SASA SPORTPESA KUZIPAISHA SIMBA, YANGA MPAKA ITALIA

SASA SPORTPESA KUZIPAISHA SIMBA, YANGA MPAKA ITALIA

2585
0
KUSHIRIKI

NA JONATHAN TITO


BAADA ya kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa kufanikiwa Kenya, England na sasa Tanzania, safari hiyo ya mafanikio imetinga nchini Italia.

Kampuni hiyo ya SportPesa ambayo imedhamini Chama cha Rugbi cha Kenya, pamoja na klabu za Gor Mahia na AFC Leopards kwa upande wa Kenya.

Kwa England ni moja wa wadhamini wa klabu za Arsenal na Southampton, huku wakiwa wadhamini wakuu wa Hull City na Everton.

Tanzania wamedhamini klabu za Simba, Yanga na Singida United, huku udhamini huo ukionyesha kuleta mafanikio makubwa nchini kwa muda mfupi kwa upande wa soka na hata utalii, baada ya kuileta klabu ya Everton wiki iliyopita.

Ujio huo wa Everton umetoa fursa kubwa kwa Tanzania kujitangaza kiutalii na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soka zaidi baada ya nyota wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kufanya hivyo kwa kupata nafasi ya kuichezea  K.R.C. Genk ya nchini Ubelgiji.

Sasa wawekezaji hao wamepiga hodi nchini Italia, baada ya kupata hisa za umiliki wa kampuni ya michezo ya kubashiri ya RCS ya Italia ambayo inamilikiwa na kampuni mama ya RCS Media Group.

Kampuni hiyo ya kubashiri ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa upande wa michezo hiyo ya kubashiri kwa miaka mingi nchini Italia, imekuwa ikifanya kazi kwa kutumia jina la GazzaBet.

“Hii ni hatua nyingine kubwa katika harakati za kuendelea kuifanya SportPesa kuwa kampuni kubwa duniani,” alisema.

Mwenyekiti mteule wa Bodi ya SportPesa Italia, Adam Beighton, alipokuwa akizungumzia taarifa hizo za SportPesa kuingia Italia.

“Kupata hisa kwenye kampuni ya michezo ya kubashiri ya RCS kutawezesha kampuni kukua kwa kasi nchini Italia na itatoa fursa mpya kwetu kutangaza utamaduni wetu kama SportPesa kwa wateja wetu wa sasa na wa baadaye,” alisema mwenyekiti huyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa SportPesa nchini Tanzania, Pavel Slavkov, alifunguka kuhusiana na habari hizo za kampuni hiyo kuingia Italia, akisema nchi hiyo ina soko kubwa la michezo ya kubashiri katika Bara la Ulaya.

“SportPesa ina furaha kubwa kutanua wigo wake kibiashara katika nchi ya Italia, ambayo imekuwa ni soko kubwa la michezo ya kubashiri Ulaya,” alisema Slavkov.

“Kuiongeza Italia kwenye orodha yake ya utendaji ni mafanikio makubwa, huku tukitazamia kuboresha huduma kwa wateja wetu waliomo nchini humo na kuzifanya kuwa za kiwango cha daraja la juu zaidi,” aliongeza Slavkov.

Kwa sasa RCS Media Group wataendelea kuwa wamiliki wa hisa wa kampuni hiyo kwa asilimia chache, huku wakisubiria kuona jinsi washirika wao watakavyoongeza soko hilo la biashara ya kubashiri.

Kupanuka kwa wigo huo wa utendaji kwa SportPesa hautakuwa na mafanikio kwa kampuni hiyo pekee, bali itazibeba hata klabu wanazozidhamini.

Kama ilivyokuwa Everton kutua nchini Tanzania, basi kupanuka kibiashara kunaweza kuiwezesha klabu ambazo zimedhaminiwa na SportPesa nchini na kwingineko kama Simba, Yanga na Singida United kupata fursa ya kwenda kucheza michuano ambayo inaweza kuandaliwa na kampuni hizo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU