DUNIA YA MKE WANGU (30)

DUNIA YA MKE WANGU (30)

653
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Julia alishindwa amjibu Rebeca nini. Kilio kikubwa kilimvamia. Alishuka upesi kwenye gari na kumkumbatia Rebeca kwa nguvu.

 “Nitaipeleka nakuahidi,” aliongea Julia maneno mawili yaliokuwa faraja aliyokuwa nayo kwa dakika hizo.

Baada ya kuachana, alipanda kwenye gari huku akiwatazama Dora, Khadija na Zuwena waliokuwa wamesimama kwenye lango la kanisa pamoja na mapadre wakitokwa na machozi mengi. Hakika huzuni ilikuwa imetawala sehemu ile.

SASA ENDELEA

VILAN aliwasha lori na kuliondoa pale kanisani. Wakati wakiliacha kanisa, Julia alikuwa akiwatazama Dora na wenzake kupitita saitimila.

Lori lilishika njia ya vumbi iliyokuwa ikielekea katikati ya kijiji. Bado huzuni haikukauka usoni na kwenye mioyo yao. Julia alifungua begi lake na kuchukua simu yake ya mkononi. Aliiwasha na kukutana na picha ya mume wake aliyoiweka kama skrini seva. Moyo wake ulishtuka, huzuni iliongezeka zaidi tone jipya la chozi lilimtoka na kudondokea kwenye simu. Tabasamu zuri la mume wake ndilo lililompa maumivu makali zaidi. Moyoni alijisemea.

“Mume wangu nisamehe, kwa kosa nililofanya. Sikupaswa kuja katika nchi hii tena nikiwa mjamzito na mbaya zaidi nimekuficha mume wangu na nimekudanganya. Usiponisamehe, nitakubali adhabu utakayonipa, maana nina stahili.”

Vilan akiwa anaendesha gari, aligeuka kumtazama Julia, aliyemkuta akiwa na mawazo ya mbali huku akitokwa na machozi.

“Julia punguza kulia sahau tuliyoyaacha nyuma,” aliongea Vilan.

“Vilan ni maumivu makali sana ambayo nayahisi. Ni vigumu kuyaelezea.”

“Natambua Julia lakini hebu jikaze kiume.”

“Ni vigumu Vilan, kumbuka wale ni Watanzania wenzetu hawakupaswa kubaki kwenye ardhi hii. Tutawaambia nini ndugu zao.”

“Ni kweli Julia, lakini  ndio imeshatokea hatuna budi kuikubali hali iliyopo.”

Baada ya maongezi hayo, ukimya ulitawala, Vilan aliendelea kukanyaga mafuta akiendesha lori taratibu na kwa tahadhari.

“Samahani Julia naomba kukuuliza,” aliongea Vilan.

Julia hakujibu lolote zaidi alilisubiria swali kutoka kwa Vilan.

“Kwanini mumeo alikuruhusu uje Ethiopia, tena ihali kuwa ni mjamzito?”

Swali hilo lilimuumiza Julia. Alimgeukia Vilan na kumjibu.

“Hili ni kosa ambalo nimelifanya mimi. Mume wangu hajui lolote.”

“Unamaana gani unaposema hajui si umemuacha nyumbani?”

“Vilan siku zote umekuwa ukiniona katika majonzi, huzuni wasiwasi na machozi ni kwa sababu hiyo. Mume wangu yuko London kwa sasa. Nilitamani kuwasaidia watoto wa kijiji cha Keneza pindi nilipowaona kwenye taarifa ya habari. Nilipenda kuja kutoa huduma, kwa sababu nilitamani niwe sehemu ya msaada kwa Waafrika wenzangu. Hivyo niliondoka pasipo kumtaarifu mume wangu, nikijua kuwa lazima asingekubaliana na uamuzi wangu.”

“Mmh kweli Julia hukupaswa kufanya hivyo. Mumeo anaitwa nani?”

“Kai Luda.”

“Kai Luda?”

“Ndio.”

“Yule mwanasayansi?”

“Nadhani unamfahamu, Waafrika wengi wanamtambua.”

“Ni kweli namfahamu kumbe wewe ni mkewe?”

“Ndio bila shaka.”

“Aisee siamini kumbe nimefanya kazi na mke wa mtu mashuhuri kama yule,” aliongea Vilan pasipo kuamini.

Wakiwa wanaendelea na maongezi hayo lori lilikuwa likipita katikati ya kijiji, eneo lililokuwa na shughuli nyingi za biashara kipindi ambacho Ebola haijashika kasi. Kulikuwa na watu wachache sana katika mitaa yote, maiti nyingi zilikuwa zimezagaa kila mahali. Watu wanaougua ugonjwa huo walikuwa kila sehemu. Hata wanyama pia walikuwa na maambukizi.

Lori likiwa linasonga mbele, walikutana na kundi la watu. Watu hao walionekana ni wale wenye maambukizi ya hatua ya kwanza ambao wanauwezo wa kufanya kazi yoyote ngumu. Walikuwa wamebeba mapanga na silaha nyingine za jadi. Walipoliona lori likipita barabarani, walianza kulifukuzia, wakitaka kuwakamata Julia na wenzake na kisha kuchukua lori pamoja na mali walizokuwa nazo. Hofu ilitanda kwa Julia na wenzake. Vilan aliongeza mwendo ili watu hao wasilifikie.

“Vilan ongeza mwendo wanakuja,” aliongea Julia akiwatazama watu hao kupitia saitimila.

Vilan alifaulu kulikimbiza lori hadi barabara kuu ambao aliongeza mwendo na kuwaacha nyuma kabisa watu wale. Wote walishusha pumzi na kutazamana. Julia alifungua dirisha dogo ambalo humuwezesha mtu aliye mbele ya lori kutazama nyuma ya lori, ambako kulikuwa na wale wauguzi wanne.

“Jamani mko salama?” aliuliza Julia.

“Tuko salama,” alijibu kijana mmoja wa kiume.

Julia alianza kuwajawa na hofu juu ya wale wenzake waliokuwa wamewaacha kanisani. Aliinamisha kichwa chini, akitamani kurudi nyuma. Kwa kuwa watu waliokuwa wamelikosa lori lao, alijua lazima watakwenda kanisani ambako wapo Dora na wenzake.

“Vilan geuza gari turudi,” aliongea Julia huku akitokwa na machozi.

“Una wazimu?” Aliuliza Vilan huku akimshangaa Julia.

“Naomba ugeuze gari, wenzetu watakumbwa na matatizo makubwa zaidi. Wale watu lazima watakwenda kanisani.”

“Julia hatuna jinsi ni lazima tusonge mbele. Kama unataka kuiona Tanzania, fikiri jambo lijalo si lililopita,” aliongea Vilan huku akiongeza gia.

Julia hakuwa na jingine la kujibu alibaki kuinamisha kichwa chini, maana maneno ya Vilan yalivunja nia yake ya kutaka kurudi nyuma kuwasaidia wenzake waliobaki kanisani. Machozi yalizidi kumbubujika, maana alijua jambo baya zadii litawakuta Rebeca na wenzake.

Lori likiwa lizidi kuziacha nyumba za watu, mbele walimuona mtoto mdogo akiwa amelala katikati ya barabara. Julia alimsihii Vilan asimamishe gari asije kumkanyaga yule mtoto. Vilan alifunga breki, lori lisimama karibu kabisa na mtoto. Kabla Vilan hajamkataza Julia kushuka,  Julia alishakuwa ameshashuka kitambo.

Alivaa kofia yake vizuri kwa kujiziba uso vema, alipiga hatua hadi pale alipokuwa amelala yule mtoto. Alimshika na kumuamsha. Mtoto yule aliinua kichwa na kumtazama Julia usoni. Damu nyingi zilikuwa zikimtoka kila sehemu ya matundu ya mwili wake. Miguu yake ilishakuwa imeanza kuoza. Julia alitokwa na machozi, huruma kubwa ilimshika. Aliona kama yule ni mtoto wake. Alitazama pande zote, hakuwa na mtu yoyote mahali pale.

Mtoto huyo alikuwa akilia kwa maumivu makali huku akilalamika kuwa njaa ilikuwa ikimuuma. Julia alirudi kwenye gari ambao alichukua chakula cha kopo, kabla hajashuka Vilan alimwambia.

“Chukua sindano ya Reeb ukamchome ndipo umpe chakula.”

Sindano ya Reeb ilikuwa ni sandano yenye sumu, ambayo mtu akichomwa hulala na baadae hupoteza maisha.

“Kwanini Vilan,” aliuliza Julia kwa mshangao.

“Hatuwezi kuondoka na huyo mtoto pili hatuwezi kumuacha peke yake akiwa hai. Hadi muda huu ameshateseka sana. Ni vema apumzike.”

Julia aliona kuwa alichokisema Vilan kilikuwa ni cha kweli. Alimfuata yule mtoto akambeba hadi kando ya barabra na kumkalisha chini ya mti. Akampa kile chakula cha kopo. Mtoto alikipokea na kuanza kula kwa pupa, ikionyesha kuwa hakuwa amekula kwa zaidi ya siku tatu. Akiwa anakula, Julia alimchoma ile sindano ya sumu. Wakati akimchoma nafsi yake ilikuwa ikiumia kupita kiasi.

Baada ya kumchoma, alirudi kwenye lori. Vilan aliwasha gari na kuliondoa. Julia alimtazama yule mtoto kupitia saitimila, akiwa anakula huku taratibu usingizi ukimchukua ambapo baadaye angepoteza maisha.

Lori lilizidi kusonga mbele. Baada ya masaa matatu lilikuwa likiingia mji wa Amhara. Na kwa muda huo tayari lilikuwa kwenye barabara ya lami. Mji huo nao ulitawaliwa na ukimya, watu wachache walionekana kwenye mitaa ya mji huo. Baadhi ya maiti zilikuwa bado zikionekana mitaani. Magari machache yalikuwa yakipita.

KANISANI, KENEZA

Kundi la watu waliokuwa na maambukizi na wasio na maambukizi, walilivamia Kanisa Katoliki, hii ilikuwa ni baada ya kufanikiwa kuwaua wanajeshi wawili waliokuwa wakililinda kanisa hilo, kanisa lililokuwa msaada mkubwa wa kuhifadhi misaada ya chakula na wauguzi wanaokuja kwenye kijiji hicho.

Baada ya kuwaua wanajeshi hao waliokuwa na maambukizi ya Ebola, waliingia kanisani na kuwakuta Dk Dora, Rebeca, Khadija na Zuwena pamoja na watumishi wa kanisa.

Zaidi ya watu 40 walikuwa wameingia mle ndani. Waliwashikia mapanga  wote, hofu ilitanda ndani ya kanisa hilo. Amani ndogo iliyokuwa imebaki nayo ilitooweka, kwani watu hao walikuwa na hasira wakiugulia maumivu makali ya njaa.

Walianza kuingia kwenye kila chumba cha kanisa na kuchukua kila kitu, mali zote za Dora na wenzake zilichukuliwa. Padre mkubwa wa kanisa alimfuata kiongozi wa kundi hilo.

“Ndugu yangu kwanini mnafanya haya. Kumbekeni kila mtu katika kijiji hichi anahitaji msaada,” aliongea padre akimtazama mtu huyo.

Mtu huyo hakujibu lolote zaidi aligeuka pembeni na kumgeukia tena padre.

Nini kitafuatia usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU