AVEVA, KABURU WARUDISHWA RUMANDE

AVEVA, KABURU WARUDISHWA RUMANDE

694
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA,

KESI ya madai ya utakatishaji fedha inayowakabili viongozi wa Simba, Rais Evance Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, imeahirishwa hadi Julai 20, mwaka huu.

Kesi hiyo iliahirishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, kwa kuongozwa na mawakili wa upande wa Jamhuri na wale wa Takukuru kufuatia upelelezi wa kesi hiyo kushindwa kukamilika.

Wakili wa Jamhuri, Christopher Msigwa, aliiomba Mahakama kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Kufuatia ombi hilo, upande wa utetezi ambao una mawakili watatu wakiongozwa na wakili, Evodius Mtawala uliiomba Mahakama hiyo kuharakisha upelelezi kwa kuwa washtakiwa wapo ndani, huku kesi inayowakabili ikiwa ni ya mwaka 2016.

“Hili kosa linalotajwa ni la mwaka 2016, hivyo tunaomba upande wa Jamhuri iharakishe upelelezi kwa kuwa tayari washtakiwa wapo ndani mpaka sasa,” alisema.

Hakimu Nongwa aliliridhia maombi hayo yaliyowasilishwa na upande wa utetezi  na kuwataka upande wa mashtaka kufanya hima kukamilisha upelelezi huo.

“Hii ni kesi ambayo makosa yake hayana dhamana, hivyo lazima washtakiwa wapate haki zao, fanyeni hima upelelezi ukamilike ambapo mtarudi tena hapa  Julai 20, mwaka huu,” alisema Hakimu Nongwa.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walipandishwa kizimbani Juni 29, mwaka huu, wakikabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya kutakatisha fedha na kughushi nyaraka.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha Dola za Marekani 300,000; zaidi ya Sh milioni 650 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba ambazo zilitokana na mauzo ya mchezaji, Emannuel Okwi kutoka klabu ya Esperance ya Tunisia.

Washtakiwa wote walirudishwa rumande hadi Julai 20, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU