PIGO USAJILI WA SIMBA

PIGO USAJILI WA SIMBA

9413
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY


FURAHA za mashabiki na wanachama wa Simba kuhusu usajili wa nyota kadhaa uliofanywa, umeanza kuingia dosari baada ya wachezaji hao kubainika kuwa wagonjwa.

Simba imefanya usajili wa nyota kadhaa   kutoka kwa mabingwa wa Afrika Mashariki, Azam FC, ambao ni kipa namba moja Aishi Manula, beki wa kulia Shomari Kapombe na mshambuliaji tegemeo John Bocco.

Lakini taarifa za uhakika ambazo BINGWA limezipata ni kwamba, Kapombe amejitonesha tatizo lake la nyonga katika dakika ya 13 baada ya kuchezewa rafu na Mico Justin wa timu ya taifa ya Rwanda, wakati anaitumikia timu yake ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars mechi iliyochezwa CCM Kirumba na kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).

Pamoja na Kapombe, lakini pia Bocco licha ya kucheza imeelezwa kwamba hayuko fiti na hivyo anahitaji kufanyiwa matibabu ya uhakika ili apone kabisa na kuwa fiti kuitumikia Simba.

“Kapombe ndiyo hivyo amejitonesha, Bocco kama unakumbuka hata msimu uliopita hakucheza mechi nyingi kwa sababu ya kuwa majeruhi, naye hajakaa vyema anahitaji kuendelea na matibabu,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba.

Akizungumza na BINGWA, Daktari wa Taifa Stars, Richard Yombo, alisema kwa sasa Kapombe yupo chini ya uangalizi wa madaktari mkoani  Mwanza kwa muda wa masaa 72, baada ya kumalizika kwa mchezo kabla ya kufanyiwa vipimo kuona kama ataweza kuendelea kuitumikia Stars au arejeshwe Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

“Hakuumia kwa maana ya kupata jeraha la kushona, ila amejitonesha matatizo yake aliyowahi kuwa nayo hivyo ndani ya masaa 72 tutakuwa tumejua iwapo ataweza kuendelea kuambatana na timu kwenye mechi ya marudiano au kurejea Dar es Salaam kuangalia jinsi gani atatibiwa.

“Hivi sasa tutaendelea kumpa huduma za hapa na pale kwa muda huu atakaokuwa huku ili kumrejesha kwenye hali yake ya kawaida, ikitokea tatizo likawa kubwa tunaweza kumsafirisha kabla ya huo muda,” alisema.

Kapombe  alikuwa akitumiwa mara kwa mara nje ya nchi na klabu yake ya Azam, huku Bocco akikosa mechi kadhaa za mwishoni mwa msimu kutokana na kuwa majeruhi na kama wataendelea kuwa majeruhi wataigharimu Simba ambayo imewasajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na mechi za kimataifa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU