HEBU ICHEKI ‘FIRST ELEVEN’ YA BEI KALI DUNIANI

HEBU ICHEKI ‘FIRST ELEVEN’ YA BEI KALI DUNIANI

1255
0
KUSHIRIKI

LONDON, England


USAJILI wa Kyle Walker kwenda Manchester City umemfanya mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham kuwa beki wa kulia aliyenunuliwa kwa fedha nyingi katika historia ya mchezo wa soka.

Beki huyo ametua Etihad kwa ada ya Pauni milioni 50 na amesaini mkataba wa miaka mitano kuwa chini ya mkufunzi Pep Guardiola.

Hata hivyo, licha ya kuongoza kwa mabeki wa kulia, Walker si mchezaji pekee kusajiliwa kwa fedha nyingi kwenye soko la usajili.

Hebu cheki ‘first eleven’ hii inayoundwa na wachezaji ambao usajili wao uligharimu fedha nyingi.

Ederson (Benfica –Man City)

Ederson ndiye kipa ghali zaidi duniani kwa sasa baada ya kuhamia Etihad kwa Pauni milioni 34.7. Alitua England mwezi uliopita akitokea Ureno na amesaini mkataba wa miaka mitano.

Anatarajiwa kuwa mlinda mlango namba moja mbele ya Claudio Bravo, ambaye alinaswa kwa Pauni milioni 17 akitokea Barcelona.

Kyle Walker (Tottenham – Man City)

Kabla ya usajili wa Walker, Fabio Coentrao aliyetua Real Madrid mwaka 2011 akitokea Benfica, ndiye aliyekuwa beki wa kulia aliyenunuliwa kwa fedha nyingi.

Madrid walimnasa kwa Pauni milioni 27 lakini sasa Man City wametumia takribani mara mbili ya kiasi hicho kumpata Walker ambaye pia anaingia kwenye ‘first eleven’ hii na kucheza nafasi hiyo ya beki wa kulia.

David Luiz (Chelsea – PSG)

Anapokuwa katika safu ya ulinzi hasa eneo la beki wa kati, amekuwa akifanya vizuri na usajili wake wa kutoka Chelsea kwenda PSG kwa Pauni milioni 50 unampa tiketi ya kuingia kwenye first eleven hii.

Alikuwa sehemu ya Chelsea kilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, likiwa ni taji la 12 katika historia ya timu hiyo yenye masikani yake Magharibi mwa Jiji la London.

John Stones (Everton -Man City)

Ni mmoja kati ya mabeki bora wa kati, hivyo anastahili kucheza eneo hili kwenye kikosi hiki.

Wakati wa majira ya kiangazi yaliyopita, Everton walifanya biashara nzuri kwa kumuuza Stones kwenda Man City ambapo waliweka mfukoni Pauni milioni 50.

Baada ya kusaini mkataba wa miaka sita na amecheza mechi 23 za Ligi Kuu katika msimu wake wa kwanza.

Luke Shaw (Southampton – Man United)

Anapata bahati ya kuwa beki wa kushoto wa kikosi hiki kutokana na usajili wake wa bei kali kutoka Southampton kwenda Man United.

Man United walilipa Pauni milioni 28 kumchukua mchezaji huyo na mpaka leo anabaki kuwa beki ghali wa upande wa kushoto.

Angel Di Maria (Madrid – Man United)

Winga wa kulia atakuwa ni Di Maria aliyetua Man United kwa ada ya Pauni milioni 59.7 akitokea Real Madrid, ingawa baadaye aliondoka Old Trafford na kutua PSG kwa ada ya Pauni milioni 44.3.

Anaingia kwenye ‘first eleven’ hii kwa uhamisho wake huo wa bei kali kutoka Man United kwenda Ufaransa.

Paul Pogba (Juve – Man United)

Atakuwa kiongozi wa safu ya kiungo wa kati katika ‘first eleven’ hii. Mfaransa huyo ndiye anayeongoza kwa kununuliwa kwa fedha nyingi kwenye historia ya soka.

Pogba alitua Man United akitokea Juventus na usajili wake wa mwaka jana uligharimu Pauni milioni 93.25.

James Rodriguez (Monaco – Madrid)

Eneo la kiungo wa kati litakuwa pia na Rodriguez. Alisajiliwa na Madrid akitokea Monaco na hiyo ilitokana na uwezo wa juu aliouonyesha akiwa na timu yake ya Taifa ya Colombia kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.

Baada ya kuchemsha Madrid ambayo aliigharimu Pauni milioni 63 kumnasa,  amepelekwa Bayern Munich kwa mkopo wa miaka miwili.

Gareth Bale (Tottenham – Madrid)

Kwa Pauni milioni 85 walizotoa Madrid mwaka 2013, Bale anaingia kwenye kikosi hiki na kupewa winga ya kushoto. Ikumbukwe kuwa Bale ameifanya Tottenham kuwa klabu pekee ya Uingereza kupata fedha nyingi kwa mauzo ya mchezo mmoja.

Kwa sasa anatajwa kuwa mbioni kuondoka Bernabeu na kwa umri wake wa miaka 27, ni wazi klabu itakayomtaka italazimika kujipanga kuinasa huduma yake.

Gonzalo Higuain (Napoli – Juve)

Katika kikosi hiki, Lukaku atalazimika kusubiri katika safu ya ushambuliaji kwani amenunuliwa kwa Pauni milioni 75 pekee huku Higuain akiwa ameigharimu Juve Pauni milioni 75.3 kumng’oa Napoli.

Msimu uliopita wa Seria A, Higuain aliifungia Juve mabao 24 na aliiwezesha timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Cristiano Ronaldo (Man United – Madrid)

Ndiye mshambuliaji atakayeshirikiana na  Higuain katika kikosi hiki. Ronaldo ndiye mshambuliaji anayeshikilia rekodi ya kununuliwa kwa mpunga mrefu hadi leo hii, licha ya kuwa ni miaka nane imepita tangu alipotua Madrid akitokea Man United kwa Pauni milioni 80.

Ronaldo amekuwa akihusishwa kuondoka Bernabeu lakini kwa klabu itakayomhitaji, ni wazi italazimika kuvunja kipengele cha mkataba wake wa sasa kinachoitaka Madrid kulipwa Pauni bilioni moja.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU