PACQUIAO: MBWA WAKE KUFANYWA MSOSI KULIMKIMBIZA NYUMBANI

PACQUIAO: MBWA WAKE KUFANYWA MSOSI KULIMKIMBIZA NYUMBANI

575
0
KUSHIRIKI

 

LONDON, England


 

PRESHA kubwa aliyonayo bondia Manny Pacquiao, ni kuwathibitishia mashabiki wake kuwa hajakwisha licha ya kupoteza pambano lake la hivi karibuni dhidi ya Jeff Horn.

Mwanamasumbwi na mwanasiasa huyo wa Ufilipino, ameomba kurudiana na Horn aliyemdunda kwa pointi katika pambano hilo la Shirikisho la Ngumi Duniani (WBO).

Inasemekana kuwa wawili hao watarudiana Novemba mjini Melbourne, Australia na tayari promota Bob Arum amethibitisha kuwa atafika Ufilipino wiki ijayo kuzungumza na Pacquiao juu ya mpango huo.

Kitendo cha staa huyo kupoteza pambano hilo la raundi 12, limewashtua wadau wengi wa ngumi ambao wamemtaka kutangaza kuachana na mchezo huo.

Hata hivyo, ingawa alipoteza kwa pointi mbele ya Horn, bado Pacquiao anabaki kuwa mmoja wa mabondia wenye mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa masumbwi.

Hata katika pambano hilo, Pacquiao alimtupia lawama mwamuzi Mark Nelson kutoka Marekani, akisema alimbeba mpinzani wake huyo. “Hakuna tatizo juu ya aina ya uchezaji wa ovyo wa Jeff, mwamuzi alikuwapo.

“Tatizo ni kwamba, sijui mwamuzi alifanya makusudi au hakuwa na uzoefu. Aliruhusu (rafu) na wala hakutoa onyo. Ni kama mwamuzi alitaka kumsaidia mpinzani wangu,” alisema Pacquiao.

Mbali na masuala yake ya siasa akiwa ni mbunge nchini kwao Ufilipino, amekuwa akiingiza fedha nyingi kutokana na mapambano yake.

Hata hivyo, hadithi ilikuwa tofauti miaka mingi iliyopita akiwa kijana mdogo nchini Ufilipino.

Akiwa na umri wa miaka 12, Pacquiao alikuwa mmoja wa vijana wanaoishi maisha magumu katika Jimbo la General Santos, nchini Ufilipino.

Halikuwa jambo la kushangaza kwa Pacquiao na wazazi wake kulala njaa, ilikuwa ni sehemu ya maisha yake kabla ya utajiri alionao sasa.

Hata mchezo wa ngumi ulikuja tu baada ya kushindwa kuendelea na shule kutokana na umasikini wa wazazi wake na ni mjomba wake aitwaye Sandro Mejia, ndiye aliyempeleka huko.

Kutokana na hali mbaya kiuchumi, siku moja baba yake aliamua kumchinja mbwa wa Pacquiao na kumfanya msosi wa usiku.

Jambo hilo lilimkera mno mwanamasumbwi huyo na ndipo alipoamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi mitaani.

Akiwa huko, Pacquiao alijiingiza katika harakati za kusaka kipato kwa kuuza mikate na kuna kipindi alikuwa akipanda ulingoni na kupata kiasi kidogo cha fedha.

Baadaye, aliamua kukimbilia mjini Manila ambako aliweza kupata dili la kufanya kazi katika moja ya ‘gym’ akiwa mtunza bustani.

Akiwa hapo, alitumia muda mwingi pia kufanya mazoezi na mara kadhaa aliweza kupata nafasi ya kuzichapa na mabondia kutoka Korea Kusini, Japan na Thailand.

Safari ya mafanikio aliyonayo leo hii ilianza pale aliposhinda ubingwa wa dunia akiwa na umri wa miaka 19 baada ya kumchakaza Chatchai Sasakul, aliyekuwa akilitetea taji hilo la WBC.

Siku chache kabla ya kupanda ulingoni kuzichapa na Horn, aliposti picha iliyomwonyesha akiwa anagawa fedha kwa watoto wa nchini Ufilipino.

Picha hiyo iliyokuwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, ilikuwa na maelezo yaliyosomeka: “Ndiyo maana bado napigana.”

Bingwa huyo wa dunia mara nane ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 38, ameonekana kutilia maana suala la kustaafu akisema anapaswa kusikiliza ushauri wa wengi.

“Nazingatia pia ushauri wa watu, familia yangu na hata mwili wangu,” alisema Pacquiao baada ya kurudi Ufilipino.

“Nimepanga kutulia kwanza na kupona majeraha ya mwilini mwangu na baada ya hapo, ndipo nitakapofikiria kwa makini kuhusu hilo.”

Mke na mwalimu wa mwanamasumbwi huyo wameweka wazi kuwa watamshawishi kuachana na mchezo huo baada ya kuutumikia kwa kipindi kisichopungua miaka 22.

Baada ya kupigwa na Floyd Mayweather, Pacquiao alijipa mapumziko marefu kwa ajili ya mambo yake ya kisiasa ambapo aliweza kuchaguliwa kuwa mbunge na aliporejea ulingoni alimdunda Jessie Vargas.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU