MAANDALIZI… TIZI LA YANGA USIPIME

MAANDALIZI… TIZI LA YANGA USIPIME

4423
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, hataki masihara kabisa katika maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kukipigisha tizi la kufa mtu kikosi chake.

Lwandamina, akiwa na wasaidizi wake, Noeli Mwandila, Juma Pondamali na Shadrack Nsajigwa, waliwahenyesha wachezaji hao kwa muda wa saa mbili, kuanzia saa 3:00 hadi 5:00 asubuhi, katika ‘gym’ iliyopo eneo la Akiba, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Wachezaji hao walianza kwa mazoezi ya kupasha na kunyoosha viungo, baada ya hapo waliingia kwenye hatua nyingine ya kukimbia katika mashine maalumu na kunyakua vitu vizito ili kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa timu hiyo, Hafidhi Saleh, alisema kwa mujibu wa ratiba ya kocha, wataendelea na mazoezi ya ‘gym’ kwa muda wa wiki nzima, ili kuwaweka sawa wachezaji wao kabla ya kuanza rasmi harakati za kujenga kikosi cha ushindani.

“Kwa mujibu wa Lwandamina, wachezaji watafanya mazoezi ya ‘gym’ kwa muda wa wiki nzima, kabla ya kurejea uwanjani au ufukweni, lengo kubwa ni kuiweka miili ya wachezaji katika hali ya utayari kwa kuwa walikuwa mapumziko,” alisema.

Pia meneja huyo alizungumzia kuonekana kwa mchezaji mmoja wa kigeni kwenye mazoezi hayo, ambaye ni Amis Tambwe.

“Mchezaji pekee ambaye hajarejea Tanzania ni Donald Ngoma na anatarajiwa kuingia nchini kesho usiku (leo) na ataungana na wenzake Ijumaa (kesho), lakini Thaban Kamusoko na Obrey Chirwa tayari wameshafika,” alisema Hafidhi.

Katika mazoezi ya jana, wachezaji waliohudhuria ni pamoja na mshambuliaji Ibrahim Ajib, Pius Buswita na Abdallah Hajji, ambao ni wapya kwenye kikosi hicho na kiungo mkabaji kutoka timu ya Cotton Sports  ya Cameroon, Fernando Bonnyang, aliyekuja kufanya majaribio.

Wengine ni Juma Abdul, Tambwe, Geofrey Mwashiuya, Emanuel Martin, Andrew Vincent ‘Dante’, Juma Mahadhi, Said Makapu, Mwinyi Haji, Yusuph Mhilu, Maka Mwakalukwa, Said Juma na Pato Ngonyani.

Yanga, ambao wanataraji kutetea taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu unaokuja, walianza rasmi mazoezi yao juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na wanatarajia kukutana na mahasimu wao, Simba, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 19, mwaka huu.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU