UZIKWASA WAJA NA TAMTHILIA YA TAMAPENDO

UZIKWASA WAJA NA TAMTHILIA YA TAMAPENDO

399
0
KUSHIRIKI
Baadhi ya washiriki wa tamthilia ya redio ya Tamapendo iliyoandaliwa na shirika la UZIKWASA

NA HASSAN BUMBULI


SHIRIKA la Uzikwasa ambalo limejipatia umaarufu katika uandaaji wa filamu za uelimishaji hapa nchini, limeendelea na mpango wake wa kutumia sanaa kama njia ya kufikisha ujumbe kwa jamii.

Shirika hilo lenye makao yake Mtaa wa Jamhuri, mjini Pangani, mkoani Tanga, hivi sasa limeandaa tamthilia ya redio inayofahamika kwa jina la Tamapendo, ambayo imetengenezwa katika studio za redio Pangani na itarushwa kupitia kituo cha Redio Pangani Fm 107.7 kinachomilikiwa na shirika hilo.

“Tamthilia hii ni mwendelezo wa jitihada za Uzikwasa katika kujenga jamii bora ya watu wa Pangani, ni tamthilia iliyojaa mafundisho mengi na inaonyesha changamoto za masuala mbalimbali yaliyopo kwenye jamii ya Afrika,” anasema Ofisa Habari wa Uzikwasa, Mohammed Hammie.

Anasema lengo la tamthilia hii ni kuonesha changamoto za unyanyasaji wa kijinsia katika jamii, ikiwa ni mwendelezo wa masuala nyeti na muhimu ambayo yamekuwa yakifanyiwa na shirika hilo.

Tamapendo inakuwa tamthilia ya pili ya redio kutengenezwa na Uzikwasa baada ya Penye Nia ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa katika uelimishaji wa jamii ya watu wa Pangani.

Tamthilia hii inahusisha hadithi ya vijana wawili Fatuma na Chaballa, ambao wamelemewa na mambo mazito yanayotokana na hali ya ukatili wa kijinsia na dhuluma ya haki za msingi kwa wasichana na wanawake.

Ni  mchezo unaoonyesha harakati za vijana hao kukabiliana na changamoto hiyo iliyoigubika jamii yao ambao umetokana na utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa jamii ya watu wa Pangani.

Pamoja na tamthilia hizo za redio, Uzikwasa imepata umaarufu mkubwa katika uandaaji wa filamu za uelimishaji, filamu ya kwanza ilikuwa ni Fimbo ya Baba iliyotengenezwa mwaka 2006 na kushinda tuzo mbalimmbali ikiwamo tuzo ya filamu bora ya Afrika Mashariki. Filamu hiyo ilizungumzia changamoto za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na ndoa za utotoni.

Filamu ya pili ilikuwa Chukua Pipi iliyotoka 2012 na ya tatu ni Aisha ya mwaka 2015, ambayo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa hata katika anga za kimataifa na kunyakua tuzo mbalimbali kutoka matamasha maarufu ya filamu Afrika na Marekani.

Tamthilia ya filamu zote za Uzikwasa hushirikisha wasanii wengi kutoka wilayani Pangani na kwa tamthilia ya Tamapendo, imeongozwa kwa ushirikiano wa waongozaji mahiri wa filamu na michezo ya kuigiza hapa nchini, Chande Omar na Irene Sanga.

Tamthilia hiyo mbali ya kuwa na mazingira ya Kipangani, lakini ujumbe wake ni mtambuka kwa taifa zima kwani masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na unyimi wa haki za msingi kwa watoto wa kike, ni hali inayoikabili jamii nzima ya Tanzania.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU