USAJILI UZINGATIE MASLAHI KWA WACHEZAJI, KLABU

USAJILI UZINGATIE MASLAHI KWA WACHEZAJI, KLABU

1167
0
KUSHIRIKI

KLABU za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili Tanzania Bara, kwa sasa zipo katika mchakato wa usajili wa wachezaji ambao unatarajiwa kufungwa Agosti 6, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa timu ambazo hazitakamilisha usajili, kama ilivyotokea msimu uliopita.

Dirisha la usajili huanza kwa kipindi cha kutangaza wachezaji walioachwa au kusitishiwa mikataba ili kutoa nafasi kwa klabu kufanya usajili mpya.

Wakati shabiki akisubiri kwa hamu kuona mchezaji gani anakwenda wapi na akina nani wanabaki kwenye timu zao, macho na masikio yataelekezwa kwa wale waliong’ara msimu uliopita kuona kama watabaki kwenye klabu zao au kuhama.

Katika hilo, tayari baadhi ya timu zimeanza kuanika majina ya wachezaji zinaotarajia kuwasajili, iwe ni kwa kuwaongezea mikataba wale walionao au kunasa wengine wapya kutoka kwingineko.

Miongoni mwa ambao tayari wametikisa soko la usajili ni Haruna Niyonzima wa Yanga ambaye inadaiwa amejiunga Simba kwa dau nono, ingawa klabu hiyo haijamtangaza rasmi.

Mwingine ni Ibrahim Ajib, ambaye ameikacha Simba na kujiunga na Yanga, huku wengine kadhaa wakiwa wamezihama timu zao za zamani katika kile kilichoonekana kupigania maslahi.

Bingwa tunapenda kuwakumbusha wachezaji, hasa waliomaliza mikataba, kuwa hiki ni kipindi muhimu mno kwao, kwani ndicho  kinachoweza kuwaboreshea maslahi yao.

Katika hilo, ni vema wakafahamu kuwa kwenye soka hakuna suala la mapenzi na timu, kinachoangaliwa ni maslahi tu.

Pia ifahamike kuwa, mchezaji anaposhuka kiwango, hakuna shabiki wa timu atakayetamani kumwona zaidi ya kumzomea uwanjani.

Ukiachana na hilo, ni vema viongozi wa klabu  wakawa makini katika kipindi hiki cha usajili kwa kuhakikisha wanasajili wachezaji kulingana na mapendekezo ya makocha wao.

Uzoefu unaonyesha kuwa, mara nyingi kuna viongozi wa klabu za soka hapa nchini, hasa zile kongwe za Simba na Yanga, ambazo zimekuwa zikisajili wachezaji kwa maslahi yao binafsi, bila kuzingatia matakwa ya kocha na timu zao.

Mwisho wa siku, wachezaji wanaosajiliwa hugeuka kuwa mzigo kwa klabu, kama tulivyojionea msimu uliomalizika, ambapo wapo waliosajiliwa kwa mbwembwe na fedha lukuki, lakini hakuna lolote la maana walilolionyesha uwanjani.

Tumalizie kwa kuzitakia kila la heri klabu katika kipindi hiki cha usajili, pia wachezaji ambao tunaamini hawatafanya makosa, ikizingatiwa kufanya hivyo kunaweza kugharimu soka na maisha yao kwa ujumla.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU