BAO LA ROONEY LAWEKA REKODI DAR

BAO LA ROONEY LAWEKA REKODI DAR

969
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU,

Wayne Rooney ametumia dakika 35 kwenye nyasi za Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kufunga bao lake la kwanza tangu arejee Everton Jumapili ya wiki iliyopita.

Bao hilo la Rooney alilolifunga jana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, limeacha rekodi lukuki nchini Tanzania.

Rooney amerejea Everton baada ya kuondoka kwenye klabu hiyo Merseyside mwaka 2004 na kutua Manchester United, alikocheza miaka 13 akifunga mabao 183 katika mechi 393.

Katika mchezo huo ambao Everton walishinda mabao 2-1 na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, Rooney aliweka rekodi ya kufunga bao lake la kwanza kwenye Uwanja wa Taifa tangu arejee kwenye klabu yake hiyo ya Everton.

Katika dakika ya 35, nahodha huyo wa England alipokea pasi kutoka kwa Ademola Lookman na kuangalia wa kumpasia kabla ya kuamua kupiga shuti la umbali wa yadi 30, ambalo lilimpita mlinda mlango wa Gor Mahia, Boniface Oluoch.

Bao hilo la kwanza tangu arejee Everton, limelinganishwa na lile aliloifungia klabu hiyo ya Goodison Park mwaka 2002 akimtungua mlinda mlango wa Arsenal, David Seaman na timu yake kushinda 2-1, akiwa na umri wa miaka 16 na kukatisha rekodi ya mechi 30 za Gunners bila ya kufungwa.

Pia tukio hilo la kufunga bao lake la kwanza kwenye Uwanja wa Taifa limelingana na lile la kiungo wa zamani wa Chelsea, Ramires, alilofunga kwenye uwanja huo alipokuwa ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Brazil mwaka 2010.

Pamoja na tukio hilo la kufunga bao lake la kwanza Uwanja wa Taifa la umbali wa yadi 30, lakini kitendo cha kuvamiwa na shabiki na kukumbatiwa kinarandana na kile kilichomkuta kiungo wa Brazil, Kaka, ambaye alivamiwa na shabiki mwaka 2010 katika uwanja huo.

Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na Jacques Tuyisenge aliyeisawazishia Gor Mahia dakika ya 37 na mchezo kwenda mapumziko ukiwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili kocha wa Everton, Ronald Koeman, alifanya mabadiliko ya wachezaji 11, akimpumzisha Rooney na mchezaji mpya, Davy Klaassen, huku winga Aaron Lennon akicheza mechi yake ya kwanza tangu Februari 11, mwaka huu baada ya kusumbuliwa na ugonjwa unaotokana na msongo wa mawazo.

Mchezaji mwingine mpya, Michael Keane, alicheza kipindi cha pili baada ya kusajiliwa kutokea Burnley na mpira wake wa kichwa ulimfanya Dominic Calvert-Lewin afunge bao ambalo lilikataliwa kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea.

Kieran Dowell aligongesha mwamba kwa mpira wake wa adhabu kabla ya baadaye, dakika tisa kabla ya mchezo kumalizika kufunga bao kwa mguu wa kushoto kwa umbali wa yadi 25 na kuibuka na ushindi huo wa 2-1.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU