YANGA SC HAITANIWI

YANGA SC HAITANIWI

12312
0
KUSHIRIKI

ZAINAB IDDY NA LEONCE GODFREY (UDSM)

WAKATI mashabiki wa Simba wakiwa na matumaini ya kumwona Haruna Niyonzima akitambulishwa rasmi kama mchezaji wao mpya Julai 23, mwaka huu, kibao kinaelekea kugeuka baada ya Yanga kukubali kumrejesha kundini nyota wao huyo.

Yanga ilitangaza kuachana na Niyonzima baada ya kushindwa kufikia makubaliano kuhusu kuongeza mkataba mpya, sababu ikitajwa ni dau kubwa alilohitaji mchezaji huyo.

Kutokana na hilo, Simba waliingilia kati na kukubaliana na kiungo huyo ili atue Msimbazi kwa dau lililotajwa Sh milioni 100, ambapo mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewij ‘MO’, ndiye bosi aliyesimamia ‘shoo’ ya Niyonzima kuhamia Msimbazi kwa kukubali kutoa kitita cha Sh milioni 130 alizohitaji Mnyarwanda huyo.

Lakini wakati wadau wa soka wakiamini Niyonzima ni mali ya Simba msimu ujao kutokana na madai ya kiungo huyo kumalizana na Mo, lakini ghafla kuna taarifa kuwa Mnyarwanda huyo ameghairi na ameomba mwenyewe kubaki Jangwani.

Taarifa ambazo BINGWA limezinasa kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Yanga, zinasema Niyonzima ameamua kuwaangukia mabosi wake hao wa zamani na kutaka kuendelea kufanya nao kazi, huku akiwa tayari kupewa hata Sh milioni 70.

“Niyonzima anarudi Yanga, kwani yeye mwenyewe ndiye kaomba ingawa kulikuwa na mabishano, wengine wakikataa kumrejesha lakini mwisho wa siku, tumekubaliana kumpa nafasi kwa mara nyingine kutokana na mchango wake mkubwa tangu ajiunge nasi.

“Baada ya kutuomba tumrejeshe, tulimweleza hatuna uwezo wa kumpa kiasi alichotaka wala kile tulichomwambia awali (Sh milioni 90), hivyo amekubali kurudi kwa Sh milioni 70, hivyo suala lake limeshamalizika kwani Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussen Nyika, alikwenda Rwanda hivi karibuni na kukutana naye,” kilisema chanzo chetu cha uhakika.

Kubaki kwa Niyonzima Yanga kunaweza kuchochea mtindo maarufu wa uchezaji uliobatizwa jina la ‘kampa kampa tena’, ambao baadhi ya wachezaji wa timu hiyo waliutumia msimu uliopita zaidi ukiwahusisha viungo na washambuliaji.

Kwa kuwa Niyonzima ndiye aliyekuwa ‘monita’ wa mtindo huo, kubaki kwake na ujio wa Ibrahim Ajib Jangwani ambaye naye si haba katika suala zima la pasi maridadi, utanogesha zaidi na kuendelea kutoa burudani kwa mashabiki wao.

Lakini wakati suala la Niyonzima likifika patamu, Yanga wameamua kuiliza Simba kwa mara nyingine baada ya kumpandia ndege beki Mganda, Jjuuko Murushid kuziba nafasi moja iliyobaki ya wachezaji wa kigeni.

Taarifa ambazo BINGWA linazo zinasema kuwa, Yanga wameamua kuisaka saini ya Jjuuko ili kuziba nafasi ya beki wao raia wa Togo, Vicent Bossou, ambaye wameachana naye.

Lakini pia, imeelezwa kuwa Yanga wamepata beki kutoka Nigeria ambaye amefichwa katika moja ya hoteli jijini Dar es Salaam.

BINGWA limefanikiwa kukutana na Katibu wa Yanga, Charles Mkwassa aliyekataa kutoa ufafanuzi juu ya usajili wa timu yake, lakini akiweka wazi kuwa hivi sasa suala  hilo linafanywa na Nyika kwa kuzungumza na wachezaji waliopendekezwa na kocha ndipo yafike mezani kwake kwa ajili ya kukamilisha usajili.

“Masuala yote ya usajili hivi sasa yapo chini ya Nyika, kwangu inakuja ripoti juu ya wapi amefikia katika mazungumzo yake na wachezaji waliohitajika na benchi la ufundi, hivyo tusubiri akileta kama watakuwamo hao wanaotajwa tutaweka wazi,” alisema.

Kwa sasa Yanga ina wachezaji watano wa kigeni ambao ni Mzimbabwe Donald Ngoma, Amiss Tambwe (Burundi), Thaban Kamusoko (Zimbabwe), Obrey Chirwa (Zambia) na Youthe Rostand (Cameroon), hivyo kubakia nafasi mbili za kutimiza idadi ya wachezaji saba wa kigeni wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za usajili za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU