisha, Wayne aliwahi kuwaambia waandishi wa habari: “Muda unaoupoteza kujilaumu kwa kile ulichopaswa kukifanya, ungeutumia kujenga mipango ya baadaye.”

Mwaka 2005, msanii huyo alijaribu kurudi darasani na kujiunga na Chuo Kikuu cha Houston, lakini ratiba ilimbana kutokana na kazi zake za muziki.

Tatu, Wayne alifanikiwa kwa kuwa alikuwa na kiigizo chake (role model). Ni ngumu kufanikiwa ikiwa hakuna unayefukuzia maendeleo yake. Wayne alikuwa akipambana usiku na mchana kufikia levo za staa wa hip hop, Birdman.

Wayne alikuwa akivutiwa na kazi za Birdman, mwanzilishi wa lebo ya Cash Money Records na aliiga mambo mengi kutoka kwa rapa huyo.

Kutokana na juhudi zake katika kufikia mafanikio ya Birdman, Wayne alisainiwa na Cash Money akiwa ‘dogo’ wa umri wa miaka tisa.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi pamoja kwa miaka mingi, kwa sasa wawili hao ni chui na paka. Wayne amekuwa akimtaja bosi wake huyo zamani kuwa ni mnyonyaji.

Washikaji hao walishawahi kutwangana walipokutana studio mwaka 2015 na ilielezwa kuwa Birdman alipoteza meno mawili katika varangati hilo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU