KILA MMOJA NI MZURI ILA ANAYEFAA NI HUYO ULIYE NAYE SASA

KILA MMOJA NI MZURI ILA ANAYEFAA NI HUYO ULIYE NAYE SASA

761
0
KUSHIRIKI

 

KILA binadamu ana vitu ambavyo mwingine hana. Katika vitu hivyo ndipo vipo vyenye kufurahisha sana na vipo vyenye kukera sana. kwako mwenzako ni bora sana kuliko mtu mwingine kwa sababu ana vitu ambavyo abadani huwezi kuvipata kwa mwingine.

Unajua ni kwanini watu husalitiana sana? Mbali na sababu nyingi ambazo hutolewa, mimi leo nakupa moja ambayo huonekana zaidi katika jicho la kitaalamu.

Sababu hii ni ile ya watu kudhani akitoka kwa mtu aliye naye sasa atapata furaha zaidi kwa mtu mwingine. Hii fikra imewafanya wengi kuhangaika katika mahusiano na mwisho kushindwa kupata kitu stahili.

Kama nilivyosema mwanzo kila mtu ana vitu fulani tofauti ambavyo mwingine hana. Watu wengi walio katika mahusiano hudhani wale watu wengine wawaonao mtaani ambao hawana mapungufu fulani walio nayo wenzi wao, basi wakiwa nao wataienjoy zaidi kwa kuwa zile kero ambazo huletwa na wenzao wao hawana.

Wakati wakiwaza hivi huwa wanasahau kuwa japo wenzao huwa na kero na udhaifu Fulani, ila pia kuna mambo mengi mema wao wanayo na wengine hawana.

Fikra za namna za kutaka furaha zaidi katika mapenzi bila kujua asili hasa za tabia za binadamu, huwafanya wahusika wayaangalie zaidi mambo mazuri ya wanaotaka kuanzisha nayo uhusiano na kusahau katika hayo mazuri pia kuna udhaifu mkubwa wenzao wanao, ila hawawezi kuuona katika hatua za mwanzo kwa sababu kila mmoja huwa katika tahadhari na mwenzie.

Unataka kuachana na mwenzako? Sawa. Sasa umejipanga kuishi na nani ambaye hana udhaifu? Nani ambaye ukiwa naye atakufanyia kila unachaotaka na kuacha kila usichotaka? Nani?

Akili ya binadamu hupenda kuamini kuwa sehemu aliyopo ni mbaya zaidi kuliko anayotaka kwenda. Hisia hizi ziko kila mahali.

Na ndiyo maana wengi huona kazi za wengine ni nyepesi zaidi, nzuri zaidi na zenye maslahi zaidi. Fikra hizi hujidanganya hivi kwa sababu ya ugeni na upya wa jambo husika katika utendaji wao.

Kuanzia leo amini kila unayemwona anapita basi anakabiliwa na changamoto nzito katika mahusiano yake. Kuzishinda hizi changamoto ni kufunua akili yako na kuona kuwa kila mtu yuko sawa sana eneo fulani na hayuko sawa sana eneo jingine. Kuwaza kuwa mtu fulani atakuhakikishia furaha, amani na raha kila siku si tu unajidanganya, ila pia unajiweka katika hali ambayo kila siku utakuwa unahangaika katika safari ya mahusiano yako.

Njia nzuri ya kufurahia mahusiano yako ni kumsoma na kumwelewa mwenzako. Ni kujua kuwa udhaifu wake unaweza kupambana nao katika njia kuu mbili.

Njia ya kwanza  ni kurekebisha madhaifu yanayoweza kurekebishika toka kwake na njia ya pili nai kujifunza kukubaliana na madhaifu mengine unayohisi ni asili yake na ni ngumu kupambana nayo.

Kusema kuwa utapata mtu mwenye kukujali zaidi, kukupenda zaidi, kukusikiliza zaidi, kukulindia heshima zaidi, mwenye kutumia muda mwingi na wewe zaidi kuliko uliye naye, si tu unawaza mambo magumu sana kutokea ila ni kitu ambacho kitakufanya ubadili wapenzi kila kukicha na usimpate.

Ifahamike katika mahusiano ya kimapenzi, kitu muhimu zaidi si kuwa na mtu mwenye kukujali na kukufanyia kila kitu unachotamani kufanyiwa, hapana. Kwanza mtu huyo hayupo. Kitu muhimu ni kuishi na huku mkifunzana.

Uishi naye huku mkikoseana na kuombana msamaha kwa dhati. Muishi kwa kusomana na kujua namna ya kufanya ili mjenge muunganiko bora wenye kuleta amani na furaha katika mahusiano yako.

Ili mahusiano yaweze kuwa bora kila mmoja inabidi akubali kupoteza kitu ili apate kitu. Yaani sio kila utakalo upate ila ni muhimu wewe upate mengi utakayo na yeye apate mengi apendayo. Ila yote haya yawe katika misingi ya heshima na thamani.

Sio katika kukomona wala kuoneshna nani zaidi kwa mwenzake. Jifunze kuwa msikivu, mnyenyekevu na mwenye busara. Jifunze kuelewa na kuomba msamaha.

Jifunze kuheshimu mamuzi ya mwenzako na kumuelewa kwa dhati. Kwa kufanya hivi unakuwa unatengeneza mahusiano bora na yenye heshima.

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU