POLE NOURI: JANGA ALILOPATA LIMEUSIKITISHA ULIMWENGU WA SOKA, SI AJAX TU

POLE NOURI: JANGA ALILOPATA LIMEUSIKITISHA ULIMWENGU WA SOKA, SI AJAX TU

827
0
KUSHIRIKI

AMSTERDARM, Uholanzi


TAARIFA zilizotoka kuhusu kinda la miaka 20 la klabu ya Ajax, Abdelhak Nouri, kuwa kilichomfanya aanguke uwanjani wiki iliyopita ni tatizo la ubongo, zimeitikisa klabu yake hiyo.

Baada ya kinda huyo kupewa huduma ya kwanza uwanjani hapo wakati Ajax ilipokuwa ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Werder Bremen na ikaonekana anahitaji huduma ya kihospitali zaidi, taarifa zaidi zikathibitisha Nouri hatacheza tena soka.

Ulimwengu wa soka ukapatwa na huzuni baada ya taarifa hiyo. Kijana mdogo mwenye ndoto za kuwa staa mkubwa, ghafla anapata tatizo linalozima ndoto zake mithili ya upepo uzimavyo mshumaa mmoja katikati ya msitu mnene!

Tatizo lililozima ndoto za Nouri kitaalamu linaitwa ‘cardiac arrhythmia’. Ni mshtuko ambao pindi unaposhambulia moyo, huweza kusababisha matatizo makubwa ikiwamo kuharibu baadhi ya sehemu za mwili wa binadamu kama vile ubongo kama janga lililompata Nouri.

Ni habari mbaya sana kwa klabu ya Ajax na mashabiki wake, kwani watakosa huduma ya mchezaji huyo mwenye kipaji, ufundi mkubwa akiwa na mpira.

Ni ngumu kuamini kijana mdogo kama huyo anakumbwa na tatizo kubwa linalofuta kila kitu kuhusu soka kichwani mwake, ni ngumu kuamini tabasamu lake litaonekana kwa nadra.

Nouri maarufu kama ‘Appie’, alikuwa mchezaji anayependwa sana na kocha wake, Marcel Keizer, wakongwe wa Ajax na wachezaji wenzake pia.

Si wafanyakazi wenzake tu, bali hata mashabiki tayari walishapagawa na uwezo wake.

Kwa sasa atakuwa hashangiliwi tena uwanjani, bali atakuwa akipewa pole zisizo na kipimo ili aweze kurudi kwenye hali yake ya kawaida ingawa kaka yake, Abderrahim Nouri, haamini kama mdogo wake atarudi tena uwanjani.

“Madaktari wanaamini atarudi vizuri ila nimekuwa mzito kuamini kama ataweza kufikiri vyema, kula, kutembea au hata kutambua watu. Sijui yaani,” alisema Nouri.

“Lakini hatukati tamaa, Mungu ataamua hatima yake. Dini yetu inatufundisha kukubaliana na yote na tunamuombea awe na afya njema. Tunafahamu kuwa haya maisha ni mafupi, tutaishi tena baada ya hapa lakini najua kila mtu angependa kumuona akifunga mabao uwanjani.”

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, klabu ya Ajax iliamua kusitisha mazoezi na kuwataka wachezaji wake kujitokeza na kuzungumzia wanachofikiri juu ya mwenzao. Ndani ya wiki nzima iliyopita mawazo ya Waholanzi yalikuwa ni juu ya Nouri.

“Nouri ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, hatukujua ni kwa muda gani angeng’ara kama si hilo tatizo lililomkumba,” alisema Edwin Van der Sar, Mkurugenzi mkuu wa Ajax.

Nouri ni nuru iliyozimika ghafla kwa upande wa Ajax. Alikuwa kijana mwenye roho nzuri, kipaji cha asili na akiwa na umri wa miaka mitano tu tayari alishaanza kuwaacha mashabiki wa Ajax midomo wazi kwa jinsi alivyokuwa akipanda kiwango siku hadi siku.

Vitu vilivyomtambulisha kinda huyo ni chenga za maudhi, kasi na ufundi wake wa kuuchezea mpira, alikuwa na jicho kali la kuona wapi pasi ipenyezwe, upigaji pasi wake ulikuwa na mbwembwe kama vile pasi nyepesi za kutanguliza au za kuinua au visigino.

Licha ya ufupi wake (sentimita 170), Nouri alikuwa mgumu kukabika kutokana na kontroo yake nzuri na uwezo wa kugeuka kwa kasi akiwa na mipira kwenye msitu wa mabeki na baada ya hapo hutengeneza nafasi kwenye eneo hilo hilo bila watu kutegemea kama angeweza kufanya hivyo.

Aidha, Nouri alikuwa mzuri kwenye mipira ya kutenga, mashuti ya mbali na ‘muvumenti’ zake ndani ya 18 zilikuwa ni balaa, akiweza kufunga mabao 10 akiwa na timu ya akiba ya Ajax (Jong Ajax) Ligi Daraja la Pili Uholanzi sambamba na kutoa pasi 11 za mabao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU