KWANINI JUVENTUS WAMEMUUZA BONUCCI?

KWANINI JUVENTUS WAMEMUUZA BONUCCI?

471
0
KUSHIRIKI

MILAN, Italia


BAADA ya kuwanasa wachezaji saba kwenye soko la usajili wa majira haya ya kiangazi, AC Milan imeushtua tena ulimwengu wa soka kwa kumbeba na beki wa Juventus, Leonardo Bonucci, kwa uhamisho uliogharimu euro milioni 40.

Wengi walishindwa kuelewa kwanini mmoja wa mabeki bora na muhimu duniani aliyesaidia kuunda ukuta imara katika klabu ya Juve, aliruhusiwa kuondoka ghafla tena kwa kujiunga na mahasimu wa timu yake ya zamani.

Kuna wengine wanaobeza uhamisho huo kuwa beki huyo ameiacha timu iliyonyakua mataji sita ya Serie A na yenye uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwenda timu itakayoshiriki Ligi ya Europa.

Lakini ukitazama mabeki wa Ulaya waliowahi kununuliwa kwa bei ghali, David Luiz kwenda Chelsea (euro mil.50), Man City wakitumia euro milioni 128 kwa John Stones, Nicolas Otamendi na Eliaquim Mangala na hakuna anayeufikia uwezo wa Bonucci.

Lakini, ni kipi hasa kilichosababisha beki huyo atimkie Milan?

Bifu

Sababu kuu ya kuondoka kwa Bonucci ni kutoelewana na kocha wa Juve, Massimiliano Allegri.

Katika mchezo wa Serie A baina ya Juve na Palermo uliomalizika kwa wababe hao wa Turin kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1, Bonucci na Allegri walionekana kujibizana vikali.

Hata wakati wenzake wanafurahi pamoja na mashabiki mara baada ya mchezo huo kumalizika, Bonucci aliamua kuondoka zake na kwenda vyumbani baada ya tukio hilo hakupangwa kweye mchezo uliofuatia wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Porto.

Kufuatia mzozano huo, kwa pamoja walikubaliana wayamalize kwa faida ya timu. Na Bonucci alishapanga kuondoka ifikapo majira ya kiangazi.

Kwanini Milan?

Bado swali jingine litaibuka, kwanini asingeenda Ligi Kuu England kama tetesi zilivyokuwa zikidai kwamba Chelsea na Man City walishajipanga kutoa ofa kuzidi ya Milan?

Hata Juve wasingependa kuona nyota wao akihamia kwa mahasimu, lakini sababu kubwa ya kubaki Italia ni ya kifamilia zaidi.

Mtoto wa kiume wa Bonucci anaumwa mno hivyo hakutaka kwenda mbali na mwanawe na timu pekee iliyoonesha dhamira ya kumsajili ni Milan.

Itakuwaje kwa Juve?

Hakuna hata mmoja mwenye wasiwasi na kuondoka kwa Bonucci, kwani hata msimu uliopita Allegri aliwahi kunukuliwa akisema anatafuta suluhisho la kubadili ukuta wake ulioundwa na wazee kama Dani Alves mwenye umri wa miaka 34, Bonucci (30), Giorgio Chiellini (32) na Andrea Barzagli (36), jumla wakiwa na umri wa miaka 132.

Kuondoka kwa Bonucci na Alves kutamfanya Allegri sasa aweze kutoa nafasi kwa beki mwenye kipaji murua, Daniele Rugani (22) ambaye ataweza kuziba pengo la Bonucci.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU